NA WILLIUM PAUL, ROMBO.
KATIKA kuhakikisha kuwa Watendaji wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi wilaya (UWT) wilaya za mkoa wa Kilimanjaro wanafanya kazi katika mazingira mazuri na rafiki kwao Mbunge wa viti maalum kupitia mkoa huo, Zuena Bushiri amekabidhi mabati 50 kwa ajili ya kupauwa nyumba ya mtumishi huyo wilaya ya Rombo.
Hii ni awamu ya nne Mbunge huyo anakabidhi mabati hayo ambapo alianza na nyumba ya Katibu wa UWT mkoa, nyumba ya Katibu wa UWT wilaya ya Mwanga na Same.
Mbunge Zuena alisema kuwa, lengo lake ni kuunga mkono juhudi za chama cha Mapinduzi na Jumuiya zake za kuhakikisha kuwa, kila mtumishi anafanya kazi katika mazingira mazuri na rafiki kwao.
"Nilianza kampeni hii ya kutoa mabati kwa ngazi ya UWT mkoa na sasa naendelea na ngazi za wilaya ambapo lengo ni kuhakikisha naunga mkono juhudi za wanachama wenzangu kukamilisha nyumba hizi za Watendaji wa Jumuiya yetu ngazi ya wilaya na mkoa" Alisema Mbunge Zuena.
Aidha Mbunge huyo aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha nyumba zote zinakamilika kwa wakati ili kuendelea kuongeza ufanisi kwa Makatibu wa UWT wilaya.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Rombo, Masoud Melimeli alisema kuwa, mchango huo wa Mbunge utaongeza chachu na morali ya kukamilisha ujenzi wa nyumba hiyo.
Mbunge huyo pia alifanya mkutano na wanachama wa UWT wilaya ya Rombo na kuwasisitiza kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi pamoja na kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha anapata kura nyingi na za kishindo.
Mwisho..
0 Comments