Na Mwandishi Wetu
Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency - PBPA) umesema mfumo wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja umeendelea kuimarisha upatikanaji wa mafuta nchini, kudhibiti mfumuko wa bei, kuhakikisha ubora wa mafuta na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa wa Logistic wa Petroli wa PBPA, Hilda Kowero, alisema taasisi hiyo inatumia maonesho hayo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake na mafanikio yaliyopatikana kupitia mfumo huo.
Alisema jukumu kuu la PBPA ni kuratibu uagizaji wa mafuta kwa pamoja ili kuhakikisha mafuta yanapatikana kwa uhakika katika maeneo yote ya nchi, hatua inayochangia maendeleo ya sekta mbalimbali za uchumi na huduma za kijamii.
Kowero alisema pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa mafuta, wakala huo hushirikiana na mamlaka mbalimbali za Serikali kuhakikisha mafuta yote yanayoingia nchini yanakidhi viwango vya ubora vilivyowekwa na mamlaka husika kabla ya kuanza kutumika.
Alieleza kuwa ushirikiano huo unahusisha taasisi kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) pamoja na Wakala wa Vipimo, jambo linalowapa wananchi uhakika wa kutumia mafuta yenye ubora na usalama unaokubalika.
Aidha, alisema mfumo huo umeongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa kuwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwa na uhakika wa kiwango cha mafuta kinachoingia nchini na hivyo kurahisisha ukusanyaji sahihi wa kodi kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Kwa mujibu wa Kowero, kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja kulikuwa na changamoto ya kuyumba kwa bei za mafuta, lakini kwa sasa mfumo huo umechangia kudhibiti mfumuko wa bei na kuhakikisha wananchi wanapata mafuta kwa bei zinazodhibitiwa kupitia taratibu zilizowekwa na EWURA.
Alisema mfumo huo pia umeendelea kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usambazaji wa mafuta katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ambapo mafuta yanayoagizwa kupitia bandari za Tanzania husafirishwa kwenda Rwanda, Burundi, Uganda, Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kowero alibainisha kuwa hali hiyo imeimarisha mahusiano ya kidiplomasia na biashara kati ya Tanzania na nchi jirani huku ikiongeza mchango wa sekta ya nishati katika kukuza uchumi wa taifa.
Aliwataka wananchi kutembelea banda la PBPA katika Maonesho ya Sabasaba ili kujifunza zaidi kuhusu majukumu ya wakala huo na namna mfumo wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja unavyoendelea kuchochea maendeleo ya uchumi wa Tanzania kupitia upatikanaji wa mafuta ya kutosha, salama na yenye ubora.











0 Comments