Na. Anangisye Mwateba-Pasiansi Mwanza
Jeshi la uhifadhi limetakiwa kuakisi maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kulinda, kuhifadhi maliasili za Tanzania kwa kufanya kazi katika mazingira rafiki na wananchi wanaoishi karibu na maeneo yaliyohifadhiwa.
Wito huu umetolewa na Naibu waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) alipokuwa akizindua bodi ya magavana ya Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi Jijini Mwanza Leo.
Mhe. Kitandula alisema kuwa moja ya majukumu ya bodi hiyo ni kuhakikisha askari wanaotoka katika Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi wanajengewa uzalendo na kuwa wanaenda kufanya kazi ya kulinda rasilimali za maliasili kwa niaba ya watanzania hivyo hakuna sababu ya kumuonea mwananchi wakati wakitimiza majukumu yao.
Aidha Mhe. Kitandula ameitaka Bodi ya Magavana ya Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi kuanzisha kozi za mafunzo ya muda mfupi katika nyanja za uhifadhi na malisili, Misitu na Utalii ili kukuza utalii wa ndani na kuongeza ufanisi katika maeneo ya kazi.
Mhe. Kitandula Aliongeza kuwa juhudi ziendelee za kutoa mafunzo ya kozi ndefu na fupi kwa kufuata Sheria na Miuongozo ya nchi, ili Taifa liendelee kupata watumishi wenye sifa kufanya kazi katika Maeneo yetu yaliyohifadhiwa, na Sekta ya Utalii.
“Vilevile juhudi hizo ziende sambamba na kuhakikisha mazingira ya kutolea mafunzo ni mazuri, chuo kinakuwa na vifaa vya kufundishia vya kisasa vyenye kuendana na tekinolojia ya kisasa. Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa miradi inayoendelea kutekelezwa hapa chuoni inakamilika kwa wakati na kwa viwango stahiki” Alisema Mhe. Kitandula
Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Agnes Sirima kwa niaba ya wajumbe wa bodi ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uteuzi wao ili watekeleze majukumu na kusimamia shughuli mbalimbali zinazoendeshwa na Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi.
Prof. Sirima aliongeza kuwa uteuzi wao ni deni kwa taifa kwani wapo Watanzania wengi wenye sifa ambao wangeweza kuteuliwa kufanya jukumu waliopewa wao. Hivyo wanaahidi kutimiza wajibu wao kwa juhudi, maarifa, weledi na tija ili shughuli mbalimbali za uhifadhi wa maliasili na utalii zionyeshe matunda kwa kuacha alama katika taasisi hiyo.
0 Comments