Header Ads Widget

HOTUBA YOTE YA RAIS DKT SAMIA AKIVUNJA BUNGE LA 12 JUNI 27/2025 BUNGENI DODOMA

HOTUBA YA MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA BUNGE LA 12 LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, 27 JUNE 2025


Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mb.), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

> Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

> Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;

> Mheshimiwa  Kassim  Majaliwa  Majaliwa (Mb.), Waziri 

Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

> Mhe. Frederick Tluway Sumaye, Waziri Mkuu Mstaafu;

Mhe. Mizengo Pinda, Waziri Mkuu Mstaafu;

> Mheshimiwa  Dkt.  Doto Mashaka  Biteko (Mb.), Naibu  Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati;

> Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb.), Naibu Spika wa 

 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

> Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;


> Waheshimiwa Wenyeviti na Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

> Mhe. Hamza Saidi Johari, Mwanasheria Mkuu wa Serikali;

> Ndugu Baraka Leonard, Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

> Viongozi mbalimbali mliopo;

> Wageni waalikwa; 

> Mabibi na Mabwana;


Habari za mchana!

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania...!


UTANGULIZI

  Mheshimiwa Spika, hakika tunayo kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kushuhudia siku hii adhimu katika historia ya Bunge letu Tukufu. Ibara ya 91(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inanitaka ninalihutubia Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuhitimisha shughuli za Bunge ili kuwezesha kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. 


SALAMU NA PONGEZI

Mheshimiwa Spika,  nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kulihutubia Bunge lako tukufu ili niweze kutimiza wajibu wangu huu wa msingi wa Kikatiba. Shukrani nyingi ni kwa uongozi wako shupavu, mahiri na wenye weledi mkubwa. Hakika umeliongoza vyema Bunge hili na  kukamilisha mikutano 19 katika Bunge hili la 12. Najua haikuwa kazi lakini pia ni kazi nyepesi kwako.  Kwani penye wengi kuna mengi na kila mtu na kichwa chake. Ila kwa uhodari mkubwa umeweza kuifikisha mashua yetu bandarini kama wafanyavyo Manahodha makini. Katika historia ya nchi yetu wewe ni mwanamke wa pili kushika wadhifa huu wa juu kabisa katika mhimili huu wa kutunga sheria. Hakika hujatuangusha wanawake wenzio. Uzoefu wako Kitaifa na Kimataifa umekuwa chachu  inayohakikisha kazi hii inafanyika kwa viwango vya hali ya juu, na hivyo kuendelea kulijengea heshima Bunge letu. Hongereni sana!


Mheshimiwa Spika, nikupongeze pia kwa kutekeleza majukumu haya sambamba na majukumu yako ya Rais wa 31 wa Umoja wa Mabunge Duniani. Kule nako umeweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Afrika kuchaguliwa kushika nafasi hiyo. Tunakupongeza sana kwa kuitumikia ipasavyo nafasi hiyo.


  Mheshimiwa Spika, vilevile niwashukuru Naibu Spika, Mheshimiwa Mussa Azan Zungu pamoja na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kutekeleza majukumu yao kwa uzalendo na weledi. Ahsanteni sana. 


Halikadhalika, nitoe shukrani na pongezi zangu za dhati kwenu nyinyi Waheshimiwa Wabunge kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya. Mmetimiza ipasavyo wajibu wenu wa kuwawakilisha wananchi, kutunga sheria na kuisimamia Serikali. Bunge hili limekuwa na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo na ustawi wa wananchi. Na bila shaka, ninyi wawakilishi wa wananchi mmeielewa vyema dhana ya "maendeleo ya watu". Kwamba, hatua na jitihada zote za Serikali hazina budi kuelekezwa kwenye kuboresha maisha ya kila Mtanzania. Hii imesaidia kujijengea nyinyi wenyewe Wabunge heshima kubwa lakini heshima ya Bunge letu. 


  Mheshimiwa Spika, sina budi kutambua mchango na mafanikio ya Waheshimiwa Wabunge waliotuwakilisha, kwenye majukwaa ya Mabunge ya Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, na Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu. Kipekee, nimpongeze Dkt. Deo Mwapinga kwa kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jukwaa la Mabunge ya Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu. Ni wazi kuwa mmeitendea haki demokrasia ya Tanzania na kuliletea heshima kubwa Bunge letu.


  Mheshimiwa Spika, vilevile, nitumie fursa hii kulishukuru tena Bunge hili kwa tuzo mliyonipatia kwa kutambua na kuthamini mchango wangu katika maendeleo na ustawi wa nchi yetu.  Ila kama nilivyosema siku nikiipokea tuzo hiyo,mafanikio yaliyopatikana yanatokana na mchango mkubwa wa Bunge, viongozi wenzangu Serikalini pamoja na Watanzania wote; kwa hivyo, tuzo ile ni yetu sote. Ninawashukuru sana kwa ushirikiano wenu. 


  Mheshimiwa Spika, Nitumie fursa hii kuwashukuru watangulizi wangu ambao leo hii nipo hapa kwa kuwa nilisimama juu ya mabega yao na kuweza kujifunza. Hakika misingi imara waliyoiweka imewezesha kupatikana kwa mafanikio haya mbalimbali katika kipindi changu cha miaka minne. Nikiri tu kwamba misingi yao na ushauri wao kwa wale niliobahatika kufanya kazi nao umenisaidia sana mimi binafsi pamoja na Serikali ninayoiongoza. Nimefurahi kumuona Mheshimiwa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete pamoja na Makamu wa Rais Wastaafu na pia Mawaziri Wakuu wastaafu tupo nao hapa.  Nichukue fursa hii kuwashukuru sana viongozi hawa kwa msaada wa kimawazo na ushauri ambapo wameendelea kunipa katika kipindi chote cha uongozi wangu. Hakika, nimeamini kuwa wazee ni dawa na palipo na wazee, hapaharibiki jambo. Nawashukuru sana!


  Mwisho wa shukrani ila sio kwa umuhimu niwashukuru waajiri wangu,  Watanzania, hakika wao ndio hamasa na chachu ya mie kufanya yote haya. Nawashukuru kwa sala, dua na maombi yao, bila kusahau ushirikiano mkubwa wa  hali na mali katika kuijenga Tanzania tunayoitaka na Taifa linalotumainiwa.


SALAMU ZA POLE

  Mheshimiwa Spika, tangu Bunge hili la 12 lianze, kuna viongozi, ndugu, jamaa na marafiki waliotutoka. Kama tunavyojua, tuliondokewa na Hayati Dkt John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano. Vilevile, tuliondokewa pia na Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Hayati Cleopa David Msuya aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, na Hayati Edward Ngoyai Lowassa, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu.

  Mheshimiwa Spika, hata katika Bunge hili, wapo pia Wabunge wenzetu tuliokuwa nao wakati wa ninahutubia Bunge tarehe 22 April, 2021, ila sasa wametangulia mbele ya haki. Tutaendelea kuwakumbuka Mhe. Martha Umbulla, Viti Maalum, Mhe. Atashasta Nditiye wa Jimbo la Muhambwe, Mhe. Khatib Haji wa Jimbo la Konde, Mhe. Elias Kwandikwa wa Jimbo la Ushetu, Mhe. William Ole Nasha wa Jimbo la Ngorongoro, Mhe. Irene Ndyamkama, Viti Maalum, Mhe. Mussa Mussa wa Jimbo la Amani, Mhe. Francis Mtega wa Jimbo la Mbarali, Mhe. Ahmad Abdulwakil wa Jimbo la Kwahani, na vilevile Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile wa Jimbo la Kigamboni. Hivyo, naomba tusimame kwa dakika moja kuwaombea. Mwenyezi Mungu azipumzishe roho zao mahali pema peponi. Amina!


UTEKELEZAJI WA AHADI KWA BUNGE

  Mheshimiwa Spika, utakumbuka kuwa, tarehe 22 Aprili, 2021, takriban mwezi mmoja baada ya kushika Wadhifa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nililihutubia Bunge hili. Nilielezea mtazamo wangu kuhusu nchi yetu na kutaja vipaumbele  vya Serikali ya Awamu ya Sita. Vilevile, vipaumbele vilivyoainishwa na Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2020/25. Niliahidi  kudumisha mema ya Awamu zilizopita, kuendeleza mema yaliyopo na kuleta mema mapya. Niliahidi pia kufanya mabadiliko pale itakapobidi kwa lengo la kuongeza ufanisi na tija. 


  Kama ilivyo ada, tunapohitimisha shughuli za Bunge, naomba kutumia fursa hii kutoa mrejesho wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali na yale ambayo tuliahidi kufanya.


  Ninapenda kusema maendeleo ni hatua, na tumesikia kutoka kwa Mawaziri mbalimbali pamoja na wabunge kazi iliyofanywa na Serikali. Lakini kwa kuwa mimi ndiye niliyetoa ahadi mbele ya Bunge hili, ninawajibika kutoa mrejesho hapa Bungeni. 


  Ninafurahi kusema kuwa kipindi hiki kimekuwa ni cha kufanya mageuzi makubwa, kuongeza tija kwenye shughuli za kiuchumi, na kujenga msingi imara wa ukuaji endelevu, wenye kasi zaidi na unaowainua watu kiuchumi. Vilevile, kimekuwa ni kipindi cha kuimarisha ustahimilivu wa jamii, kukuza ustawi wa wananchi na kuwawezesha kujiletea maendeleo.  


UMOJA , AMANI, USALAMA NA MSHIKAMANO WA KITAIFA


  Mheshimiwa Spika, nilipokabidhiwa dhamana ya kuiongoza nchi yetu, niliahidi kudumisha Tunu za Taifa letu, yaani amani, umoja na mshikamano, uhuru wa nchi yetu, Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar pamoja na kudumisha Muungano wetu. Kama ilivyokuwa kwa Serikali za Awamu zilizopita tumeshuhudia nchi yetu ikiendelea kujivunia tunu hizo na kuziimarisha.  Nyote ni mashahidi wa namna nchi yetu ya Tanzania imeendelea kuwa nchi moja na Watanzania wanaendelea kuwa wamoja, wenye mashirikiano licha ya kuwa na tofauti zao za kidini, mila na desturi , Itikadi za kisiasa na hata ushabiki wa michezo (Simba na Yanga). 


  Mtakumbuka kuwa katika Hotuba yangu kwa Bunge nilisisitiza umuhimu wa viongozi wa pande zote mbili za Muungano kukutana na kuzungumzia ustawi wa Muungano wetu. Nafurahi kuwataarifu kwamba maagizo yangu yale yametekelezwa kwa ufanisi zaidi chini ya Uenyekiti wa Makamu wa Rais akisaidiwa na Waziri Mkuu kwa upande wa Tanzania Bara na kwa Upande wa Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais.


   Katika kipindi hiki, tumepiga hatua kubwa, hususan kwa kuzipatia ufumbuzi jumla ya hoja 15 za Muungano; hatua inayozidi kuongeza imani ya Watanzania kwa Serikali. Pamoja na hayo, niwaase Watanzania wenzangu, tuendelee kushikamana, na kuwa makini na vitisho vyovyote dhidi ya Muungano wetu, na niwasihi kuendeleza umoja, utulivu na amani; vitu ambavyo  ni sifa njema kwa nchi yetu. 


Amani na Usalama


  Mheshimiwa Spika,  Nchi yetu iko salama, mipaka yetu ipo salama na imara  kwa sababu Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limeendelea kutimiza ipasavyo jukumu lake la kulinda uhuru na mipaka ya nchi yetu.


  Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, lilitimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake. Katika kipindi hiki tumewekeza sana katika kuliimarisha kwa vifaa,  zana za kisasa na mafunzo. Weledi na nidhamu ya Wanajeshi wetu ni ya hali ya kupigiwa mfano. Tumeboresha maslahi na makazi ya wanajeshi kwa kujenga nyumba mpya 6,064 za kuishi askari. 


   Uwezeshaji huo umechangia kulifanya Jeshi letu kushiriki ipasavyo katika shughuli mbalimbali za kitaifa na kimataifa, ikiwemo ulinzi wa rasilimali, ulinzi wa miradi mikubwa ya kimkakati, na oparesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa, hasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Lebanon, Sudan Kusini na eneo la Abyei. 


  Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), tumepanua miundombinu na kuongeza idadi ya vijana wanaojiunga na jeshi kutoka 160,427 mwaka 2020 hadi 190,059 mwaka 2025. Tumefanya hivyo kwa kutambua kuwa Jeshi la Kujenga Taifa ni nyenzo muhimu ya kujenga ujasiri, uzalendo na dhana ya kujitegemea miongoni mwa vijana. Vilevile, SUMAJKT imeweza kushiriki kikamilifu kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uzalishaji na miradi ya ujenzi.


  Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Jeshi la Polisi, tumeendelea kuliimarisha kwa kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza miundombinu, ambapo vituo vya polisi 472 vimejengwa hadi ngazi ya kata na shehia. Halikadhalika, tumeboresha makazi ya askari na kununua vitendea kazi, ikiwemo magari na pikipiki, kwa ajili ya kazi za utawala na operesheni. Aidha, askari wapya 16,009 wameajiriwa, huku Maofisa, Wakaguzi na Askari 10,363 wakipandishwa vyeo. Natoa pongezi nyingi kwa Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya. Hatuna budi kutambua kwamba uhalifu unaozuiliwa kwa jitihada za Jeshi la Polisi ni mkubwa kuliko unaofanyika. Kasi ya kuwabaini na kuwakamata wahalifu, na kuwafikisha Mahakamani imeongezeka.  Jambo ambalo bado hatujafanikiwa vya kutosha ni ajali za barabarani.  Lazima nazo tuendelee kuzitafutia muarobaini wake. Aidha, nalielekeza Jeshi la Polisi kuongeza jitihada katika kukomesha matukio ya watu kupotea.


  Mheshimiwa Spika, Jeshi letu la Magereza nalo limeendelea kutekeleza vizuri majukumu yake ya kulinda wafungwa na kurekebisha tabia zao. Aidha, katika kulinda haki za binadamu, tumeendelea kuboresha huduma za malazi, mavazi na chakula  kwa wafungwa jinsi hali ya uchumi inavyoimarika.  Kwa upande wa Watumishi, Serikali  imepandisha vyeo  maafisa waandamizi na askari wa Jeshi hilo wapatao 14,733 na kuajiri askari wapya 3,404; hivyo kupunguza uhaba wa rasilimali watu. Vilevile, tumewapa vitendea kazi, ikiwemo magari, kwa ajili ya  kuimarisha utendaji kazi. Magereza mapya 8 pamoja na Hospitali Kuu ya Kanda ya Jeshi la Magereza Dodoma, yanaendelea kujengwa. Serikali imewezesha jumla ya magereza 66 kuanza kutumia mfumo wa TEHAMA wa Mahakama Mtandao ambao unarahisisha usikilizaji wa kesi bila wafungwa kusafirishwa hadi mahakamani.


  Mheshimiwa Spika, ili kuongeza uwezo wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kufikia maeneo ya dharura kwa wakati, Serikali imewezesha ujenzi wa vituo vipya vya zimamoto vitatu vilivyokamilika na vinane vinaendelea na ujenzi. Vilevile, vituo vya zamani vimefanyiwa ukarabati, na kununua magari 12 ya kuzima moto yakiwemo magari mawili yenye ngazi kwa ajili ya kufikia majengo marefu, na boti mbili za uokoaji katika Bahari na Ziwa Victoria.


  Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Idara ya Uhamiaji, zaidi ya maafisa, wakaguzi na askari 3,115 wamepandishwa vyeo, na askari wapya 2,251 wameajiriwa. Aidha, doria, misako na operesheni ziliimarishwa katika maeneo mbalimbali nchini, na zimewezesha kukamatwa watu 97,538 kwa makosa ya uhamiaji, ambao wamechukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo, kwa baadhi yao, kuondoshwa nchini. Vilevile, tunaendelea na ujenzi wa Chuo cha Mafunzo cha Uhamiaji cha Raphael Kubaga kilichopo Boma Kichakamiba Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga.


  Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kupunguza uingizaji, uzalishaji na usambazaji wa dawa za kulevya kwa kubaini na kudhoofisha mitandao ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya. Katika kipindi hiki, tulikamata jumla ya Kilogramu 4,697,511.35 za dawa za kulevya zikihusisha watuhumiwa 25,715. Kwa upande mwingine, katika kuwasaidia waathirika, tumeongeza vituo vya utoaji huduma za tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya kutoka vituo 9 mwaka 2020 hadi 18 mwaka 2025, ili kupanua wigo wa huduma hii muhimu. Pamoja na hatua hizo, hatua nyingine madhubuti za kudhibiti na kuwalinda vijana wetu dhidi ya dawa hizo zinaendelea kuchukuliwa.


Uratibu wa Maafa

  Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha mfumo wa usimamizi wa maafa, tulirekebisha Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya Mwaka 2004, Toleo la Mwaka 2025 na tulitunga Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya Mwaka 2022 kwa lengo la kuweka mfumo wa kitaasisi wa usimamizi wa maafa kuanzia ngazi ya Taifa hadi Wilaya.


  Nyote ni mashahidi wa maafa makubwa yaliyotufika kwa nyakati tofauti, kutokana na mvua kwenye maeneo ya Hanang, Mbeya, Rufiji na Moshi. Kipekee, nivipongeze vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuwa mstari wa mbele na kushiriki  katika uokoaji wakati wa maafa, na vilevile usambazaji wa mahitaji muhimu kwa waathirika. 


  Mheshimiwa Spika, kufuatia maafa ya Hanang, Serikali iliratibu ujenzi wa nyumba 109 za kudumu zenye thamani ya Shilingi bilioni 3.08 kwa ajili ya waathirika 745 ambao nyumba zao ziliharibiwa.


  Pia, nitambue mchango wa taasisi za kiraia, Wafanyabiashara na wananchi waliojitolea na kushiriki kikamilifu katika mazoezi ya uokoaji kama tulivyoona kwenye ajali ya ndege ya Bukoba, maporomoko ya Hanang, na kuanguka kwa jengo Kariakoo. Huu ndio Utanzania, na ninawapongeza tena kwa moyo wao wa utu na uzalendo.

 

MASUALA YA SIASA NA UTAWALA BORA


Hali ya Siasa na Demokrasia Nchini

  Mheshimiwa Spika, nilipoingia madarakani niliona haja ya kuhakikisha tunaendelea kujenga Taifa lenye maelewano na maridhiano ili tuweze kwenda pamoja katika mwelekeo wa maendeleo. Dhima hii ilinisukuma kubuni na kutekeleza falsafa ya R Nne. Tukiongozwa na falsafa hiyo ilituelekeza kwenye mageuzi, maridhiano,ustahimilivu na kujenga upya, na tuliweza kuwaleta wadau wa kisiasa na wengineo pamoja, na kufanya maamuzi na maboresho mbalimbali yaliyojumuisha na kushirikisha wadau wote. Serikali iliunda Tume ya Maridhiano iliyofanya kazi nzuri na  ilikuja na mapendekezo ya aina mbili, yale ambayo ni ya muda mrefu kama mabadiliko ya Katiba, na yale ya muda mfupi ambayo yalihusu masuala ya uhuru wa vyombo vya habari na masuala ya vyama vya siasa kufanya shughuli zao.


Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mapendekezo ya Tume, Serikali iliondoa mara moja zuio la mikutano ya hadhara kwa Vyama vya Siasa, na wote tumeshuhudia vyama vikiendelea kufanya shughuli zao kwa uhuru, ikiwemo mikutano ya hadhara kote nchini. Vilevile, Baraza la Vyama vya Siasa limefanya mikutano sita (6) na kutoa mawazo na ushauri uliowasilishwa Serikalini na kufanyiwa kazi. Kufuatia mashauriano yaliyowahusisha wadau wote wa kisiasa, Bunge  lilitunga Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 1 ya Mwaka 2024, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 2 ya Mwaka 2024, Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258, na Sheria ya Gharama za Uchaguzi. Kwa mara ya kwanza, katika historia ya nchi yetu, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi iliundwa kwa sheria yake yenyewe. Tulifanya  ili kujibu rai ya muda mrefu ya wadau wa kisiasa nchini. Miongoni mwa maboresho kwenye Sheria ya Uchaguzi yalikuwa ni kuongeza takwa la kila mgombea kupigiwa kura hata akiwa mgombea pekee, hatua ambayo inafuta kilichojulikana kama mgombea kupita bila kupingwa. Vilevile, utungaji wa Kanuni za uendeshaji wa uchaguzi ulifanyika, na Serikali imeendelea kuimarisha uendeshaji wa shughuli za vyama vya siasa nchini, ambapo hadi Juni, 2025, Serikali imetoa ruzuku ya Shilingi bilioni 87.81 kwa vyama vinavyostahili kupata ruzuku. 

  Mheshimiwa Spika, Katika hatua nyengine, asasi za kiraia nazo zimekuwa huru kufanya shughuli zao, ikiwa ni pamoja na kukutana na kuishawishi Serikali ambapo mapendekezo yao mengi  yamepokelewa na kufanyiwa kazi. Kwa kuwa suala la Katiba ni pendekezo la muda mrefu la Tume ya Maridhiano, wa msingi huo, mchakato wa Katiba mpya ni  miongoni mwa ahadi ambazo zinaonekana katika Ilani ya CCM ya 2025-2030. Hivyo, ni kusema kuwa mchakato wa Katiba Mpya itatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo. 


Mapambano Dhidi ya Rushwa

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua kuwa rushwa ni adui wa haki na kikwazo kwa maendeleo, Serikali imeongeza nguvu kwenye mapambano dhidi ya rushwa. Jitihada hizo zimeiwezesha Tanzania kushika nafasi ya pili katika Ukanda wa Afrika Mashariki na nafasi ya 14 kwa nchi za Afrika kwenye mapambano dhidi ya rushwa, na hii kwa mujibu wa taarifa ya Taasisi ya Transparency International ya mwaka 2024. Katika kipindi hiki, tulidhibiti na kuokoa kiasi cha Shilingi bilioni 211.95 na kuzirejesha Serikalini kupitia operesheni mbalimbali za uchunguzi wa tuhuma za rushwa. Aidha, mali zenye thamani ya Shilingi bilioni 35.688 zikijumuisha nyumba, viwanja, magari na fedha taslimu Shilingi bilioni 1.17 zilitaifishwa. Na katika jitihada hizi, nitoe rai kwa Watanzania kuendelea kutoa ushirikiano katika mapambano dhidi ya rushwa. 


Bunge

Mheshimiwa Spika,

Serikali imeendelea kutimiza ipasavyo wajibu wake kwa mhimili wa dola wa Kutunga Sheria. Katika kipindi cha uhai wa Bunge la 12, kulipitishwa  miswada 60, maazimio 922, na vilevile Serikali imetoa taarifa 15 kupitia kauli za Mawaziri bungeni kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala yenye maslahi mapana kwa taifa. Hakika mmefanya kazi kubwa kwani michango na ushauri wa Bunge hili umekuwa chachu kwa baadhi ya hatua tulizochukua kwenye mabadiliko ya kisera, kisheria na kiutendaji yaliyofanywa na Serikali.


Serikali iliongeza kiwango cha Mfuko wa Jimbo kutoka shillingi  bilioni 11 mwaka 2021/2022 hadi shillingi bilioni 15.9 kuanzia mwaka 2022/2023 hadi sasa ili kurahisisha utendaji wenu majimboni na kuchochea maendeleo. Ni matumaini yangu kwamba fedha hizi mlizitumia vyema katika kuwaletea wananchi maendeleo. 


Uchaguzi Mkuu

Mheshimiwa Spika,

  Uchaguzi Mkuu ndio mazungumzo makubwa nchini kwa sasa. Niseme kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi itatangaza hivi karibu tarehe ya siku ya Uchaguzi. Zoezi la uandikishwaji limeshaisha nchi nzima.  Zoezi la Kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura limekamilika kwa awamu mbili kama ambavyo  Sheria inaelekeza. Sote tumeshuhudia mwitikio mzuri wa wananchi kujitokeza kwenye vituo vya  kuandikisha wapiga kura, na ninawapongeza wananchi wote kwa kujitokeza kwao. Tunatarajia Tume kwamba itatutangazia idadi ya wapiga kura. 


Uhuru wa Habari

Mtakubaliana nami kuwa uhuru wa habari na uhuru wa watu kutoa maoni yao umeongezeka. Majukwaa ya kutolea habari nayo yameongezeka tofauti na hapo awali sasa hivi kutokana na kukua kwa matumizi ya mtandao na kuongezeka kwa majukwaa ya kidijitali habari nyingi zinapatikana kiganjani. Serikali imetoa leseni kwa magazeti na majarida 356, vituo vya redio 247, vituo vya televisheni 68, redio na televisheni za mitandaoni 325 na blogs 72.


Tuna magazeti ya kila siku na kamwe Serikali haijafanya uhakiki wa habari kabla hazijachapishwa au kuandikwa. Tunafanya hivi tukiamini waandaaji wa maudhui haya ni watu wenye weledi wa kutosha, na kwamba tunafahamu ustawi wa demokrasia yetu hutegemea sana uhuru wa vyombo vyetu vya habari. Tunathamini na kutambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika kuelimisha jamii, kupambana na maovu pamoja na kuhimiza uwajibikaji.


Katika kulinda na kutambua michango wa waandishi wa habari kwa jamii tulifanya marekebisho ya Sheria ya Huduma za habari ya Mwaka 2016 na Kanuni zake. Pia tuliandaa Tuzo za Samia Kalamu Awards kutambua waandishi wa habari za maendeleo Tanzania. Pamoja na hatua zote hizi hatukusita wala kuchelea kuchukua hatua pale uhuru huu ulipotumiwa vibaya na kutishia kuleta vurugu nchini pamoja na kuvuruga usalama wa jamii au pale uhuru huu ulikiuka Sheria za nchi au maadili, mila na desturi za Kitanzania. Hivyo basi tutaendelea kusimamia uhuru wa vyombo vya habari wakati wote.


MASUALA YA KIUCHUMI


Hali ya Uchumi  (Mapato na Matumizi ya Fedha na Mali za Serikali)

  Mheshimiwa Spika,  Serikali imeendelea kuelekeza nguvu kwenye sera za uchumi jumla na sera za uchumi katika ngazi ya chini zinazogusa wananchi wa kawaida.  Ni wazi kuwa kazi hii haikuwa nyepesi wala rahisi kutokana na hali ya UVIKO 19 na Migogoro ya kikanda inayoendelea ambayo imepelekea uchumi wa duniani kutetereka. Ili kukabiliana na hali hii Serikali ilichukua hatua mbalimbali za kisera, kiutawala na uwekezaji ili kukuza uchumi wa nchi yetu. Ni wazi kuwa jitihada  zetu zilizaa matunda.  ukuaji wa uchumi wa nchi ulipanda kutoka wastani wa asilimia 3.9 mwaka 2021, hadi asilimia 5.5 mwaka 2024. Ukuaji huu uko juu ya wastani wa ukuaji wa bara la Afrika ambao ni asilimia 4 kwa mwaka 2024. Aidha, wakati uchumi wa dunia unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 2.3 mwaka 2025, Shirika la Fedha Duniani linakadiria kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania mwaka huu itafikia asilimia 6.  Pato ghafi la Taifa limeongezeka kutoka shillingi trilioni 156.4 mwaka 2021 hadi kufikia  shillingi  trilioni 205.84 mwaka 2024 Hivyo basi, pato la wastani la Mtanzania nalo limeongezeka kutoka shillingi 2, 397,411 mwaka 2020 hadi shillingi  2,938,634 mwaka 2024. Pia shillingi yetu imeendelea kuimarika.


  Mheshimiwa Spika, kiashiria kingine muhimu cha utulivu wa kiuchumi ni mfumuko wa bei, ambao uliendelea kuwa chini ya asilimia 5 kwa miaka yote minne. Kiwango hiki sio tu kipo ndani ya lengo letu kama nchi la kuhakikisha hakizidi asilimia 5, pia ni miongoni mwa viwango bora Afrika Mashariki, na kiko chini ya wastani wa mfumuko wa bei ulioshuhudiwa barani Afrika. Hali hii inatokana na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na kibajeti, na uhakika wa upatikanaji wa chakula katika masoko ya ndani kutokana na kukuza tija katika uzalishaji wa chakula. 


  Mheshimiwa Spika, Mauzo yetu  ya bidhaa nje ya nchi yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 6.39 mwaka 2021 hadi kufikia dola za Marekani bilioni 8.7 mwaka 2024 na kutunisha akiba yetu ya fedha za kigeni ambapo hadi Mwezi Aprili 2025 tulikuwa na akiba ya Dola za Marekani bilioni 5.6 inayotosheleza kuagiza bidhaa na huduma kwa miezi nne na nusu, kama lilivyo lengo la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, kufuatia marekebisho ya Sheria ya Madini, Sura ya 123, Benki Kuu ya Tanzania iliweza kununua na kuwa na akiba ya kilo za dhahabu 3,424 zilizonunuliwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 702.3, na ununuzi unaendelea ili kuimarisha zaidi kiwango cha akiba tulichonacho.


  Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la makusanyo ya kodi, nililielezea Bunge kwamba ningependa kuona wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi wanaelimishwa na kutambua kwamba kodi ndio msingi wa  maendeleo ya nchi, na hivyo, wawezeshwe  kulipa kodi bila kutumia mabavu. Katika kufikia azma hii, Serikali imeimarisha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji mapato, udhibiti wa mianya ya kupoteza mapato, kuanzisha Jukwaa la Kodi na Uwekezaji, na kuijengea uwezo Mamlaka ya Mapato Tanzania na mamlaka nyingine za ukusanyaji mapato ya Serikali. Jitihada hizo zimeongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa mwezi kutoka Shilingi trilioni 1.51 mwezi Novemba, 2020 hadi Shilingi trilioni 3.09 mwezi Machi, 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 104. Ili kuimarisha zaidi usimamizi wa kodi nchini, niliunda Tume ya Rais ya Marekebisho ya Kodi ambayo tunatarajia itakuja na mapendekezo yatakayoleta mageuzi ya kiutendaji kwenye mifumo ya utozaji na ukusanyaji wa kodi nchini.


  Mheshimiwa Spika, ili kutoa huduma bora kwa wananchi, Bajeti ya Serikali imeongezwa kutoka Shilingi trilioni 34.88 mwaka 2020/21 hadi Shilingi trilioni 50.29 mwaka 2024/25, ikiwa ni ongezeko la wastani wa asilimia 8.84 kwa mwaka. Nalishukuru Bunge hili kwa kupitisha Bajeti hizo, kwa kweli, zimekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa kuboresha huduma za kijamii na kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati. 


DENI LA SERIKALI


  Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia Mei 2025, deni la Serikali lilifikia shilingi trilioni 107.70. Kati ya deni hilo, deni la nje ni shilingi trilioni 72.94 na deni la ndani ni Shilingi trilioni 34.76. Kuongezeka kwa deni la Serikali kumetokana na sababu mbalimbali. Mojawapo ni kupokelewa kwa fedha za mikopo mipya na ya zamani ambayo mikataba yake iliingiwa tangu Serikali za Awamu za nyuma kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Ni vyema tukafahamu kuwa mkopo unaweza ukasainiwa leo lakini fedha husika zikaanza kupokelewa baada ya maandalizi ya mradi kukamilika na mradi kuanza. Hivyo, ili mkopo uwe deni ni lazima Serikali iwe imepokea fedha, huduma au vifaa. Hivyo, ni vyema wananchi wakaelewa kuwa katika awamu ya Sita pamoja na kusaini mikopo mipya lakini pia tunaendelea kupokea fedha za mikopo ambayo ilisainiwa katika vipindi tofauti na kuongeza kiasi cha deni la Serikali.  Kwa mfano awamu ya sita imepokea kiasi cha shilingi trilioni 11.3 ikiwa ni mikopo iliyosainiwa na awamu zilizopita. Sababu nyingine ya ongezeko la deni la nje ni kuimarika kwa dola ya Marekani dhidi ya shilingi ya Tanzania. Kwa mfano mwezi Machi 2021 kiwango cha kubadilisha shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani kilikuwa shilingi 2,298.5 wakati Machi, 2025 kilikuwa 2,650. Hivyo, endapo deni la serikali litatajwa kwa shilingi ya Tanzania ni lazima lionekane limeongezeka mathalani kwa sasa deni limeongezeka kwa zaidi ya shilingi trilioni 9.3. Hatua hii ya kushuka kwa thamani kwa shilingi dhidi ya dola ya Marekani isichukuliwe kama ni hatua hasi bali ilikuwa ni hatua muhimu ya kukabiliana na mtikisiko wa uchumi wa Dunia.


  Mheshimiwa Spika, kuhusu mwenendo wa ulipaji wa deni la serikali, ninapenda kutaarifu kuwa malipo ya deni la Serikali yamekua yakiongezeka kutoka Shilingi trilioni 8.22 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi kufikia makadirio ya Shilingi trilioni 14.20 kwa mwaka 2025/26. Ongezeko hili ni kutokana na kuiva kwa mikopo ya muda mrefu, na mikopo yenye masharti ya kibiashara iliyokopwa katika awamu zilizopita kwa ajili ya miradi ya maendeleo.  Aidha, kuongezeka kwa malipo ya deni hasa la nje, kumesababishwa pia na mabadiliko ya mara kwa mara ya riba katika masoko ya fedha ya kimataifa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo athari za UVIKO-19 na uamuzi wa hazina ya Marekani (US Treasury) kubadilisha viwango vya riba vya dhamana za Serikali ya nchi hiyo. Mabadiliko hayo yalisababisha baadhi ya nchi zinazoendelea hasa Afrika kushindwa kulipa madeni kwa wakati. 


  Mheshimiwa Spika, ongezeko la Deni la Serikali la Ndani limechangiwa na mikopo ya kugharamia miradi ya maendeleo na kulipa madeni ya ndani yaliyoiva kwa wawekezaji wa Dhamana za Serikali kwa utaratibu wa kulipia mtaji wa dhamana za Serikali zilizoiva. Aidha, tulifanya maamuzi ya kutambua madeni mengine ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa Serikali kupitia hatifungani maalumu isiyo taslimu yenye thamani ya shilingi trilioni 2.67 kati ya kiasi hicho shilingi trilioni 2.18 madeni ya PSSSF ya waliokuwa wafanyakazi wa Serikali kabla ya 1999 (maarufu kama pre-99). Shilingi bilioni 433.71 ni madeni ya NSSF ya muda mrefu na shilingi bilioni 63.52 ni madeni ya kampuni ya Ubia ya mifuko ya Pension yaani PPP (Pension Property Limited) Kampuni hii ilifadhili miradi ya Serikali kwa kutoa mikopo kwa vipindi tofauti kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya Serikali ambayo ni ujenzi wa ukumbi wa Bunge-Dodoma na ujenzi wa Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela, Arusha. Madeni haya hayakuwahi kuwa sehemu ya deni la Serikali. Kiasi cha shilingi trilioni 2.2 kilichobaki kinatarajiwa kuanza kutambuliwa ndani ya miaka mitatu ijayo kwa kuanzia na mwaka wa 2025/2026 ambapo deni la kabla ya mwaka 1999 kiasi cha bilioni 630 litatambuliwa na deni la NHIF kiasi cha bilioni 180 zilizotumika kujenga Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma. Lengo la hatua hizi ni kunusuru mifuko ya Hifadhi ya Jamii yenyewe lakini pia kuhakikisha wastaafu wetu waliolitumikia Taifa wanapata mafao yao kwa wakati.Tumetambua madeni haya ili kutoa nafuu kwa mifuko yetu.


  Mheshimiwa Spika, nimeona niyaseme haya kwa urefu ili Watanzania waelewe kuhusu suala hili la deni la Taifa ambalo hupotoshwa mara kwa mara. Aidha, niwahakikishie Watanzania kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha deni linaendelea kuwa himilivu. Tutaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi wa mikopo katika ugharamiaji wa bajeti zetu. Tutaendelea kuelekeza fedha za mikopo katika miradi inayokuza mapato ya ndani na mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi. Tutaendelea kuhakikisha Maafisa Masuuli wanazingatia maandalizi ya msingi ya mradi kabla ya kuingia mikataba kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo ikiwemo Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada Sura 134.  Vilevile, tutaendelea kuimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa miradi inayotekelezwa kwa mikopo ili kuhakikisha inaleta tija iliyokusudiwa.


  Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa nidhamu ya matumizi  ya fedha na mali za Serikali tumeendelea kuelekeza nguvu zetu katika kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuimarisha utaratibu wa manunuzi Serikalini na ukaguzi wa hesabu za Serikali. Kwa upande wa ununuzi wa bidhaa  na huduma, tumehakikisha Sheria ya  Mamlaka ya Ununuzi wa Umma inafanya kazi ipasavyo ili kuhakikisha kuwa kuna usimamizi thabiti wa sheria hiyo na kanuni zake. 


Mipango

  Mheshimiwa Spika, Sote tunafahamu kwamba mipango si matumizi. Hivyo basi, katika kuimarisha matumizi sahihi ya fedha tunazozikusanya au kukopa  tuliunda tena  Tume ya Mipango ili kuhakikisha mipango ya kisekta inafungamanishwa na malengo ya kitaifa pamoja na rasilimali tulizonazo.  


Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050

  Mheshimiwa Spika, tumesimamia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 kwa mafanikio makubwa. Uchumi umekua na nchi kuweza kuingia katika kipato cha kati,  na kuimarisha maisha ya Watanzania. Serikali imekamilisha maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050. Dira hiyo mpya tutakayoizindua rasmi mwezi Julai 2025 itatupa mwelekeo utakaowezesha Taifa letu kupiga hatua zaidi za maendeleo. Niwashukuru wote waliohusika kuitayarisha, hususan wananchi walioeleza bayana mahitaji na matarajio ya Tanzania wanayotaka kuiona katika miaka 25 ijayo.


Mheshimiwa Spika,

  Vilevile, ninafurahi kwamba tumefanya mazoezi yaliyoimarisha mfumo wetu wa takwimu muhimu katika kufanya mipango yetu. Mwaka 2022, tulifanya Sensa ya Watu na Makazi, tukiendeleza utamaduni wetu wa kufanya Sensa kila baada ya miaka 10. Vilevile, tulifanya Utafiti wa mwenendo wa idadi ya watu na Masuala ya Afya. Zaidi ya hapo, na kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, tuliweza kufanya Sensa ya Majengo kote nchini. Mazoezi yote hayo yametuwezesha kupata taarifa muhimu zitakazotusaidia kupanga mipango yetu ya maendeleo kisayansi zaidi.


 Utawala wa Sheria na Madaraka ya Wananchi 

Maboresho ya Mfumo wa Utoaji Haki

  Mheshimiwa Spika,  Amani tuliyonayo kwa kiasi kikubwa inalindwa na uimara na ufanisi wa Mahakama zetu na vyombo vingine vya kusimamia haki.  Hii ni kwa sababu amani na utulivu hustawi pale ambapo haki huonekana kutendeka. Katika kuimarisha utawala wa sheria, kuongeza uwajibikaji, ufanisi na kupunguza malalamiko ya wananchi na ucheleweshaji wa mashauri,  niliunda Tume ya Rais ya Kuangalia namna ya Kuboresha Mifumo ya Haki Jinai. Mapendekezo ya Tume hiyo yanaendelea kutekelezwa na taasisi mbalimbali. Kwa kipindi chote Mahakama imeendelea kuwa huru na kamwe Serikali haikuiingilia Mahakama katika kazi zake. Ili kuboresha utendaji na ufanisi wa mahakama tumeongeza bajeti ya mahakama kutoka shilingi bilioni 166.2 mwaka 2020/2021 mpaka kufikia shilingi bilioni 321 mwaka 2025/2026, sawa na ongezeko la asilimia 93. Vilevile tumeongeza idadi ya Majaji, Mahakimu na Mawakili wa Serikali, na nafarajika kwamba tumezingatia uwakilishi wa kijinsia. Katika kipindi hiki pia nimeteua Majaji wapya 83 ambapo Majaji wa Mahakama ya Rufani ni 15 kati yao wanne (4) ni wanawake na Majaji wa Mahakama Kuu 68, kati yao 30 ni wanawake. Aidha, tuliwezesha ajira mpya ya Mahakimu na watumishi wengine jumla 1,153. Majaji na Mahakimu wanawake wamekuwa wengi wakati huu kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi yetu. 


  Hatua hizi zimewezesha Mahakama kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa pamoja na kuhakikisha  mifumo ya TEHAMA katika utoaji huduma za kisheria inasomana na mifumo ya NIDA, TAKUKURU, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Jeshi la Polisi Tanzania na Taasisi nyingine za Sheria. Aidha, Serikali imeendelea kutekeleza Mpango wa Kutenganisha Shughuli za Mashtaka na Upelelezi kwa kuendelea kuongeza idadi ya Mawakili wa Serikali na kuongeza  Ofisi za Mashtaka za Wilaya kutoka 50 hadi 108 ili kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi.

  Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha mifumo ya utoaji haki, mafanikio mbalimbali yamepatikana yakiwemo kukamilika kwa ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama sambamba na nyumba za kuishi Majaji zilizopo eneo la Iyumbu Dodoma; ujenzi wa majengo ya Mahakama za Wilaya tatu (3) na Mahakama za Mwanzo 26 katika maeneo mbalimbali nchini; ujenzi wa vituo sita (6) Jumuishi vya Utoaji Haki katika maeneo ya Dodoma, Morogoro, Mwanza, Arusha, Kinondoni na Temeke. Vilevile, tumefanya ujenzi wa Vituo tisa (9) Jumuishi vya Utoaji Haki katika  mikoa ya Katavi, Songea, Songwe, Njombe, Simiyu, Lindi, Singida, Pemba na Geita ambapo ujenzi unaendelea. Miradi hii imewezesha kusogeza huduma za Mahakama karibu na Wananchi.


  Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha upatikanaji haki kwa watu wote Serikali imetekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign - MSLAC). Jumla ya wananchi 2,698,908 kwenye Mikoa mbalimbali wamepatiwa huduma mbalimbali za kisheria. 


Mheshimiwa Spika, kwa mara ya pili katika historia ya nchi yetu, Serikali imekamilisha urekebu wa Sheria Kuu 446 za nchi na kuandaa Toleo la Sheria Zilizofanyiwa Urekebu la Mwaka 2023. Hatua hii inawarahisishia watumiaji wa sheria zetu kufanya rejea ya sheria mbalimbali hususan wakati wa utoaji wa haki. Toleo hili ambalo litaanza kutumika tarehe mosi Julai, 2025 litaimarisha utawala wa sheria. Aidha, hadi sasa Sheria Kuu 300, kati ya 446, zimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili, hatua ambayo itaenda kuimarisha uelewa wa Sheria miongoni mwa Watanzania.


  Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara na Uwekezaji


MheshimiwaSpika; kwenye Hotuba yangu kwa Bunge niliahidi kuifungua nchi kiuwekezaji ili kukuza uchumi, kuzalisha ajira, kuongeza mapato na kupunguza kiwango cha umaskini kitaifa na kwa mtu mmoja mmoja. Tunaendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini (MKUMBI). Katika utekelezaji huu tulipitia  na kurekebisha sheria na kanuni 66 pamoja na kufuta au kupunguza tozo, ada na faini mbalimbali zipatazo 383. Kituo cha Uwekezaji (TIC) kimesajili jumla ya miradi ya uwekezaji 2,175 iliyopo kwenye sekta mbalimbali za uzalishaji na huduma. Miradi hiyo ina jumla ya thamani ya Dola za Marekani bilioni 25.53 na inatarajia kuzalisha jumla ya ajira 650,674 za moja kwa moja na nyenginezo. 


  Mheshimiwa Spika, jitihada za kuhamasisha uwekezaji katika  maeneo maalum ya kiuchumi (SEZ) pia zimevutia jumla ya miradi 45 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.17 iliyopatiwa leseni za EPZ na SEZ. Miradi hiyo iliyojikita katika sekta zinazozalisha bidhaa zitokanazo na kilimo, viwanda, mifugo, kemikali, madini na mazao ya misitu imeongeza ajira 20,674 na kuongeza ukuaji wa mauzo ya nje kwa Dola za Marekani milioni 397.64. Katika kuchochea uwekezaji Nchini, tumetunga Sheria ya uwekezaji na maeneo maalum ya kiuchumi ya mwaka 2025 ambayo, pamoja na mambo mengine, inaanzisha mamlaka ya uwekezaji na maeneo maalum ya kiuchumi, kwa pamoja.


Sekta za Uzalishaji

Kilimo

Mheshimiwa Spika, kilimo kimeendelea kuwa uti wa mgongo wa taifa letu kwa kutoa ajira nyingi na kuchangia kwa kiasi kikubwa pato letu la taifa. Kwa kutambua mchango wa sekta hii kwa maisha ya Mtanzania wa kawaida Serikali imeongeza bajeti ya kilimo kwa zaidi ya asilimia 300 kutoka Shilingi Bilioni 294 mwaka 2021 hadi Shilingi Trilioni 1.24 mwaka 2025. Shabaha yetu kuu ni  kuongeza tija, pamoja na kuweza kujitosheleza kwa chakula. 


Upatikanaji wa pembejeo bora  za kilimo

  Mheshimiwa Spika, katika kuongeza tija, Serikali imeongeza upatikanaji wa mbegu bora za kilimo kwa asilimia 41.9 kutoka tani 50,747 mwaka 2021 hadi tani 72,031.89 mwaka 2024. Aidha, uzalishaji wa mbegu bora ndani ya nchi umeongezeka kwa asilimia 61 kutoka tani 34,797 mwaka 2021 hadi tani 56,114 mwaka 2024.  Pia tumewezesha Maabara ya mbegu  ya Taasisi ya kudhibiti Ubora wa Mbegu ( TOSCI) kupata ithibati ya kimataifa ya uzalishaji mbegu. Hatua hii imewezesha uzalishaji mbegu bora unaoleta tija kwa wakulima.


  Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, Serikali imeongeza upatikanaji wa mbolea kutoka tani 678,017 mwaka 2021 hadi tani milioni 1.21 mwaka 2025. Hii ni sawa na asilimia 80.9 ya makisio ya mahitaji ya tani milioni 1.5 za mbolea kwa msimu wa mwaka 2025. Sambamba na hilo, Serikali imetoa ruzuku ya mbolea yenye thamani ya Shilingi Bilioni 300 kwa mazao yote. Hatua hiyo, imewezesha kuongezeka kwa matumizi ya mbolea kwa hekta kutoka kilo 19 mwaka 2021 hadi kilo 24 mwaka 2025, na hivyo kuongeza tija kwenye uzalishaji. Mbali na mbolea Serikali pia imekuwa ikihakikisha upatikanaji wa viuatilifu  pamoja na huduma za ugani kwa kuhakikisha inaajiri maafisa ugani pamoja na kuwapa vitendea kazi kama pikipiki, vishkwambi, visanduku vya ugani na soil scanners ili kuongeza tija kwenye kilimo chetu.


Usalama wa chakula

  Mheshimiwa Spika, tayari jitihada hizo za Serikali sio tu zimemfaidisha mkulima, bali pia zimeongeza kiwango cha uzalishaji wa mazao ya chakula kwa asilimia 33 kutoka tani milioni 17.1 mwaka 2021 hadi tani 22.8 mwaka 2024. Ongezeko hilo limeiwezesha nchi kuwa na utoshelevu wa chakula kwa asilimia 128, hatua muhimu kwa ustawi wa jamii na ustahimilivu wa uchumi pia. Pamoja na hayo, ili kulinda jasho la mkulima kwa kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, tumejenga maghala 46 na vihenge 20 vyenye uwezo wa kuhifadhi mazao tani 219,921.


  Mheshimiwa Spika, miongoni mwa maeneo mawili yaliyoibua mjadala kipindi hiki yalihusu sukari na mafuta ya kula. Ili kuimarisha upatikanaji wa sukari kunapokuwa na upungufu, tuliipa NFRA mamlaka ya kununua na kuhifadhi sukari kisheria. Sukari imeingia kwenye mazao ya usalama wa chakula ndani ya nchi. Niwashukuru Wabunge kwa kuunga mkono mabadiliko hayo. Na ninaamini tayari tumeshaanza kuona tofauti. Pamoja na hayo, Serikali inaendelea na jitihada za kuongeza uzalishaji wa sukari nchini kwa kuhamasisha ujenzi wa viwanda. Mbali na kiwanda kipya cha Bagamoyo chenye uwezo wa kuzalisha sukari tani 35,000 na Mkulazi chenye uwezo wa kuzalisha sukari tani 50,000, upanuzi wa kiwanda cha Kilombero utaongeza uzalishaji wa sukari kwa tani 271,000. Halikadhalika, upanuzi umefanyika kwenye mashamba ya Mtibwa (hekta 4,700) na Kagera (hekta 9,071). Hadi sasa, hatua hizi, zimeongeza uzalishaji wa sukari kutoka tani 311,358 mwaka 2020 hadi tani 392,724 mwaka 2024. Tunaendelea kuvutia uwekezaji zaidi kwenye viwanda na kupanua maeneo ya uzalishaji wa miwa tukilenga kufikia uzalishaji wa tani 700,000 za sukari.


  Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa msukumo pia katika kuongeza uzalishaji wa mafuta ya chakula. Hivyo, msukumo huo umewezesha uzalishaji mbegu za mafuta kuongezeka kutoka tani 1,713,178 mwaka 2021 hadi tani 2,181,603.65 mwaka 2024. Pamoja na hayo, uzalishaji wa mafuta ya kula nchini umefikia tani 396,335 tu. Hivyo, tunaendelea na hatua zitakazotuwezesha kuchochea uzalishaji zaidi wa mazao ya mafuta kuelekea lengo la tani 650,000. Aidha, tumedhamiriaa kuongeza usindikaji na uzalishaji wa mafuta ya kula nchini ili kupunguza uagizaji kutoka nje ambao, kwa kweli, unatugharimu fedha nyingi za kigeni.

 

Uzalishaji wa Mazao ya Biashara

  Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kilimo biashara, kuimarika kwa uzalishaji wa mazao ya biashara nchini kumeongeza thamani ya mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi kwa asilimia 67 kutoka Dola za Marekani Bilioni 2.1 mwaka 2021 hadi Dola za Marekani Bilioni 3.5 mwaka 2024. Pia, uzalishaji wa mazao asilia ya biashara umeongezeka kutoka tani 983,177 mwaka 2021 hadi tani 1,443,629.4 mwaka 2025. Tunacholenga ni kuongeza zaidi thamani ya mauzo nje ya nchi hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 5 ifikapo 2030.


Kilimo cha Umwagiliaji

  Mheshimiwa Spika,

 Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji ambapo eneo linalomwagiliwa limeongezeka kutoka hekta 561,383 mwaka 2020 hadi hekta 983,466.06 mwaka 2024. Hii inatokana na ongezeko la miradi ya umwagiliaji inayotekelezwa kutoka 13 mwaka 2020 hadi 780 mwaka 2025. Ni matumaini yetu kuwa kukamilika kwa miradi hii yote kutatuwezesha kufikia lengo tulilojiwekea la kufikia hekta 1,200,000 za eneo la umwagiliaji. Muhimu zaidi, katika jitihada hizi, Serikali imeamua kutekeleza miradi mikubwa ya umwagiliaji kwa kutumia maji ya Ziwa Victoria na Tanganyika ambayo itaunda Gridi ya Taifa ya Umwagiliaji kwa ajili ya eneo lenye ukubwa wa hekta 3,000,000, ambapo ujenzi wake unatarajiwa kuanza ndani ya miezi 18 kuanzia sasa. 


Maendeleo ya Ushirika

  Mheshimiwa Spika, Serikali katika kukuza sekta hii imewezesha kutimia kwa azma ya muda mrefu ya kuimarisha Ushirika kwa kuanzisha Benki ya Ushirika iliyoanza na mtaji wa Shilingi bilioni 58. Kuanzishwa kwa benki hiyo ambayo wanahisa wakubwa ni vyama vya ushirika vyenyewe kunajibu hitaji kubwa na la muda mrefu la upatikanaji wa mikopo zaidi kwa gharama nafuu, na hivyo kutaviwezesha Vyama vya Ushirika kujiimarisha kibiashara na kiuwekezaji.


  Mheshimiwa Spika,

Kupitia mfumo rasmi wa manunuzi, kiwango kilichouzwa kupitia ushirika kimeongezeka kutoka Tani 591,268.12 zilizouzwa kwa thamani ya Shilingi Trilioni 1.1 mwaka 2021 hadi Tani milioni 2.23 zenye thamani ya Shilingi Trilioni 4.2 mwaka huuongezeko linalokaribia asilimia 300.


  Vilevile, Serikali iliiongezea mtaji Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na hivyo kuongeza wigo wa upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wakulima. Dhamana ya mikopo kwenye sekta ya kilimo imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 63 mwaka 2020, hadi Shilingi bilioni 418.3 mwaka 2025, na tayari benki 19 zinatumia mfuko wa Dhamana wa Benki ya Kilimo kuongeza mikopo kwa wakulima.


Mifugo na Uvuvi

  Mheshimiwa Spika, Jitihada za kufungua masoko nje ya nchi, zimeongeza mauzo ya nyama  kutoka tani 1,774 zenye thamani ya dola za marekani milioni 4.2 mwaka 2020/2021, hadi kufikia tani 14,701 zenye thamani ya dola za marekani milioni 61.4 mwaka huu. Tarehe 17 Juni 2025, nilizindua kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa mifugo, inayolenga kulinda afya na kuongeza thamani ya mifugo yetu. Serikali katika kampeni hiyo itabeba nusu ya gharama ya chanjo ya mifugo ya ng'ombe na mbuzi, na gharama zote kwa kuku, na gharama zote za hereni za utambuzi.  Tuendelee kuhimiza matumizi bora ya ardhi kwa kuhamasisha watu wetu kutenga maeneo ya kilimo na ya ufugaji. Tuendelee kuhimiza vijiji vyetu kutekeleza mipango hiyo ili wafugaji wapate maeneo ya malisho mbali na mazao ya wakulima. Pia, tuhimize uhamilishaji kama mlango wa kuingilia kwenye kuboresha kosafu za mifugo yetu.  Ni vyema kuhimiza watu wetu kuachana na uchungaji na kujikita katika ufugaji. Nimnuku Rais Kikwete mchungaji hanenepi, na mfugaji hanenepi. 


  Mheshimiwa Spika, 

maboresho katika sekta ya uvuvi yamechangia upatikanaji wa ajira za moja kwa moja kwa wavuvi 201,661, wakuzaji viumbe maji 49,084 na takriban Watanzania milioni 6 wako katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na  uvuvi. Aidha, Serikali ilitoa mikopo iliyowezesha uwekaji  wa vizimba 1,636 na ununuzi wa boti 280. Vilevile, Serikali ilitoa boti 160 zenye thamani ya Shilingi bilioni 11.51 ambazo zimetoa ajira  13,180. Kutokana na uwekezaji huo, mazao ya uvuvi yameongezeka kutoka tani 477,018.48 zenye thamani ya Shilingi bilioni 2.77 mwaka 2021, hadi kufikia tani 543,598.91 zenye thamani ya Shilingi bilioni 3.04 mwaka 2025. 


  Mheshimiwa Spika, 

Serikali imeendelea kuimarisha biashara ya mazao ya uvuvi, ambapo mauzo yameongezeka kutoka tani 42,302.03 zenye thamani ya Shilingi bilioni 412 mwaka 2021, hadi tani 59,746.41 zenye thamani ya Shilingi bilioni 675 mwaka 2024. Tunaendelea na ujenzi wa mradi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko wenye thamani ya Shilingi bilioni 279.5 ambao umefikia asilimia 81.9. Kukamilika kwa bandari hiyo kunatarajia kuzalisha ajira takribani 30,000 na nchi kwa ujumla kunufaika zaidi na uvuvi wa bahari kuu.


Ujenzi 

  Mheshimiwa Spika, 

Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji ikiwemo kuongezeka kwa mtandao wa barabara za changarawe kutoka kilomita 24,493 mwaka 2020 hadi kilomita 44,372.21 mwaka 2025, na  mtandao wa barabara za lami kutoka kilomita 38,086.95 mwaka 2020 hadi kilomita 40,902.34 mwaka 2025.


  Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine yaliyopatikana ni kukamilika kwa ujenzi wa madaraja tisa (9) ambayo ni Gerezani na Tanzanite (Dar es Salaam), Wami (Pwani), Kitengule (Kagera), Kiyegeya (Morogoro), Ruaha (Morogoro), Ruhuhu (Ruvuma), Mpwapwa (Dodoma) na Daraja la Msingi (Singida). Vilevile, tumekamilisha ujenzi wa mradi wa kimkakati wa Daraja la Dkt. John P Magufuli (Kigongo - Busisi) ambalo niliwaongoza Watanzania kulizinduliwa rasmi tarehe 19 Juni 2025. Vilevile, Serikali imetekeleza miradi ya kupunguza msongamano wa magari na foleni katika majiji. Tumekamilisha mradi wa Miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), Awamu ya Pili kilomita 20.3 (Mbagala - Mzunguko wa Bandari (Bendera Tatu), Bendera Tatu - Kariakoo, Sokoine - Zanaki, Barabara ya Kawawa - Barabara ya Morogoro (Magomeni) na tunaendelea na utekelezaji wa Awamu ya Tatu, kilomita 23.3, kutoka katikati ya Jiji hadi Gongo la Mboto, ambayo imefikia asilimia 80, na Awamu ya Nne ya kilomita 30.1, kutoka katikati ya Jiji hadi Tegeta ambayo imefikia asilimia 22. Miradi hii itakapokamilka itaongeza ufanisi na tija. Tunaendelea kushughulikia changamoto na kasoro zilizopo ili wananchi waweze kunufaika ipasavyo na usafiri huo.


  Mheshimiwa Spika, 

Serikali pia inaendelea na ujenzi wa barabara ya Mzunguko wa Nje (Outer Ring Road)  katika Jiji la Dodoma yenye jumla ya urefu wa kilomita 112 ambapo utekelezaji kwa awamu zote mbili umevuka asilimia 80.  Vilevile, Serikali inaendelea na upanuzi wa Barabara Kuu ya TANZAM sehemu ya Uyole - Ifisi - Songwe Airport, Jijini Mbeya yenye urefu wa kilomita 36 kutoka njia mbili kuwa njia nne ambapo ujenzi umefikia asilimia 23.5. Miradi hii yote inaenda kuchochea shughuli za kiuchumi.


  Mheshimiwa Spika, 

kwa upande wa viwanja vya ndege, Serikali imekamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Nduli mkoani Iringa. Vilevile, inaendelea na ujenzi na ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma ambapo ukarabati umefikia asilimia 58, Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga ukarabati umefikia asilimia 60, Kiwanja cha Ndege cha Shinyanga ukarabati asilimia 80, Kiwanja cha Ndege cha Tabora ujenzi umefikia asilimia 93, Kiwanja cha Ndege cha Kigoma ujenzi umefikia asilimia 20, na Kiwanja cha Ndege cha Geita ujenzi umefikia asilimia 80. Aidha, ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato (Dodoma) sehemu ya kwanza inayohusisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua Ndege (runway), Barabara za maungio (Taxiways) na Maegesho ya Ndege umefikia asilimia 87. Sehemu ya pili inayohusisha ujenzi wa jengo la abiria, jengo la kuongozea ndege, Kituo cha Zimamoto, Kituo cha Hali ya Hewa, ujenzi umefikia asilima 53.22. Miradi hii itafungua zaidi anga la Tanzania, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuongeza fursa biashara, ikiwemo mazao ya mbogamboga, matunda na maua.


Uchukuzi 

  Mheshimiwa Spika, kwa upande wa reli, nililiahidi Bunge hili kuwa tutakamilisha ujenzi wa reli ya Dar es Salaam hadi Dodoma na kuendelea na ujenzi wa vipande vingine. Ninafurahi kusema kuwa awamu mbili zimeshakamilika na huduma kwa njia ya reli ya kisasa (SGR) kwa kipande cha Dar es Salaam - Morogoro - Dodoma zimeanza. Tangu safari za abiria zianze mwezi Agosti mwaka 2024, tayari jumla ya abiria 2,054,828 wamesafiri na maduhuli ya Shilingi bilioni 60.88 yamekusanywa. Kuanza kwa huduma za usafiri kwa reli hiyo kumeongoza tija kwenye uchumi, kwani kumefupisha safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma kutoka masaa 8 hadi 9 kwa gari hadi wastani wa masaa 3. Sasa, imekuwa kawaida mtu kuamka Dar es Salaam, kusafiri kuja Dodoma kwa reli kufanya shughuli zake na kisha kurejea Dar es Salaam jioni. Hii ni hatua kubwa katika maendeleo ya nchi yetu. 


  Mheshimiwa Spika, ujenzi wa vipande vingine vya  SGR unaendelea ambapo kipande cha kutoka Mwanza - Isaka (km 341) umefikia asilimia 63.16; Makutupora - Tabora (km 368) umefikia asilimia 14.53; Tabora - Isaka (km 165) umefikia asilimia 6.65; na Tabora - Kigoma (km 506) umefikia asilimia 7.81. Aidha, maandalizi ya kuanza ujenzi wa  kipande cha Uvinza - Malagarasi - Musongati (Km 282) kinachounganisha Tanzania na Burundi yameanza na tunatarajia kuzindua ujenzi hivi karibuni. Kutekelezwa kwa mradi huu wa SGR, kumezalisha ajira 9,376 pamoja na kampuni zaidi ya 792 za Watanzania kusaini mikataba kwa ajili ya kandarasi na huduma mbalimbali.


  Mheshimiwa Spika, Serikali pia imenunua mabehewa ya mizigo 264 ambapo kazi ya majaribio ya mifumo imefanyika. Ninafurahi kulijulisha Bunge hili kwamba, leo ni siku ya kihistoria kwenye reli yetu ya SGR kwa kuwa Shirika la Reli limeanza rasmi safari za mizigo kati ya Dar Es Salaam hadi Dodoma. Tunatarajia hatua hii ya kimageuzi nchini itapunguza muda na gharama ya uchukuzi, kuchochea biashara, na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama lango la biashara la Afrika Mashariki.


  Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, Serikali inaendelea na uboreshaji wa reli ya kati iliyokuwepo awali, yaani Metre Gauge Railway au MGR, ambayo inaendelea kutoa huduma kwa njia ya  Kati na Kaskazini sambamba na reli ya SGR. Katika kutekeleza azma hiyo, tumenunua vichwa vya treni vitatu, mabehewa ya abiria 22 na ya mizigo 44. Vilevile, jumla ya mabehewa 350 ya mizigo na 33 ya abiria yamekarabatiwa. 


  Mheshimiwa Spika, katika utoaji wa huduma za usafiri wa anga, niliahidi kuwa tutaendelea kuiboresha Kampuni yetu ya Ndege (ATCL) kimkakati ili iweze kujiendesha kwa ufanisi. Katika kipindi hiki, Serikali imenunua ndege sita za abiria na moja ya mizigo, na hivyo kufanya ATCL kuwa na jumla ya ndege 16 hadi Aprili, 2025. Ununuzi wa ndege hizo umesaidia nchi kuwa na usafiri wa anga wenye uhakika, na wenye muunganiko wa safari za ndani, kikanda na kimataifa. Ndege zetu sasa zinaenda  hadi China, India, Kenya, Dubai na  DRC, na mwaka huu zitaanza kwenda Nigeria, Msumbiji, Oman na Angola. Ununuzi wa ndege ya mizigo imepunguza hasara kwa wazalishaji na kujenga mtangamano wa uzalishaji wa ndani na soko la kimataifa. Vile vile, kuimarishwa kwa ATCL kumekuwa kichocheo cha ukuaji wa sekta nyingine, ikiwemo utalii, na kumesaidia katika kuitangaza nchi yetu kimataifa. Hivyo, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha tunafanya jitihada za makusudi ili ATCL iweze kuimarika zaidi na kujiendesha kwa tija. 

 

  Mheshimiwa Spika, kwa upande wa bandari, maboresho ya bandari zetu za Tanzania na ushirikishwaji wa Sekta Binafsi kwenye uendeshaji wa baadhi ya gati imewezesha kupunguza  Wastani wa muda wa meli kusubiri nangani umepungua kutoka siku 46 hadi siku saba (7); muda wa meli za makasha kusubiri nangani umepungua kutoka siku tano na sasa  huingia moja kwa moja gatini pindi zinapowasili katika Bandari ya Dar es Salaam; Idadi ya makasha iliyohudumiwa imeongezeka kwa asilimia 35 kutoka makasha  159,807 hadi  215,286; na jumla ya uzito wa shehena iliyohudumiwa imeongezeka kwa asilimia 14 kutoka shehena tani milioni 14.824 hadi tani milioni 16.870. 


  Mheshimiwa Spika, uwekezaji uliofanywa umeongeza makusanyo ya mapato ya Serikali, hususan yale yatokanayo na kodi, kutoka wastani wa Shilingi bilioni 850 kwa mwezi kwa mwaka 2023/24, hadi Shilingi trilioni moja (1) kwa mwezi mwaka 2024/25; na umepunguza matumizi kwa takribani Shilingi bilioni 100 kwa mwezi, kutoka wastani wa Shilingi bilioni 262.153 kati ya mwezi Mei 2023 na Machi 2024, hadi  Shilingi bilioni 166.323 kati ya mwezi Mei 2024 hadi Machi 2025. Pia tunaendelea kufanya maboresho katika bandari zetu za Mtwara na Tanga. 


  Mheshimiwa Spika, uboreshaji wa Bandari ya Mtwara uliohusisha ujenzi wa gati, uzio na barabara inayounganisha gati jipya na maeneo mengine katika bandari umekamilika. Hatua hiyo imesaidia wananchi wa Mtwara na maeneo ya jirani kuongeza biashara na uwekezaji pamoja na kurahisisha usafirishaji wa mizigo kwa gharama nafuu, hususan mazao ya korosho, ufuta na makaa ya mawe.  

  Mheshimiwa Spika, sambamba na uboreshaji wa bandari zilizopo katika bahari ya Hindi, Serikali pia imeendelea kuongeza wigo wa huduma za kibandari kwa kujenga na kuboresha bandari zilizopo katika maziwa makuu nchini. Kazi kubwa zilizofanyika ni pamoja na kukamilisha uboreshaji wa Bandari ya Kemondo, kuendelea na uboreshaji wa Bandari ya Bukoba, ambao umefikia asilimia 94 na Bandari ya Mwanza North ambao umefikia asilimia 58. 


  Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha ukarabati wa boti MV Tangazo iliyopo Tanga pamoja na matengenezo ya Boti MV Mkongo iliyopo Pwani ambazo zimeanza kutoa huduma. Vilevile, tunaendelea na ukarabati mkubwa wa vivuko vingine ambao umefikia hatua tofauti: MV Kilombero II , MV Nyerere, MV Old Ruvu, MV Magogoni, MV Ukara, na MV Kigamboni na MV Pangani II vipo katika hatua tofauti. Pia, tunaendelea na ujenzi wa vivuko vipya sita (6) kama ifuatavyo: Bwiro-Bukondo, Kisorya-Rugezi, Ijinga - Kahangala, Nyakaliro-Kome, Buyagu - Mbalika na Nyamisati - Mafia. Sambamba na hayo, ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza katika Ziwa Victoria unakamilika ndani ya muda mfupi. Pamoja na juhudi hizi Serikali inakaribisha Sekta Binafsi kuwekeza katika maeneo ya vivuko Nchini.


Mawasiliano na Teknolojia ya Habari


  Mheshimiwa Spika, katika sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari, Serikali imefanikiwa kuongeza mtandao wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kutoka kilomita 8,319 hadi 13,820 sawa na ongezeko la asilimia 66; kuongeza Wilaya zilizounganishwa na Mkongo kutoka 36 mwaka 2020 hadi Wilaya 109 hivi sasa; na kukamilisha vituo 111 vya kutolea huduma za mkongo wa mawasiliano. Aidha, Serikali imepunguza gharama za intaneti na kupiga simu ndani na nje ya Nchi.


  Mheshimiwa Spika, vilevile, minara ya mawasiliano imeongezeka kutoka 754 mwaka 2020 na kufikia 9,278 mwaka 2025. Minara hiyo imewezesha upatikanaji wa mawasiliano kwenye maeneo yenye changamoto na kuchagiza maendeleo ya uchumi kupitia biashara mtandao. 


  Mheshimiwa Spika, vilevile, kadri matumizi ya mifumo ya kidijitali inavyokua kwenye kila sekta, ndivyo kumeongezeka haja ya kujipanga kuhakikisha mageuzi ya kidijitali yanatuletea fursa zaidi. Ni kwa msingi huo, tuliandaa Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa miaka kumi (2024-2034) na Mkakati wa Taifa wa Brodibandi (2021-2026) inayolenga kujenga miundombinu wezeshi ya kidijitali, kuweka sera rafiki kwa uchumi wa kidijitali, kuimarisha ujuzi wa masuala ya kidijitali na kukuza utamaduni wa ubunifu miongoni mwa watu wetu.


  Mheshimiwa Spika, miongoni mwa wadau muhimu katika ubunifu tunapojenga uchumi wa kidijitali ni Kampuni Changa maarufu kama Start-Ups hususan kwenye eneo la TEHAMA. Kipindi hiki Serikali imeimarisha mashauriano na wadau wa sekta hii, na nimekuwa ninasititiza kuwa ninataka kuona Serikali inazisaidia Start-Ups ili vijana watumie ujuzi wao kuongeza tija kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Ili kukuza kampuni hizo, Serikali itatunga Sera kuendeleza kampuni changa (Start-Up Policy). Aidha tutaendeleza miradi ya ubunifu (innovations) 464 iliyotokana na mashindano ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU); na tumeanzisha Mfuko wa Bunifu ujulikanao kwa jina la SAMIA Innovation Fund ili kuwezesha utoaji wa mikopo nafuu kwa wabunifu, kuanzisha kampuni na kuingiza bidhaa sokoni.


Madini


  Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa sekta ya madini. Tumeimarisha masoko na minada ya uuzaji madini, ambapo vituo vya  ununuzi wa madini vimeongezeka kutoka vituo 61 Novemba, 2020 hadi 109 mwaka huu, na masoko ya madini yameongezeka kutoka 41 hadi 43. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi, imeanzisha viwanda vya usafishaji wa dhahabu kwa kiwango cha kimataifa katika Mikoa ya Mwanza, Dodoma, Dar es Salaam, Geita na Chunya. Vilevile, tumeendelea kuimarisha Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) kama nilivyoahidi ili kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za madini. Serikali pia imeisimamia sekta hii na kuiwezesha kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa kutoka asilimia 6.8 mwaka 2020, hadi kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025. Ninafurahi kulijulisha Bunge lako kwamba tumeweza kufikia lengo hili mwaka 2024, kabla ya muda tuliokuwa tumepanga ikimaanisha Watanzania wananufaika zaidi na rasilimali zao.


  Mheshimiwa Spika, vile vile tumetekeleza ahadi ya kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kununua mitambo ya uchorongaji iliyosambazwa katika maeneo ya Tambi - Mpwapwa; Nyawa - Bariadi; Matondo, Makongolosi na Matundasi yaliyoko Chunya; Lwamgasa, Nyaruyeye, Nyamalimbe na Nyakagwe yaliyoko Geita; Mavota - Biharamulo; Endabash - Karatu; Mwakitolyo - Shinyanga; na Mbangala - Songwe. Aidha, Serikali imefuta leseni na maombi 2,648 ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata maeneo halali ya uchimbaji, ili wazidi kuimarika. Kwa sasa, mchango wa wachimbaji wadogo umefikia asilimia 40 ya mapato yote yatokanayo na sekta ya madini.


Maliasili na Utalii

  Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mahsusi ili kuhakikisha sekta ya maliasili na utalii inakua zaidi, na kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa. Hatua hizi zimechangia kuongezeka idadi ya watalii wa kimataifa kwa asilimia 132.1 kutoka watalii 922,692 mwaka 2021, hadi watalii 2,141,895 mwaka 2024. Vilevile, idadi ya watalii wa ndani imeongezeka kwa asilimia 307.9 kutoka watalii 788,933 mwaka 2021, hadi kufikia watalii 3,218,352 mwaka 2024. Hatua hii imewezesha vijana wengi wa kitanzania kupata ajira za moja kwa moja kwenye sekta ya utalii katika vituo na kwa kufungua kampuni zao binafsi za utalii. Idadi ya wakala wa biashara za utalii zimeongezeka kutoka 2,885 mwaka 2020 hadi 3,735 mwaka 2025, na kwa idadi ya waongoza watalii imeongezeka kutoka 5,076 mwaka 2020 hadi 7,862 mwaka 2025. Vilevile, mapato yatokanayo na utalii yamepanda kutoka Dola za Marekani milioni 700  mwaka 2020, hadi Dola za Marekani bilioni 3.9 mwaka 2024, kwa watalii wa kimataifa, na kutoka Shilingi bilioni 46.3 hadi Shilingi bilioni 209.8 kwa watalii wa ndani katika kipindi hicho. Mheshimiwa Spika, Tarehe 1 Desemba 2024, Jijini Arusha, nilifanya mkutano na wawakilishi wa wakazi wa Eneo la Hifadhi la Ngorongoro. Mazungumzo yale yaliangazia masuala makubwa mawili, matumizi ya ardhi na haki mbalimbali, na pili ni changamoto zilizojitokeza wakati wa zoezi la uhamaji kwa hiari wa wakazi wa eneo hilo kwenda eneo la Msomela, Wilaya ya Handeni, Tanga. Katika mkutano huo nilipata fursa ya kusikiliza malalamiko yao pamoja na kupata maoni na ushauri wao juu ya njia bora ya kulishughulikia suala la uhamaji wa wakazi wa eneo hili. Kwa kuwa malalamiko yalikuwa mengi na mazito, niliamua kuunda Tume mbili ili kuangalia kwa kina suala hili kwa lengo la kupata suluhu ya kudumu. Tume hizo mbili zinatathmini masuala ya ardhi na zoezi la uhamaji kwa hiari, na zitakuja na mapendekezo kwa Serikali.


Ardhi

  Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuimarisha utawala na usimamizi wa ardhi, Serikali imeboresha Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995 itakayosaidia kuboresha sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu . Ni matarajio yetu kuwa kila kipande cha ardhi nchini kitapimwa na kumilikishwa kihalali kwa shughuli za kiuchumi na kijamii ili kuondoa matumizi holela na migogoro ya ardhi. Vilevile, tutaimarisha mamlaka za utatuzi wa migogoro hii, na kuongeza matumizi ya TEHAMA katika utoaji huduma. 


  Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Novemba, 2020 hadi Aprili, 2025, jumla ya Hatimiliki 356,642 zimesajiliwa, Hati za Hakimiliki za Kimila 318,868 zimetolewa kwa wananchi, na kukamilisha upimaji na uidhinishaji wa viwanja 1,427,005. Aidha, Serikali imeendelea kutumia Mfumo wa kielektroniki wa ardhi katika kutoa Hatimiliki. Hatua hizo zimeimarisha usalama wa ardhi, utambuzi wa kisheria wa umiliki wa ardhi, kuondoa migogoro ya ardhi, na kuongeza thamani na usalama wa ardhi. Ili kuondoa migogoro ya ardhi, Serikali inajipanga kuanzisha Tume ya ardhi ili kuimarisha usimamizi wa ardhi Nchini.


Nishati 

  Mheshimiwa Spika, 

Kutokana na umuhimu wa sekta ya Nishati kwa maendeleo ya Nchi, niliahidi kuwa Serikali itaimarisha upatikanaji wa nishati nchini, hasa kwa kukamilisha ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere, na kufikisha umeme kwenye vijiji vyote. Ninafurahi kulitaarifu Bunge kwamba msukumo uliotolewa na Serikali umewezesha ongezeko kubwa la uzalishaji wa umeme kutoka MW 1,601.84 mwaka 2020 hadi MW 4,031.71 kwa sasa. Hali hii imechangiwa na ukamilishaji wa miradi mbalimbali ya uzalishaji na usambazaji umeme ikiwemo mradi wa kielelezo wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye MW 2,115. Vilevile, miradi mingine iliyokamilishwa katika kipindi hiki ni Mradi wa Kuzalisha umeme wa Kinyerezi I Extension MW 185 kwa kutumia gesi asilia na Mradi wa Rusumo ambao umetekelezwa katika Mto Kagera kwa ushirikiano wa nchi tatu (3) za Tanzania, Burundi na Rwanda kwa mgawanyo sawa wa umeme (MW 26.67). 

  Mheshimiwa Spika, Serikali pia, imekamilisha miradi ya usambazaji umeme ikiwemo mradi wa ujenzi wa njia za kusafirisha umeme yenye urefu wa kilomita 414 kutoka Singida - Arusha - Namanga; kilomita 144 kutoka Geita - Nyakanazi; njia ya Julius Nyerere hadi Chalinze; njia ya Nyakanazi hadi Kigoma; njia ya kilomita 115 kutoka Tabora  - Urambo;  njia ya kilomita 94 kutoka Rusumo-Nyakanazi; na kwenye njia ya reli (Standard Gauge Railway SGR). Mafanikio hayo yameongeza upatikanaji wa nishati ya umeme ya uhakika katika maeneo mbalimbali Nchini. Aidha, tumefanikiwa kuiunganisha mikoa ya Kigoma na Katavi kwenye Gridi ya Taifa ya umeme. 


  Mheshimiwa Spika, 

vilevile, kama tulivyoahidi, tumefikia hatua kubwa na ya kistoria kwenye usambazaji, kwa kuweza kupeleka umeme kwenye vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara kama tulivyoahidi. Kwa sasa, tunaendelea na kazi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji, ambapo tayari vitongoji 33,657 kati ya 64,359 vimeshafikiwa, sawa na asilimia 52.3. Serikali pia ina mpango wa kuzalisha nishati mbadala kupitia vyanzo jadidifu lakini pia hivi karibuni wakati namuapisha Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco nilimuelekeza umuhimu wa kuanza kuzalisha nishati ya nyuklia. Aidha tunapanga kuweka ushindani kwenye sekta hii ya nishati kwa kualika sekta binafsi kushiriki ili kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika na nafuu.


Utendaji Kazi wa Mashirika ya Umma

  Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua mbalimbali kuimarisha utendaji kazi wa mashirika ya umma ili kuongeza mchango wake katika kujenga uchumi. Tulifanya mapitio na uchambuzi kuhusu uendeshaji wa Mashirika na Taasisi za Umma 248 ili kuongeza tija na mchango wa mashirika hayo katika kuleta maendeleo. Matokeo ya tathmini hiyo yameiwezesha Serikali kuanza zoezi la kuunganisha baadhi ya Mashirika na Taasisi, kurekebisha muundo wa Mashirika na Taasisi za Umma na hivyo kuimarisha usimamizi, kuongeza uwekezaji na kujiendesha kwa faida.


  Mheshimiwa Spika, maboresho hayo pia yameiwezesha Serikali kuongeza makusanyo ya gawio na michango kwa mwaka kutoka Shilingi bilioni 691.6 mwaka 2021 hadi Shilingi trilioni 1.028 mwaka 2025, ongezeko la Shilingi bilioni 336 kwa mwaka, zinazoenda kuboresha huduma kwa wananchi. 


Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi

  Mheshimiwa Spika, Serikali imeboresha sera, sheria na programu mbalimbali ili kuweka mazingira bora ya kuwawezesha wananchi kiuchumi. Vilevile, mifuko na programu mbalimbali zimeboreshwa, ikiwemo Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF); Mpango wa Mikopo ya asilimia 10 ya Mapato ya Ndani ya Halmashauri kwa ajili ya Wanawake, Vijana na Wenye Ulemavu; Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT); Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kwa Vijana; Programu ya Kukuza Viwanda Vidogo na vya Kati; Programu ya Imarisha Uchumi na Mama Samia (IMASA); Mfuko wa Dhamana wa Wajasiriamali Wadogo; Mfuko wa SELF Microfinance na Mpango wa kutenga asilimia 30 ya manunuzi ya taasiza za umma kwa wazabuni wanawake, vijanana Watu Wenye Ulemavu. Mifuko na programu hizo zimetoa zaidi ya Shilingi trilioni 3.64 kwa kuwanufaisha zaidi ya watu milioni 24.


Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini awamu ya tatu inayotekelezwa katika  maeneo yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, idadi ya wanufaika imeongezeka kutoka kaya 876,440 mwaka 2021 hadi kaya 1,371,916 mwaka 2025. Vilevile, jumla fedha zilizohawilishwa (yaani cash transfers) kwa walengwa katika kipindi hiki ilifika Shilingi trilioni 1.15. Kupitia fedha hizo, jumla ya miradi 27,863 yenye thamani ya Shilingi bilioni 291.7 ilitekelezwa na kaya 909,440 kufikia mwaka 2025 ikilinganishwa na miradi 3,185 yenye thamani ya Shilingi bilioni 38.6 na kaya 197,110 kwa mwaka 2020. 


Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa 


  Mheshimiwa Spika, nililiahidi Bunge kuwa tutaimarisha na kukuza uhusiano na mataifa mengine pamoja na jumuiya za kikanda na taasisi za kimataifa.  Tangu mwaka 2021, tulipata fursa ya kuwapokea viongozi mbalimbali wa kimataifa waliotutembelea na sisi kufanya ziara kwenye nchi rafiki kwa lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano. Ziara hizo zimeimarisha mahusiano, kutufungulia masoko na kutuongezea misaada na mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Sekta zilizonufaika zaidi ni pamoja na nishati, kilimo, mazingira, uchukuzi, afya, elimu, biashara na uwekezaji.


  Mheshimiwa Spika, baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kutokana na ziara hizo ni pamoja na kuongeza fursa ya masoko kwa mazao yetu mbalimbali. Kwa mfano, mwaka jana, Tanzania iliondolewa ushuru wa forodha kwa asilimia 100 kwa bidhaa zote zinazozalishwa nchini kwenda soko la China. 


  Mheshimiwa Spika, vilevile, Kuna miradi mbalimbali iliyonufaika moja kwa moja na ushirikiano huo, ikiwemo Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Upimaji na Ramani; na mradi Ujenzi wa Vyuo Vinne vya Ufundi na Mafunzo katika Mikoa ya Kigoma, Mwanza, Mtwara na Zanzibar. Nchi yetu itaendelea kuanzisha na kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Mataifa mengine Duniani ili kuendelea kunufaika na fursa zipatikanazo kwa mashirikiano hayo. Tumetembelewa na wageni kutoka mataifa mbalimbali makubwa ikiwemo Marekani, Ujerumani, Indonesia pamoja na Wakuu wa Taasisi za Kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika na mimi na wasaidizi wangu Makamu wa Rais, Waziri Mkuu tumefanya ziara kwenye  mabara ya Ulaya, Amerika, Afrika, Asia na Mashariki ya Kati.


  Mheshimiwa Spika, Serikali pia imevutia mikutano mikubwa nchini, ikiwemo Mkutano wa Nishati Barani Afrika, Mkutano wa Afrika kuhusu Rasilimali Watu, na  Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika, iliyoiwezesha Tanzania kuchangia kutoa utatuzi wa changamoto zinazolikumba bara letu. Vilevile, Tanzania imekuwa mwenyeji wa mikutano mbalimbali ya Kikanda, ikiwemo ile iliyolenga kutafuta amani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo kwa mara ya kwanza, tulifanikiwa pia kufanya mkutano uliozileta pamoja Jumuiya mbili za kikanda, yaani EAC na SADC. 


  Mheshimiwa Spika, kutokana na kuimarika kwa nafasi yake kimataifa, Tanzania ilipata heshima ya kushiriki majukwaa mbalimbali kwa mara ya kwanza na kuchangia mwelekeo wa sera za ushirikiano wa kimataifa, ukiwemo Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa G20, na mkutano wa BRICS, hatua iliyokuza zaidi ushawishi wetu kimataifa. Kupitia majukwaa haya, pamoja na mengi mengine, tuliweza kutoa msukumo kwa ajenda ya upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa ajili ya kulinda mazingira na afya za watu wetu.

  Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki, Tanzania ilishika nafasi mbalimbali za kikanda. Tanzania ilichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kwa vipindi viwili, na kwa sasa ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, ambapo tulipata fursa ya kusimamia chaguzi kadhaa ikiwemo za Msumbiji; Namibia, Botswana na Mauritius. Pia tumo kwenye Kamati tendaji ya Umoja wa Afrika ambapo mwaka 2028 tutachukua Uenyekiti wa Umoja huo na hivyo kwa mara ya kwanza Umoja huo utatoa Mwenyekiti mwanamke.. Vilevile tulipata fursa ya kuchangia misheni za ulinzi wa Amani nchi DRC na Msumbiji chini ya SADC. Majukwaa yote haya yaliiwezesha Tanzania kuchangia katika jitihada za kuimarisha amani na utulivu katika bara letu. Vilevile, Watanzania mbalimbali walichaguliwa kushika nafasi za kimataifa, ikiwemo Prof. Mohamed Janabi, aliyechaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Afrika wa Shirika la Afya Duniani.


  Mheshimiwa Spika, nililiahidi Bunge kwamba tutaimarisha utendaji kazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ikiwa ni pamoja na Balozi zetu. Hivyo, pamoja na kuajiri watumishi wapya (ajira 148) kwenye Wizara na kupeleka watumishi katika Balozi zetu (128) na niliahidi watarudi kwa wakati na mwaka huu tuna mpango wa kuwarudisha na kupeleka wapya ili tujenge kizazi cha diplomasia chenye uzoefu. Pia niliunda Tume ya Rais ya kutathmini Utendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambayo iliwasilisha ripoti na mapendekezo ambayo tunaendelea kuyatekeleza. Moja ya mapendekezo ambayo tumekamilisha ni Uzinduzi wa  ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, Toleo la 2025,. Sera hiyo inalengo la kuhakikisha mikakati yetu inajibu mazingira ya sasa. Vilevile, tumechukua hatua ya kuirejesha hadhi ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim, maarufu kama Chuo cha Diplomasia. Vilevile tumeanzisha Balozi mpya katika nchi za Austria na Indonesia, na  Konseli kuu za Guanzghou  Jamhuri ya Watu wa China  na Lubumbashi  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hatua hiyo imefanya nchi yetu kuongeza balozi zake kutoka 43 hadi 45 na konseli 3 hadi 5. Pia kupitia  Diplomasia  tumeweza  kushawishi nchi zifuatazo kufungua Konseli Kuu na Konseli za Heshima Zanzibar nchi hizo ni UAE ( Konseli Kuu Zanzibar) na zilizofungua Ofisi za Uwakilishi wa Heshima ni Ufaransa, Uingereza, Italia, Ujerumani, Hispania, Sweden na Brazil na kuchochea fursa za biashara, utalii, uwekezaji hususan katika sekta uchumi wa buluu. Aidha tumenunua majengo ya ubalozi nchini Namibia ukarabati wa majengo ya Ubalozi nchini Ubelgiji, Sweden pamoja na ujenzi wa Balozi zetu katika nchi ya Kenya. Katika kuboresha utendaji wa Wizara tumeweka Katibu Mkuu wa anaesimamia Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Naibu Waziri. Vilevile, tumeunda Idara ya Diplomasia ya Uchumi pamoja na Idara ya Mikakati na Siasa za Ulimwengu. Aidha tumenunua majengo ya ubalozi nchini Namibia ukarabati wa majengo ya Ubalozi nchini Ubelgiji, Sweden pamoja na ujenzi wa Balozi zetu katika nchi ya Kenya. Katika kuboresha utendaji wa Wizara tumeweka Katibu Mkuu wa anaesimamia Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Naibu Waziri. Vilevile, tumeunda Idara ya Diplomasia ya Uchumi pamoja na Idara ya Mikakati na Siasa za Ulimwengu.


Ushirikishwaji wa Wana-diaspora katika Maendeleo ya Taifa

   Mheshimiwa Spika, kupitia maboresho ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, Toleo la Mwaka 2024, tunalenga kurahisisha ushirikishwaji wa wana-diaspora kwenye uchumi.


Ukuzaji wa Fursa za Ajira 

  Mheshimiwa Spika, hatua zote hizi nilizozitaja kuhusu masuala ya kiuchumi kwa pamoja zimechangia jitihada za Serikali kuongeza fursa za ajira nchini, kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali, ambapo kwa kushirikiana na sekta binafsi, katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025, jumla ya ajira 8,084,204 zimezalishwa. Tutaendeleza jitihada hizi kwani nguvu kazi kubwa tuliyonayo ni mtaji mkubwa wa kusukuma maendeleo ya nchi yetu.  


Maslahi ya Watumishi wa Umma 

  Mheshimiwa Spika, katika kutambua mchango wa mtumishi wa umma katika maendeleo na ustawi wa Taifa letu, Serikali imechukua hatua mbalimbali kuboresha maslahi yao. Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha mifumo ya ushughulikiaji wa maslahi ya watumishi wa umma, kuwajengea uwezo, pamoja na kuwapatia vitendea kazi. Katika kipindi hiki, jumla ya watumishi wa umma 611,063 wa kada mbalimbali wamepandishwa vyeo, 42,557 wamebadilishwa kada, na 9,620 wamefanyiwa mabadiliko ya mshahara binafsi. Aidha, katika kipindi hiki watumishi wapya 135,626 wameajiriwa katika Taasisi mbalimbali za umma. Aidha, Serikali imeendelea kulipa jumla ya Shilingi bilioni 252.76 za  malimbikizo ya mishahara ya watumishi 150,647 , na Shilingi bilioni 33.29 za malimbikizo ya mishahara ya wastaafu 10,022.


  Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, Serikali imeongeza mshahara wa kima cha chini kutoka Shilingi 370,000 hadi Shilingi 500,000 sawa na ongezeko la asilimia 35.1. Aidha, imetoa ajira katika Taasisi mbalimbali za umma kwa watumishi 135,626. Vilevile, jumla ya nafasi za ajira 155,008 zilitolewa na vibali vya ajira mbadala, ambapo 41,673 vilitolewa ili kujaza nafasi zilizobaki wazi kwa sababu mbalimbali.


Huduma za Serikali Mtandao

  Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa kutumia Mtandao wa Mawasiliano Serikalini (GovNet), Vituo vya Serikali vya kuhifadhia Mifumo, Data na Masafa ya Intaneti ili kuondoa urudufu, kupunguza gharama, kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa umma pamoja na kuhakikisha uwepo wa usalama wa mawasiliano Serikalini.  Sasa, mifumo ya Taasisi mbalimbali za Umma inabadilishana taarifa baada ya kujenga Mfumo Mkuu wa kuiwezesha mifumo ya TEHAMA Serikalini kubadilishana Taarifa (Government Enterprise Service Bus - GoVESB). Aidha, kufuatia msisitizo wangu wa kutaka mifumo ya Serikali kusomana, eneo jingine ambalo tumefanikiwa ni kuunganisha mifumo ya Serikali 898 ya kutolea huduma. Kati ya hiyo, mifumo 514 ni ya Serikali na mifumo 384 ni ya sekta binafsi. Uunganishaji wa mifumo umeongeza ufanisi katika utoaji na upatikanaji wa huduma za Serikali kwa umma kupitia Serikali mtandao.


  Mheshimiwa Spika, jitihada za Serikali yetu zimeifanya Tanzania kutambuliwa kimataifa katika matumizi ya TEHAMA Serikalini, ambapo kwa mujibu wa utafiti wa Benki ya Dunia kuhusu Ukomavu wa Matumizi ya Teknolojia Duniani, nchi yetu imepanda daraja kutoka kundi B hadi kundi A katika utoaji wa huduma za Serikali na ushirikishwaji wa wananchi (GovTech Maturity Index). Hivyo, tumeshika nafasi ya kwanza kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki, ya pili barani Afrika na  nchi ya 26 Duniani.


  Mheshimiwa Spika, vilevile, katika kuimarisha usalama wa taarifa za watu, tumeanzisha Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya Mwaka 2022, pamoja na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi inayosimamia utekelezaji wake. Sheria hiyo imewezesha uwepo wa usalama na faragha ya taarifa za mtu, watu au Taasisi. 


Anwani za Makazi 

  Mheshimiwa Spika, Kwa kutambua umuhimu wa Mfumo wa Utambuzi wa Anwani za Makazi katika kurahisisha mawasiliano, utoaji, upokeaji na ufikishaji wa huduma na ufanyaji wa shughuli za kijamii, kiuchumi na kiutawala, nilielekeza mfumo huo ukamilishwe kwa njia ya Operesheni. Kwa sasa, taarifa za anwani za makazi ziliongezeka kutoka 350,000 mwaka 2020, hadi 12,853,657 mwaka 2025. Kwa upande wa miundombinu ya anwani za makazi, vibao vya namba za nyumba vimeongezeka kutoka 300,125 mwaka 2020, hadi 7,440,812 mwaka 2025. Vilevile, nguzo za majina ya barabara zimeongezeka kutoka 9,842 mwaka 2020 hadi 229,961 mwaka 2025.



HUDUMA ZA KIJAMII


Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari

  Mheshimiwa Spika, katika kuzungumzia huduma za kijamii, niruhusu nianze na sekta ya elimu. Pamoja na kuendeleza kazi nzuri ya ujenzi wa miundombinu katika sekta ya elimu, Serikali imeboresha Sera ya Elimu ya mwaka 2014 toleo la 2024  na mitaala ya elimu katika ngazi ya elimu ya awali, msingi, sekondari na elimu ya ualimu ili kuimarisha utoaji wa elimu katika ngazi hizo na kujielekeza kutoa elimu ujuzi kulingana na mazingira ya Nchi na mahitaji ya soko la ajira.


  Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imeongeza bajeti ya sekta ya elimu kutoka Shilingi trilioni 4.72 mwaka 2020/2021, hadi Shilingi trilioni 6.16 mwaka 2024/2025, iliyosaidia kuimarisha miundombinu pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia. Pamoja na mambo mengine, Serikali imejenga shule 26 za sekondari za sayansi za wasichana kwa kila mkoa, shule 7 za sekondari za wavulana za sayansi kila kanda, na shule 103 za sekondari za amali ufundi; imeongeza vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari kutoka madarasa 191,708 mwaka 2020 hadi 254,393 mwaka 2025. Aidha, Serikali imeboresha shule 274 za michepuo ya kilimo na shule 28 za michepuo ya biashara; imetoa vifaa vya kisasa katika shule 28 za mchepuo wa elimu ya ufundi/amali; na imekamilisha ujenzi wa  nyumba  1,792 za walimu, maabara 638, maktaba 1,128, na mabweni 1,000.


  Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza mpango wa elimu bila ada kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita, na imeongeza bajeti ya mpango huo kutoka Shilingi bilioni 312.06 mwaka 2020, hadi Shilingi bilioni 796.38 mwaka 2024. Hatua hiyo, imewezesha kuongezeka kwa wanafunzi wanaonufaika na mpango huo kutoka 14,940,925 mwaka 2020, hadi 16,155,281 mwaka 2024. Vilevile, katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya elimu iliyo bora, Serikali imewarejesha shuleni wanafunzi 18,347 waliokatiza masomo kutokana na sababu mbalimbali.


Elimu Maalum

  Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza falsafa ya Asiachwe Mtu Nyuma (Leave no One Behind) katika elimu kwa kuandaa Mkakati wa Taifa wa Elimu Jumuishi Nchini wa Mwaka 2021/2022 - 2025/2026. Mkakati huo utaboresha mazingira ya utoaji wa elimu jumuishi kwa kuongeza nafasi ya mafunzo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na kukamilisha ujenzi wa shule jumuishi za mfano zikiwemo Lukuledi Mkoani Mtwara, Shule Maalum ya Sekondari Patandi Mkoani Arusha, na Shule Jumuishi ya mfano ya Awali na Msingi na Sekondari Mbuye iliyopo Mkoani Geita.


Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi

  Mheshimiwa Spika, katika kuongeza msisitizo kwenye ujuzi, Serikali imeongeza vyuo vya ufundi stadi kutoka 662 mwaka 2020, hadi 860 mwaka 2024, yaani ongezeko la vyuo 198. Jitihada hizo zimeongeza udahili katika vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi kutoka wanafunzi 344,815 mwaka 2020, hadi 446,251 mwaka 2025. Vilevile, imekamilisha ukarabati wa vyuo 10 vya VETA na 6 vya Ufundi Stadi na huduma za utengamao wa Watu wenye Ulemavu katika Mikoa ya Tanga, Tabora, Singida, Dar es Salaam na Mtwara. Vilevile, tumeanzisha vituo vya umahiri hususan katika sekta za nishati, kilimo na usindikaji, usafirishaji, TEHAMA na viwanda vya uzalishaji vilivyopo katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Mwanza.


Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu

  Mheshimiwa Spika, 

Serikali imeongeza mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kutoka Shilingi bilioni 464 mwaka 2020, hadi Shilingi bilioni 787.4 mwaka 2025. Kutokana na hatua hii, idadi ya wanufaika na mikopo ya elimu ya juu imeongezeka kutoka wanafunzi 142,170 mwaka 2020 hadi wanafunzi 248,332 mwaka 2025. Aidha, programu ya ufadhili inayojulikana kama SAMIA Scholarship imeanzishwa na, hadi sasa, imewanufaisha jumla ya wanafunzi 1,343 waliojikita kwenye masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi, hesabu na afya. Zaidi ya hapo, tumeanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya stashahada wanaosoma fani za kipaumbele, zikiwemo Afya, Sayansi na Ufundi ambapo Shilingi bilioni 19.95 zimetolewa kwa wanafunzi 7,534. Vilevile, Serikali iliondoa tozo ya asilimia 6 ya kulinda thamani ya fedha na asilimia 10 ya ucheleweshaji wa urejeshaji wa mikopo kwa wanufaika wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. 

Afya

  Mheshimiwa Spika,

Serikali imeendelea kujenga vituo vya kutolea huduma za afya, kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya, na kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongezeka kwa vituo vya kutolea huduma za afya (Health facilities) kutoka vituo 8,783 mwaka 2020, na kufikia 12,846 Aprili 2025, sawa na ongezeko la vituo 4,063. Ongezeko hilo limesogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi ambapo sasa asilimia 75 ya wananchi wanapata huduma za afya ndani ya kilomita 5 ya maeneo wanayoishi.


  Mheshimiwa Spika, nililieleza Bunge kuwa tutaendeleza kampeni ya 'Jiongeze Tuwavushe Salama' ili kuhamasisha uwajibikiaji wa wadau wote katika kupunguza vifo vya mama na mtoto. Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya kutoa huduma za afya ya Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda-Meta iliyopo katika Jiji la Mbeya iliyogharimu Shilingi bilioni 13.2 na ambayo tayari inatumika, pamoja na Hospitali za Rufaa za Mikoa za Sekou Toure (Mwanza), Geita, Simiyu, Mawenzi, Njombe na Songwe ambazo zimegharimu kiasi cha Shilingi bilioni 71.1. Vilevile, vituo vyenye uwezo wa kutoa huduma za upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni vimeongezeka kutoka 340 mwaka 2020, hadi 577.


  Mheshimiwa Spika,

Serikali imeongeza hospitali zenye majengo ya kutolea huduma za dharura kutoka 7 mwaka 2020, hadi 125 mwaka 2025. Kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya kutolea huduma za dharura kumepunguza vifo na kuokoa maisha kwa wagonjwa wa dharura na wa ajali. Vilevile, Serikali imeimarisha huduma za uchunguzi kwa kununua vifaa Tiba vya Uchunguzi ambavyo vinapatikana kuanzia ngazi ya Hospitali ya Taifa hadi Hospitali za Rufaa za Mikoa na Halmashauri. Vifaa tiba vilivyoongezeka ni pamoja na MRI kutoka 7 hadi 13, CT scan kutoka 13 hadi 45, Digital X-Ray kutoka 147 hadi 491 na Ultrasound kutoka 476 hadi 970.


  Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba aina 382 katika vituo vya umma imeongezeka kutoka asilimia 73 mwaka 2020 na kufikia asilimia 86.2 Aprili, 2025. Upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi unawezesha wananchi kupata mahitaji muhimu ya msingi katika vituo vya kutolea huduma za afya. Kutokana na kuimarika  kwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, kumekuwa na ongezeko la utalii tiba kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hizo kutoka nje ya nchi kutoka 5,705 mwaka 2020, hadi 12,180 mwaka 2025. Huduma za kibingwa na ubingwa bobezi zinazotolewa ni pamoja na uwekaji wa vifaa vya usikivu kwa watoto, upandikizaji wa figo, kuwekewa puto tumboni, upasuaji mgumu wa moyo bila kufungua kifua, upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua, upasuaji ubongo, upasuaji wa uti wa mgongo, upandikizaji wa nyonga bandia, na tiba ya saratani ya mlango wa kizazi.


Mapambano Dhidi ya UKIMWI


  Mheshimiwa Spika, utafiti wa viashiria na matokeo ya VVU na UKIMWI umeonesha kuwa tumefanikiwa kuvuka lengo kwenye utekelezaji wa shabaha ya asilimia 95 ya pili inayohusu Tiba kwa watu wenye VVU waliotambua hali zao, ambapo asilimia 98 wapo kwenye Tiba. Pia, utafiti katika shabaha ya Tatu inayohusu kufubaza Virusi kwa WAVIU wanaoendelea na tiba unaonesha kwamba asilimia 94 ya waliopo kwenye tiba ndio wamefubaza VVU. Aidha, katika kufikia shabaha ya kwanza inayohusu watu wote wanoishi na VVU kupima na kujua hali zao za maambukizi, asilimia 82.7 ya watu wanoishi na VVU nchini sasa wanajua hali zao. Pamoja na kupungua kwa baadhi ya misaada ya wabia wetu kutokana na mabadiliko ya sera zao, Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa haturudi nyuma katika kufikia shabaha ya 95-95-95. Afya za Watanzania itabaki kuwa kipaumbele cha kwanza cha Serikali. 


Maji 


  Mheshimiwa Spika, 

Ili kutimiza azma ya upatikanaji wa maji safi na salama kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya CCM, Serikali ilitekeleza mikakati na programu mbalimbali ikiwa ni pamoja na miradi ya usambazaji maji 2,331 mijini na vijijini. Aidha, miongoni mwa miradi mikubwa iliyotekelezwa ni pamoja na ifuatayo: Mradi wa kuboresha huduma ya maji katika Miji 28 ya Tanzania Bara kwa gharama ya Shilingi trilioni 1.3 ili kunufaisha wananchi wapatao 5,985,500; Mradi wa majisafi na usafi wa mazingira wa Arusha uliogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 520 na ambao umeongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 40 hadi lita milioni 200 kwa siku; Mradi wa muda mrefu wa Same-Mwanga-Korogwe uliogharimu Shilingi bilioni 406.1 na kunufaisha zaidi ya wananchi 456,930; na mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Miji ya Tinde na Shelui, ujenzi wa chujio la Butimba, mradi wa Mugango - Kiabakari - Butiama, na ule wa Orkesumet ambao umegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 200.86 na kunufaisha wananchi wapatao 1,048,910 na mifugo yao. 


  Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha uwezo wa utekelezaji wa miradi ya maji, Serikali imenunua mitambo 25 ya kuchimba visima, seti tano za mitambo ya kuchimba na kujenga mabwawa, na seti nne za vifaa vya uchunguzi wa maji chini ya ardhi. Mitambo hiyo imewezesha uchimbaji wa visima 1,749 na ujenzi wa mabwawa 16 katika maeneo mbalimbali nchini, na hivyo kuwawezesha wananchi kupata maji kwenye maeneo ya karibu na makazi yao.


  Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha ujenzi wa mabwawa 45 kwa ajili ya uvunaji wa maji ya mvua ili kuwezesha upatikanaji  maji hata wakati wa  kipindi cha ukame. Vilevile, Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda litakalokuwa na uwezo wa kutunza lita bilioni 190 za maji. Mradi huo utakaogharimu Shilingi bilioni 329.46 umefikia asilimia 29, na utapokamilika utasaidia kupunguza athari za kimazingira kwa kuimarisha utiririshaji wa maji katika mkondo wa Mto Ruvu kwa kipindi chote cha mwaka, kuwezesha mitambo ya kuzalisha maji ya Ruvu Juu na Chini na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.


  Mheshimiwa Spika, kwa ujumla jitihada za Serikali katika sekta ya maji zimewezesha hali ya upatikanaji wa maji mijini kuongezeka kutoka asilimia 84 hadi asilimia 91.6, na vijijini kutoka asilimia 70.1 hadi asilimia 85. Aidha, kuna miradi kadhaa inayoendelea na utekelezaji mijini na vijijini ambayo ikikamilika kwa sehemu kubwa tutaweza kutekeleza azma yetu ya kumtua Mama ndoo kichwani.


  Mheshimiwa Spika, 

vilevile ninafurahi kulijulisha Bunge kwamba tulikamilisha maboresho ya Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002, Toleo la Mwaka 2025, tukilenga kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji, kuimarisha utoaji huduma ya maji safi na usafi wa mazingira vijijini, kujipanga vizuri zaidi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, na kuboresha uratibu wa mipango ya pamoja kwa sekta zinazotekeleza miradi inayohusiana na maji, hususan sekta ya maji na sekta ya kilioHatua hizi zitazidi kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa maji safi na salama wakati wote.


Kinga na Hifadhi ya Jamii

  Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii ya Mwaka 2023 ambayo imeweka uratibu madhubuti na kuimarisha utekelezaji wa afua stahiki za kinga ya jamii. Utekelezaji wa sera hiyo pamoja na afua nyingine umesaidia kuongeza idadi ya wanachama wachangiaji kutoka 849,886 mwaka 2021, hadi 1,758,018 mwaka 2025. Vilevile, ulipaji wa mafao kwa wastaafu umeboreshwa kwa kufanya mabadiliko ya kikokotoo. Maboresho hayo yameongeza wigo wa malipo ya mkupuo kutoka asilimia 33 hadi asilimia 40 kwa waliokuwa wanalipwa asilimia 50 kabla ya kuunganisha mifuko mwaka 2018, na kutoka asilimia 33 hadi 35 kwa waliokuwa wanapata asilimia 25 Aidha, Serikali imeongeza kima cha chini cha pensheni kutoka Shilingi 100,000 hadi Shilingi 150,000 kwa mwezi na kuhuisha pensheni ya kila mwezi kwa kiwango cha asilimia mbili kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.


Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo


  Mheshimiwa Spika, kwa upande wa sanaa, kufuatia maboresho yaliyofanywa na Serikali, kiasi cha mirabaha kilichogawiwa kwa wasanii waliosajiliwa COSOTA kimeongezeka kutoka Shilingi milioni 245 hadi Shilingi milioni 687.7 na hivyo kuwezesha wasanii kupata fedha na kunufaika na kazi zao za sanaa. Vilevile, vibali vya wasanii wa ndani kwenda nje ya nchi kufanya shughuli za sanaa viliongezeka kutoka 122 hadi 1,492 na vibali vilivyotolewa kwa wadau kuingiza wasanii nchini kufanya shughuli za sanaa kutoka 75 hadi 623.

  Mheshimiwa Spika, kwa upande wa michezo, mafanikio mbalimbali yamepatikana; na kubwa ni Tanzania kufanikiwa, kwa mara ya kwanza, kuwa mwenyeji wa matukio makubwa ya michezo ya Kimataifa ya AFCON mwaka 2027, na CHAN mwaka huu wa 2025. Vilevile, vilabu vyetu ya mpira vya miguu, vya Simba, Yanga, Azam na nyingine, viliweza kufuzu kushiriki mashindano ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF). Tunawapongeza sana.


   Mheshimiwa Spika, Pamoja na mafanikio niliyoyabainisha si kwamba hakuna changamoto, bado zipo na zinaendelea kushughulikiwa. Kama nilivyosema awali, maendeleo ni hatua hivyo basi tunaendelea kufanyia kazi mipango na mikakati mbalimbali ili kuhakikisha  tunapunguza umasikini kwa kutumia rasilimali zetu, kuongeza uwajibikaji Serikalini, kupunguza matumizi yasiyo na tija na kupunguza utegemezi. Ni matumaini yangu kuwa mpaka 2030 Nchi itakuwa imefikia uchumi wa kati kiwango cha juu


Tunaamini wananchi watatupa ridhaa kupitia uchaguzi ujao ili tuweze kuendeleza jitahada za kuwaletea Wananchi maendeleo endelevu. 


HITIMISHO


Salamu za Shukrani

  Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha, nisisitize kwamba utendaji wa Serikali unapimwa kwa tathimini na takwimu. Mimi nimetumia takwimu kueleza utekelezaji wa ahadi zetu kwa wananchi lakini ninyi wawakilishi wa wananchi mnafahamu vyema kilichofanyika katika maeneo yenu. Mwenye macho haambiwi tazama! 


  Mheshimiwa Spika, Ninapoelekea kuhitimisha na kwa moyo mkunjufu nirudie kuwashukuru Watanzania wenzangu, kuanzia wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara, wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi hata wanasiasa, kwa kuiunga mkono Serikali. Watanzania tumeendelea kudhihirisha uungwana wetu, hususan kwa kudumisha amani na mshikamano, kuchapa kazi kwa bidii na kwa moyo wa uzalendo.


  Mheshimiwa Spika, kwa umuhimu wa kipekee, niwashukuru viongozi wenzangu wote wa Serikali tulioshirikiana katika kipindi cha miaka minne. Namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa ushauri na ushirikiano alionipa katika kutekeleza majukumu yangu. Namshukuru pia Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, na viongozi wengine wa SMZ kwa ushauri na ushirikiano walionipa. Vilevile, namshukuru na kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu, kwa hekima, unyenyekevu na uchapaji kazi mzuri. Nimshukuru Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, kwa kumsaidia Waziri Mkuu na kwa usimamizi wake wa sekta ya nishati. 


  Mheshimiwa Spika, vilevile, nitoe pia shukrani zangu kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Mheshimiwa Balozi Dkt. Moses Kusiluka, kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi, na kujitoa kwake bila kuchoka. Pia, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wote kwa kufanya kazi jitihada zenu. Nawashukuru pia Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu; Wakuu wa Mikoa; Makatibu Tawala wa Mikoa; Wakuu wa Wilaya; Makatibu Tawala wa Wilaya; Wakurugenzi wa Halmashauri; Maafisa Tarafa; Watendaji wa Kata na Vijiji, na Viongozi wa ngazi zote kwa kufanikisha kupatikana kwa mafanikio yote niliyoyataja. 

Shukrani nyingi kwa wasaidizi wangu wa Ofisi binafsi ya Rais (OBR).  Kwa upande mwengine, naishukuru sana nguzo ya matumaini yangu, hakika, bila maliwazo kutoka familia yangu kazi hii isingekuwa nyepesi.Hivyo, niwashukuru kwa kunielewa kwa kutokuwa nao kwenye shughuli muhimu za kifamilia na  kiukoo, mimi nikiwa mke, mama, dada, Shangazi na bibi, walikuwa wananikosa. Ninawashukuru wote. 

Nawashukuru sana!


  Mheshimiwa Spika, pia, nakishukuru Chama changu cha CCM, kwa kuisimamia vyema Serikali na kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 - 2025 inatekelezwa ipasavyo. Napenda kuwaahidi wanachama, wapenzi wa CCM na wananchi kwa ujumla kuwa tumejipanga kutekeleza Ilani ijayo kwa kauli mbiu ya  "KAZI NA UTU: TUNASONGA MBELE".


   Mheshimiwa Spika, Navishukuru pia vyama vyote vya siasa kwa ushirikiano wao kwa Serikali katika kipindi hiki cha miaka minne. Licha ya tofauti zetu za kisiasa na kiitikadi, ukweli ni kuwa sote ni Watanzania na tunajenga Taifa moja. Na wengi waliokuwa wakitukosoa au kukosa Serikali kwa nia ya kujenga, sio kupinga tu kila lililokuwa linafanywa, walikuwa wakisaidia kuboresha utendaji wa Serikali. 


  Mheshimiwa Spika, Nitumie fursa hii pia kuwashukuru viongozi wa dini nchini kwa sala na dua zao za kuliombea Taifa letu, na kutuombea sisi tuliokabidhiwa dhamana ya kuliongoza Taifa hili.

  Mheshimiwa Spika, Aidha, ninawashukuru wanahabari kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya ya kutoa taarifa na kuelimisha umma wa Tanzania pamoja na dunia nzima kwa ujumla kuhusu masuala mbalimbali ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nivishukuru sana vyombo vya ulinzi na usalama. Amani na usalama wa nchi inachangiwa sana na vyombo hivi.


  Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine, narudia kulishukuru Bunge lako la 12 kwa ushirikiano mkubwa liliotoa kwa Serikali katika kipindi cha miaka mitano. Mbali na kuishauri na kuisimamia Serikali, Bunge hili ndilo lililopitisha bajeti na miswada mbalimbali ya sheria iliyoiwezesha Serikali kutimiza majukumu yake kwa ufanisi. 


  Mheshimiwa Spika, napenda pia nitumie fursa hii kuwashukuru washirika na wadau wetu mbalimbali wa maendeleo kwa ushirikiano mkubwa waliotupatia. Ushirikiano wao ulitupa nguvu na ari ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Hivyo basi, tunawashukuru sana washirika wetu wa maendeleo, ambao kwa bahati nzuri, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, wakati akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Serikali, aliwataja moja baada ya mwingine, na mchango wao umetambuliwa na kuingia kwenye Hansard za Bunge hili. Ahsanteni sana, tunawashukuru sana!


Kuhitimisha Shughuli za Bunge

  Mheshimiwa Spika, nilianza kwa kusema kuwa, nimekuja kulihutubia na kuhitimisha shughuli za Bunge hili la 12 ili kuruhusu kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 2025. Uchaguzi ni zoezi la kikatiba na lenye umuhimu katika kukuza demokrasia nchini na kuwapa wananchi fursa ya kuchagua viongozi wanaowataka. Katika hilo, natambua kuwa baadhi yenu hapa mmeonesha nia ya kuwania tena nafasi zenu, na wapo waliotangaza kukaa pembeni. Hivyo, kwa wanaoendelea, niwatakie kila la kheri.


  Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Serikali tumejipanga kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki. Na Serikali itakuwa macho kipindi chote kusimamia sheria na utulivu wa nchi. Nitumie fursa hii kuhimiza vyama vyote vya siasa kutoa fursa za kutosha kwa wagombea Wanawake,  Vijana na Watu Wenye Ulemavu kugombea nafasi tofauti za uwakilishi. Vilevile ninawasihi wagombea kuepuka matusi, au vitendo ambavyo haviendani na mila, desturi na tamaduni zetu. Kama nilivyosema, sisi sote ni wamoja, hivyo, tubishane kwa hoja na tushindanishe kwaIlani zetu. Kamwe tusiruhusu uchaguzi uwe chanzo cha vurugu amani, bali tuhakikishe unakuwa nyenzo ya kuimarisha amani, utulivu na demokrasia nchini.


  Mheshimiwa Spika, Baada ya kusema hayo na kwa Mamlaka niliyonayo  chini ya ibara ya 90(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,  sasa ninayo heshima ya kutamka kuwa shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimehitimishwa, na Bunge litavunjwa rasmi tarehe 03 Agosti, 2025.



Mungu libariki Bunge la Tanzania!

Mungu wabariki Wabunge Wote!

Mungu ibariki Afrika!

Mungu ibariki Tanzania!

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!

Asanteni sana kwa kunisikiliza!





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI