NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa viti maalum kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Zuena Bushiri amewataka Wakinamama, Vijana na Watu wenye ulemavu mkoani hapo kuendelea kuchangamkia fursa ya mikopo isiyo na riba inayotolewa na serikali ili kujiletea maendeleo na kujikwamua kiuchumi.
Mbunge Zuena alitoa kauli hiyo jana alipokutana na Wakinamama wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Moshi mjini katika ukumbi wa CCM mkoa.
Alisema kuwa, lengo la serikali kutoa fedha hizo ni kuhakikisha kuwa inawainua kiuchumi Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu na kuwataka kutochezea fursa hiyo.
"Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na mwanamama mwenzetu Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonyesha upendo wa dhati kwetu sisi Wakinamama hivyo hatupaswi kumuangusha Rais wetu tunapaswa kutumia fursa hii kutimiza lengo lililokusudiwa na serikali" Alisema Mbunge Zuena.
Mbunge huyo pia alitumia nafasi hiyo kuwaomba Wakinamama kumuunga mkono Rais Dkt. Samia kwani amefanya mambo makubwa na kwa kipindi chake cha miaka minne wananchi wa mkoani wa Kilimanjaro hakuna wanachomdai.
"Kwa sasa hakuna tunachomdai huyu mama isipokuwa yeye ndio anayetudai na tunajukumu la kumlipa kwa kumpa kura za kishindo katika boksi la kura katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu" Alisema Mbunge Zuena.
Aidha aliwataka Wakinamama kutoka na kusemea kazi zilizofanywa na Rais ili wananchi watambue kwanini Chama cha Mapinduzi kikampitia kugombea Urais na kumpa kura za kishindo.
Kwa upande wake, Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) mkoa wa Kilimanjaro, Irimina Mushongi alitumia nafasi hiyo kuwahamasisha Wanawake kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi pindi muda utakapofika.
Mwisho.
0 Comments