Header Ads Widget

SHIRIKA LA SOS CHILDREN'S VILLAGES LAZINDUA BARAZA LA WATOTO MANISPAA YA IRINGA




 Na Zuhura Zuheri  Iringa

Katika jitihada za kuhakikisha haki na wajibu wa mtoto vinatekelezwa, Shirika la SOS Children's Villages kwa kushirikiana na Manispaa ya Iringa limezindua Baraza la Watoto. Baraza hilo linalenga kutoa elimu na kusaidia kufichua vitendo vya ukatili dhidi ya watoto katika jamii.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Maendeleo wa Mkoa wa Iringa, Grace Simalenga, ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliwataka maafisa maendeleo kushirikiana wanapotoa elimu mashuleni na maeneo mengine ili kuwasaidia watoto na jamii kwa ujumla kupata sehemu salama ya kutoa taarifa za ukatili.

"Watoto wanapaswa kufundishwa jinsi ya kutambua vitendo vya kikatili na kuwa na ujasiri wa kutoa taarifa pale wanapokutana na aina yoyote ya dhuluma. Mara nyingi wanatishiwa ili wasiseme, hivyo ni muhimu kuweka ukaribu na watoto ili waweze kuripoti bila hofu," alisema Simalenga.




Kwa upande wake, Afisa Miradi wa Shirika la SOS Children's Villages, Benson Lwakatare, alisisitiza kuwa watoto wanapaswa kufahamu haki na wajibu wao ili kukabiliana na vitendo vya ukatili.

"Mtoto anapaswa kuelewa haki na wajibu wake kwa mzazi wake, na wazazi pia wanapaswa kutambua majukumu yao ili kuwalea watoto katika mazingira salama na yenye malezi bora," alisema Lwakatare.

Afisa Dawati la Msaada wa Kisheria na Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Iringa, Bakari Mzee, alieleza kuwa sheria za nchi zinamtaka mzazi kutekeleza wajibu wa kumlinda na kumtunza mtoto. Aliongeza kuwa iwapo mzazi atashindwa kutekeleza majukumu hayo, sheria itasimama kumsaidia mtoto huyo.

Afisa kutoka Dawati la Jinsia na Watoto wa Mkoa wa Iringa, Stephano Wasira, aliwahimiza watoto kutoa taarifa za ukatili bila woga.




"Watoto wengi wanakumbana na ukatili lakini wanatishiwa ili wasiripoti. Nataka kuwaambia, hao wanaowatishia ni waongo. Njooni dawati la polisi au kwa walimu wenu, serikali ipo kwa ajili ya kuwalinda," alisema Wasira.




Uzinduzi wa Baraza hilo pia ulihusisha uchaguzi wa viongozi wa watoto kwa mwaka mmoja. Waliochaguliwa ni Mwenyekiti Lucy Sogoti,Makamu Mwenyekiti:Danian Mamba ,Katibu Elizabeth Mayanga na Mtunza Hazina: Steven Mauve

Baraza hilo litaongozwa na kaulimbiu isemayo: "Muimarishe Mtoto Kuwa Kiongozi Bora."

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI