Mtoto wa pili amefariki kutokana na ugonjwa wa Surua ambao umeenea hasa magharibi mwa Texas nchini Marekani.
Kulingana na Naibu rais wa mfumo wa afya wa UMC, Aaron Davis ameiambia BBC kuwa Mtoto huyo hakuwa amepata chanjo ya kumkinga na ugonjwa huu na alikuwa akipokea matibabu hospitalini.
Waziri wa Afya nchini Marekani Robert F Kennedy Jr ambaye tayari amelaumiwa kwa jinsi anavyosimamia na kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo alizuru jimbo la Texas huku idadi ya vifo ikiongezeka.
Serikali ya jimbo hilo imeripoti visa 480 vya ugonjwa wa surua mwaka huu na mkurupuko huo unaonekana kuenea hadi majimbo jirani.
Mtoto wa kwanza wa umri wa miaka 6 ambaye hakuwa amechanjwa dhidi ya ugonjwa huo alifariki mwezi Februari huku mwanaume ambaye pia hakuwa amechanjwa akifariki katika eneo la New Mexico mwezi Machi mwaka huu.
Raia wa Marekani wamesisitiziwa kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa surua ili kujiepusha na maambukizi yanayosababisha madhara mwilini.
Virusi vya surua hujidhihirisha kwa dalili kama joto jingi mwilini, vipele vya rangi nyekundu, kikohozi na nyingine.
Ugonjwa huo unahusishwa pia na homa ya mapafu, ubongo kufura na kifo.
Mwaka 2000 Marekani ilitangaza kwamba imetokomeza kabisa ugonjwa wa surua lakini visa vimeripotiwa tangu wakati huo huku wengi walioambukiza hawajapata chanjo.
0 Comments