TAZAMA IBADA YA KKKT DAYOSISI YA IRINGA HAPA
Askofu Gaville: Tuilinde Amani, Tuombee Taifa Katika Kipindi Hiki cha Uchaguzi Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa, Dkt. Blaston Gaville, amewataka Wakristo na Watanzania kwa ujumla kulinda tunu za taifa na kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na amani ya nchi, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Askofu Gaville aliyasema hayo wakati wa ibada ya Pasaka iliyofanyika katika Usharika wa Kanisa Kuu Cathedral Iringa, na kubainisha kuwa mwaka huu wa 2025 Tanzania itakuwa katika zoezi la uchaguzi mkuu, hivyo ni vyema Wakristo na Watanzania kwa ujumla kuelekeza maombi yao kwa ajili ya taifa ili uchaguzi uwe wa amani.
Aidha, Askofu Gaville aliwahimiza Watanzania kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi pindi muda utakapowadia, ili kuonyesha ukomavu wa kidemokrasia. Vilevile, aliwasihi wanasiasa kufanya kampeni kwa amani ili kuendeleza mshikamano uliopo.
“Niwaombe Wakristo popote mlipo, na Watanzania kwa ujumla, tukumbuke kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi. Tunatakiwa tuzidishe maombi kuhakikisha tunapita salama bila vurugu. Katika miezi hii ambayo Rais Samia bado yupo madarakani, tumkabidhi kwa maombi ili aendelee kuidumisha amani. Tumeshuhudia mengi aliyoyafanya katika miaka minne ya uongozi wake, ikiwemo kuilinda amani ya taifa,” alisema Askofu Gaville.
Pia, aliwataka Wakristo na Watanzania kupiga vita vitendo vya ukatili wa aina yoyote, ambavyo vinaendelea kushamiri na kuwaumiza zaidi watoto na wanawake. Alisema kuwa mara nyingi wanaume hususan ndugu wa karibu wamekuwa watendaji wakuu wa vitendo hivyo vya kikatili.
Alitoa wito kwa familia kujiweka katika maombi ili ziwe msingi wa watu bora, wenye hofu ya Mungu, kwani kufanya hivyo kutasaidia kutokomeza ukatili katika familia na jamii kwa ujumla.
“Tuendelee kuombea familia zetu ziwe na ustaarabu, upendo na hofu ya Mungu. Tukishirikiana kwa pamoja tutatokomeza ukatili na kuliepusha taifa letu na aibu. Familia zikishikamana, upendo utaongezeka na ukatili utapungua,” aliongeza Askofu Gaville.
Aidha, aliwakumbusha Wakristo na Watanzania kuhusu hali ya mvua isiyoridhisha katika msimu wa kilimo uliopita. Alisema kuwa ni muhimu kwa wale waliopata mazao kuyahifadhi, na wale ambao hawakubahatika, waanze kutafuta chakula mapema na kuweka akiba.
0 Comments