Header Ads Widget

TRA YAKUSANYA TRILIONI 7.53 JANUARI HADI MACHI 2025

Na Thobias Mwanakatwe 

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh.Trilioni 7.53 katika kipindi cha robo tatu ya mwaka wa fedha (Januari hadi Machi) 2024/2025 .

Kamishina Mkuu wa TRA,Yusuph Mwenda, amesema hayo jana (Aprili 3, 2025) katika taarifa yake kwa umma kuhusu ukusanyaji mapato kuanzia Julai hadi Machi katika mwaka wa fedha wa 2024/2025.

  Amesema makusanyo hayo ni sawa na ufanisi wa asilimia 101.32 ya lengo la kukusanya Sh.Trilioni 7.43 sawa na ukuaji wa asilimia 13.47 ukilinganisha na Sh.Trilioni 6.63 zilizokusanywa mwaka wa fedha wa 2023/2024.

"Makusanyo yaliyokusanywa katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha wa 2024/2025  yamefanya TRA kuweza kuweka rekodi ya kipekee katika utekelezaji wa majukumu yake kwa kufikia na kuvuka lengo la makusanyo kwa miezi sita mfululizo katika mwaka wa fedha," amesema katika taarifa hiyo.

Mwenda amesema kwa ujumla katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Machi mwaka wa fedha wa 2024/2025 TRA imefanikiwa kukusanya jumla ya  Sh.Trilioni 24.05 sawa na ufanisi wa asilimia 103.62 ya lengo la kukusanya Sh.Trilioni 23.21.

Amesema makusanyo hayo kwa kipindi hicho ni sawa na ukuaji wa asilimia 17.01 ukilinganisha na kiasi cha Sh.Trilioni 20.55 na kwamba makusanyo hayo ni kiwango cha juu kabisa kufikiwa na TRA  kwa kipindi kama hicho toka kuanzishwa kwa mamlaka hiyo.

"Makusanyo haya ni sawa na ongezeko la asilimia 77 kutoka kiasi cha Sh.Trilioni 13.59 zilizokusanywa katika kipindi hicho mwaka wa fedha wa 2020/2021,miaka minne tangu Rais Dk.Samia Suluhu Hassan aingie madarakani,"amesema Mwenda.


 Ameongeza kuwa ufanisi huu wa makusanyo uliofikiwa Julai-Machi 2024/2025 ni matokeo chanya ya kutekeleza kwa vitendo maagizo na maelekezo ya Rais Dk.Samia yanayohusiana na uongezaji wa uhiari wa ulipaji kodi kupitia uboreshaji wa huduma kwa walipakodi na uboreshaji wa shughuli za biashara nchini.

Mwenda amesema hatua zilizochukuliwa na kufanikisha ufanisi wa makusanyo hayo ni kutekeleza miongozo na maelekezo ya Rais Dk.Samia katika kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari na kuongezeka kwa utendaji kazi mzuri,nidhamu na ubunifu kazini kwa watumishi wa TRA.

Mengine ni kuendelea kutekeleza mikakati na kampeni za uhamasishaji wa uhiari wa ulipaji kodi nchini,serikali kuendelea kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini hali iliyosababisha kuongezeka kwa shehena ya mizigo inayoingizwa au kuondoshwa nchini katika vituo vya forodha nchini.

Mwenda amesema kuwa watumishi TRA wameendelea kuimarisha mahusiano na ushirikiano na Jumuiya za Wafanyabiashara pamoja na wafanyabiashara wote nchini pamoalja na kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa njia mbalimbali kwa wafanyabiashara.

Mengine ni kuanza matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Forodha (TANCIS) ulioboreshwa ambao ulizinduliwa Januari mwaka huu ili kuimarisha usimamizi wa vyanzo vyote vya mapato vya forodha,kufuatilia kwa ukaribu hali ya ufanyaji biashara nchini kwa kusimamia kikamilifu uzalishaji wa viwanda pamoja na kuhimiza matumizi ya mashine za kielektroniki (EFD).

Mwenda ameongeza kuwa katika kufanikisha ukusanyaji mapato katika miezi iliyobaki ya mwaka wa fedha 2014/2025 menejimenti ya TRA itaendelea kutekeleza maagizo ya Rais Dk.Samia kuhusu usimamizi wa kodi nchini na uhamasishaji wa ulipaji wa kodi kwa hiari.

Pia TRA itaendelea kukamilisha ujenzi wa moduli zote za Mfumo wa Usimamizi wa Kodi za Ndani (IDRAS) ifikapo Juni 2025, kuimarisha mahusiano na ushirikiano na walipakodi kupitia utoaji wa huduma bora pamoja na kampeni za elimu kwa mlipakodi.

Mengine yatakayofanyika ni kuimarisha usimamizi wa utoaji wa risiti za kielektroniki za EFD,kusimqmja na kuimarisha misingi ya mfumo mzuri wa kodi,kushirikiana kwa kikamilifu na timu iliyoteuliwa na Rais inayofanya mapitio ya mfumo wa utozaji kodi nchini na kuimarisha vitengo vya ukaguzi na uchunguzi wa kodi ili kuzuia ukwepaji kodi za ndani na forodha na hivyo kuondoa upotevu wa mapato ya serikali.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI