TAZAMA FULL MAHOJIANO HAPA BOFYA LINK HII
Na Zuhura Zukheri Matukio Daima Media, Iringa
Aliyekuwa Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Iringa Mjini, Pascal Chibala, ameeleza sababu za kuachana na chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa ni kutokana na ubabaishaji wa Tundu Lissu na kundi lake kupitia Kampeni ya No Reform No Election.
Huku Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Iringa, Frank Nyalusi, amesema chama hicho bado kina nguvu licha ya viongozi wake kuhamia CCM.
Wakizungumza katika kipindi cha Jukwaa la Siasa kinachorushwa na Matukio Daima kila siku ya Ijumaa na kinachoendeshwa na Francis Godwin, Chibala alisema hatua yake ya kujiunga na CCM imesababishwa na kazi nzuri zinazofanywa na serikali ya chama hicho.
“Nimekuwa katika siasa za upinzani kwa zaidi ya miaka ishirini, lakini miaka ya karibuni nimeona mwelekeo wa upinzani, hasa CHADEMA, ukipotea.
Hakuna mkakati thabiti unaoonesha wanataka kufanya nini katika miaka ijayo, hasa tunapoelekea uchaguzi mkuu,” alisema Chibala.
Chibala alieleza kuwa serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonyesha ufanisi kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo kukamilisha iliyokuwa imeanzishwa na mtangulizi wake, Hayati John Pombe Magufuli.
“Kazi zinazofanywa na Rais Samia zinaonekana. Nimekuwa nikifuatilia tangu aingie madarakani na nimevutiwa. Ndiyo maana nimeamua kwa hiari yangu kujiunga na CCM,” aliongeza Chibala.
Alisema ameondoka CHADEMA akiwa na dhamira njema, baada ya kujitolea kuhakikisha chama hicho kinabaki imara, ingawa kulikuwa na maneno ya kukatisha tamaa kutoka kwa baadhi ya makada na viongozi wa ndani.
Chibala alisema kuwa hali ya kuyumba kwa CHADEMA katika Jimbo la Iringa Mjini ilianza baada ya Mchungaji Peter Msigwa kuhamia CCM, lakini kama Katibu aliendelea kulijenga chama hadi alipoamua kujiunga na CCM.
Kwa mujibu wa Chibala, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ilipokuwa chini ya CHADEMA ilikuwa inakusanya mapato ya ndani ya Shilingi Bilioni 3.4, lakini baada ya CCM kuichukua, mapato yameongezeka hadi Bilioni 6.8 kwa mwaka. Aidha, alisema kuna vyanzo vipya vya mapato ambavyo vikisimamiwa vizuri vinaweza kufikisha makusanyo ya Bilioni 10 kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Alisisitiza kuwa amejiunga na CCM kwa hiari na si kwa kulazimishwa, akisisitiza kuwa kila mtu ana uhuru wa kuchagua chama cha kuunga mkono.
Pia alimnukuu Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Stephen Wasira, akiwashauri CHADEMA kukaa meza moja kujadili masuala ya mabadiliko (reforms) badala ya kufanya maandamano ambayo huathiri wananchi, hususan wanawake na watoto.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Iringa, Frank Nyalusi, alisema kuwa lengo la chama hicho ni kuhakikisha Watanzania wanaishi kwa amani na kufurahia maisha yao kupitia huduma bora.
Alilalamikia mfumo wa kodi unaowanyanyasa wafanyabiashara wadogo huku wakubwa wakibebwa kwa sababu ni makada wa CCM. Pia alisema CHADEMA hufuata katiba ya chama, na alipotakiwa kueleza sababu za baadhi ya viongozi kuhama, alishindwa kutoa majibu ya moja kwa moja.
Akizungumzia uchaguzi, Nyalusi alisema CHADEMA haitasusia uchaguzi, bali itasisitiza hoja ya mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.
“Niseme wazi, ulaghai na utapeli hatuutaki. Tunasimamia hoja ya reforms. Tukishinda hoja hiyo, tutaingia kwenye uchaguzi. Tukishindwa, hatutasusia uchaguzi bali tutajizuia usifanyike,” alisema.
Aidha, Nyalusi alisema si sahihi kuwalaumu CHADEMA kuhusu maendeleo kwa kuwa serikali iliyopo madarakani ndiyo yenye wajibu huo. Aliongeza kuwa miradi inayotekelezwa kwa fedha za mkopo inapaswa kuandikwa hivyo wazi, badala ya kusifiwa kwa majina ya viongozi.
“Huwezi kutofautisha serikali na Rais Dkt. Samia. Ndiyo maana tunashauri iandikwe wazi kuwa mradi umejengwa kwa mkopo wa serikali, si fedha binafsi za rais,” alisisitiza Nyalusi.
MWISHO
0 Comments