Kupimwa mate kunaweza kusaidia “kubadili mkondo” wa saratani ya tezi dume, kwa mujibu wa wanasayansi nchini Uingereza.
Vipimo hivyo huchambua vinasaba (DNA) vya wanaume ili kubaini wale waliozaliwa wakiwa na hatari kubwa ya kuugua saratani ya tezi dume.
Kwa kuwalenga wanaume hao kufanyiwa vipimo vya kutoa sampuli ya mate ili kupimwa kwa maabara na uchunguzi wa MRI, wanasayansi wameweza kugundua baadhi ya aina hatari za saratani ambazo zingepuuzwa pasipo dalili za wazi.
Hata hivyo, jaribio hilo bado halijathibitishwa kuwa lina uwezo wa kuokoa maisha, na wataalamu wanatahadharisha kuwa huenda ikachukua miaka kadhaa kabla ya vipimo kama hivyo kuanza kutumika kwa kawaida katika huduma za afya.
Kila mwaka, takriban wanaume 12,000 hufariki kutokana na saratani ya tezi dume nchini Uingereza.
Wito wa kuanzishwa kwa uchunguzi wa mara kwa mara kwa wanaume wenye afya njema – maarufu kama upimaji wa saratani – umekuwa mkubwa zaidi, hasa baada ya bingwa wa baiskeli wa Olimpiki, Sir Chris Hoy, kutangaza kuwa ana saratani ya hatua ya mwisho ya tezi dume.
Hapo awali, upimaji wa kawaida ulitupiliwa mbali kutokana na kasoro za kipimo kilichopo sasa, ambacho hupima viwango vya protini maalum ya tezi dume (PSA) kwenye damu.
Profesa Dusko Ilic wa Chuo Kikuu cha King’s College London amesema matokeo ya utafiti huo ni ya “kuahidi”, lakini jaribio hilo linaongeza ugunduzi wa saratani kwa kiasi kidogo tu linapotumiwa pamoja na viashiria vya hatari vilivyopo kama umri, viwango vya PSA na uchunguzi wa MRI.
Aidha, Profesa Ilic ameongeza kuwa bado hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa jaribio hilo linaongeza muda wa kuishi au kuboresha maisha ya wagonjwa, hivyo kuna haja ya kufanya tafiti zaidi.
Utafiti huo kwa sasa umejikita kwa watu wa asili ya Ulaya pekee, na juhudi zinaendelea kulibadilisha ili liweze kutumika kwa watu kutoka asili nyingine.
Inasadikiwa kuwa wanaume wenye asili ya Kiafrika wako katika hatari mara mbili zaidi ya kuugua saratani ya tezi dume.
Timu ya watafiti pia imeeleza kuwa kuna maswali yanayohitaji kujibiwa kuhusu ufanisi wa gharama, madhara yanayoweza kujitokeza, na muda muafaka wa kuchambua hatari hiyo.
Jaribio la mate sasa limeingizwa katika utafiti mkubwa unaoitwa Transform, unaolenga kubaini mbinu bora ya kuanzisha mpango wa upimaji wa saratani ya tezi dume nchini Uingereza.
0 Comments