1.0 Utangulizi
Watetezi wa Haki za Binadamu hapa nchini wana nafasi kubwa sana ya kuishauri jamii,
Serikali na vyama vya siasa kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu ustawi wa jamii,
amani , haki za binadamu , demokrasia , utawala wa sheria na maendeleo ya nchi kwa
ujumla. Watetezi wa haki za binadamu wamekuwa ni wadau wakubwa hapa nchini katika
michakato yote ya uchaguzi. Mara kadhaa wameshiriki katika kudai maboresho , kutoa
elimu ya uraia, elimu ya mpiga kura na pia kushiriki kama waangalizi wa mwenendo wa
michakato ya kidemokrasia hapa nchini.
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu ( THRDC) ni Mjumuiko wa Mashirika ya
Utetezi wa Haki za Binadamu zaidi ya 300 hapa nchini. Wanachama wa Mtandao wa
Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania mara kadhaa wamekuwa wakishauri viongozi wa
siasa hapa nchini pamoja na serikali kuhusu namna bora ya kutatua changamoto mbalimbali
za kijamii zikiwemo zinazoonekana kujitokeza wakati wote wa uchaguzi hapa nchini. Hivi
karibuni tumeshuhudia madai ya watanzania na vyama vya siasa kuhusu madai ya
umuhimu wa kufanya maboresho ya msingi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Vyama vya upinzania pamoja na watanania wameendelea kutumia mbinu mbalimbali
kufikisha ujumbe wao kwa viongozi wa nchi kuhusu madai haya ya maboresho. Wengine
wamefanya mikutano ya hadhara na wengine wameendelea kutumia mitandao na vyombo
vya habari kuelezea madai haya. Asasi za Kirai hapa Nchini pia walitoa ilani ya Uchaguzi
ambayo imesisitiza na kushauri serikali pamoja taasisi zote zinazosimamia uchaguzi
kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa huru na haki.
Tunatambua jitihada za Rais Samia kuhusu maboresho machachache yaliyofanyika katika
sheria zinazosimamia uchaguzi hapa nchini. Maboresho haya ni pamoja na wagombea wa
udiwani na ubunge kutopita bila kupingwa, Tume kuwa na mamlaka ya kuteua mtumishi
wa umma mwandamizi kuwa msimamizi wa uchaguzi na wafungwa kupiga kura kwenye
magereza. Maboresho mengine mazuri ni yale kuhusu upatikani wa wajumbe na viongozi
wa Tume ya Uchaguzi ambayo hata hivyo maboresho haya hayatumiki katika uchaguzi
huu. Pamoja na maboresho haya bado watanzania wanaona kuna maeneo mengine
yanayohitaji maboresho ya kikanuni , kisheria na kimatendo ili kuwa na uchaguzi huru na
haki. Umuhimu wa maboresho ya ziada ulidhihirika katika uchaguzi wa serikali za mitaaa
uliofanyika mwaka 2024. Uchaguzi huu ulikuwa na kasoro nyingi kama za wagombea wa
upinzani kuenguliwa ambazo pengine zingetoa nafasi ya kukaa kama Taifa kufanyia kazi
kasoro kama hizo na kuhakikisha hayatajirudia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Tunasikitika kuwa pamoja na madai yote haya ya msingi kutoka kwa wananchi, AZAKI
na wanasisa hapa nchini hadi sasa hatujaona jitihada za haraka zinazochukuliwa na
mamlaka husika walau kufanyia kazi hoja hizi au kutafuta muafaka wa kitaifa katika
kufanyia kazi hoja hizi. Utamaduni wa kujadiliana na kukaa kwenye meza ya majadiliano
kutatua kwa pamoja changamoto za kitaifa unazidi kupungua na kufanya umoja na
mshikamano wa kitaifa kuwa mashakani. Falsafa za Mhe Rais za 4R kuhusu maridhiano
na maboresho haionekani ikitumika vyema katika nyakati hizi ambazo pengine ndio falsafa
hii ingepaswa kutumika zaidi.
Kama watetezi wa haki za binadamu tumeguswa na kuhuzunishwa na kitendo cha
kukamatwa na kufunguliwa kesi ya uhani kwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Wakili Tundu
Lissu akiwa anafunga mkutano wa hadhara huko Wilayani Mbinga, Songea. Mazingira na
utaratibu uliotumika kumkamata Mhe Tundi Lissu haukuzingatia usalama wake, usalama
wa raia waliokuwa katika mkutano huo na pia usalama wa polisi wenyewe na amani ya
nchi. Nguvu iliyotumika ni kubwa wakati wa ukamataji na yenye kutia hofu kubwa kwa
wananchi kushiriki michakato ya uchaguzi. Jeshi la polisi kama walijua kuna tuhuma dhidi
yake wangemwita kwa wito au kumchukua kwa utaratibu wa kisheria nje na eneo la
mkutano halali kwa kuwa hata makosa anayostakiwa naye yanaonekana hayakutokea aneo
halilokamatiwa. . Hata hivyo, maneno anayotuhumiwa kuyatamka hayana uzito mkubwa
wa kufikia kuandikiwa kosa la uhaini. Uhaini ni kosa kubwa hapa nchini lisilokuwa na
dhamana na lenye adhabu ya kifo au maisha. Ni kosa ambalo kwa miaka kwa miaka mingi
sasa hapa nchini halijawahi kutumika pengine kutokan na uzito wake.
Ikikumbukwe kipindi hiki ni cha kuelekea uchaguzi na dhahiri kuwa lazima kutakuwa na
kauli mbalimbali kutoka kwa wanasiasa na wananchi ambazo zinaweza zisiwapendezeshe
makundi mengine au serikali. Kinachotakiwa wakati huu ni watu kuwa na uvumilivu wa
hali ya juu ili kuepuka kuvunja amani ya nchi. Pamoja na kuwa haki ya kujieleza ni muhimu
sana wakati wa uchaguzi , wananchi, watetezi na wanasiasa wote wanapaswa kuwa makini
na kauli zao ili kuepuka kujiingiza katika migongano ya kisheria. Wakati huo huo vyombo
vya dol ana viongozi walioko Madaraka wanapaswa pia kuwa makini na kuepuka kutumia
vyombo hivi vya dola vibaya dhidi ya makundi ya wanasiasa wa upinzani hapa nchini. Sisi
kama watetezi wa haki, amani na utulivu hapa nchini tunajukumu la kukumbusha haya na
kushauri makundi yote ya kijamii na serikali kuepuka kwa namna yoyote ile mazingira
ya kukandamiza demokrasia, kuvunja haki, kupoteza amani pamoja na kuvunja sheria za
nchi.
2.0 Mapendekezo Kuhusu Muafaka wa Kitaifa Kuelekea Uchaguzi Mkuu
Ili kulisaidia Taifa kwenda katika uchaguzi tukiwa wamoja na wenye utulivu Mtandao wa
Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) unapendekeza kupatikana kwa
“MUAFAKA WA KITAIFA” Muafaka huu wa Kitaifa ni muhimu sana kwa kuwa utatoa
nafasi ya hofu na duku duku zote kufanyiwa kazi kabla ya kwenda kwenye uchaguzi.
a) Wahusika wa Muafaka Huu
Suala la uchaguzi ni la Watanzania wote, hivyo tunapendekeza Muafaka huu wa Kitaifa
uwakusanye makundi yote ya kijaamii kama viongozi wa dini, asasi za kiraia, vyama vya
siasa na tasisi za kiserikali. Tunapendekeza mchakato huu wa kutafuta muafaka wa Kitaifa
usimamiwe na wazee wenye uzalendo na hekima hapa nchini na wasiokuwa na maslahi
yoyote na uchaguzi. Na tunashauri wadau wote washiriki mchakato huu wakiwa na roho
inayoamini katika dhana ya maridhiano na kuwa tayari kuachia kidogo ili kupata kidogo
(Win Win Situation). Kwa muda mrefu sana watanzania tumekuwa tukidhani swala la
maboresho na swala la uchaguzi ni swala la wanasiasa pekee. Sababu mojawapo pia
zilizochangia mambo mengi kukwama hapa nchini kama vile mchakato wa Katiba ni swala
la kuwachia na kuwahusisha wanasiasa pekee katika mambo ya msingi ya kitaifa. Madai
ya maboresho ya mfumo wa uchaguzi sio ya wanasiasa pekee na hayakuanza leo. Madai
haya yalianza toka mwaka 1992, lakini hadi leo maboresho yaliyofanyika ni machache
sana. Ili kufanikiwa katika Muafaka huu ni vyema makundi yote ya kijamii yakawa
sehemu ya mchakato huu kwa lengo la kufanyia kazi madai haya kabla ya kwenda kwa
uchaguzi.
b) Muda wa Muafaka
Mchakato wa Muafaka uanze mapema iwezekanavyo ili kutoa nafasi ya vyama vya siasa
na watanzania kuelekeza nguvu katika kujiadnaa na uchaguzi na sio kama ilivyo sasa
ambavyo muda mwingi unatumika kudai maboresho ya mfumo wa uchaguzi.
c) Hoja za Msingi wakati wa Mchakato wa Muafaka
Pamoja na kwamba washirika wa Muafaka watakuja na hoja zao zingine , tunapendekeza
msingi wa muafaka uwe ni kwenye mambo ambayo yamekuwa yakijotokeza katika
uchaguzi na kuathiri mchakato wa mzima wa uchaguzi. Tunafahamu kabisa kuwa msingi
wa changamoto za uchaguzi hapa nchini upo katika katiba na sheria zingine, lakini
kutokana na muda uliosalia katika kuelekea kwenye uchaguzi tunadhani yapo mambo
yanaweza fanyika kwa muda huu uliobaki endapo tutakwenda kwa njia hii ya muafaka wa
Kitaifa. Mambo mengine kama upatikanaji wa katiba mpya yanaweza kuwekwa kama
mambo yatakayofanyiwa kazi baada ya uchaguzi.
Maboresho na mambo ambayo yanaweza fanyiwa kazi yanaweza kuwa mengine ni ya
kisheria, kikanuni na mengine mengi ni ya kimtazamo na kiutendaji. Tunatambua kabisa
kuwa changamoto nyingi pia za kiuchaguzi zinachangiwa na aina ya wasimamizi, matendo
na mitizamo ya viongozi wakati wa uchaguzi. Changamoto hizi haziitaji mabadiliko yoyote
ya kanuni wala sheria bali msukumo wa pamoja kama Taifa kuondokakana na mambo
haya. Mfano matendo kama ya wasimamizi kukimbia wakati kurisha formu, kusumbua
mawakala wa vyama vya siasa, kuengua wagombea , matumizi ya vyombo vya dola
kusumbua vyama vya upinzani ni mambo ambayo yanaweza kudhibitwa kupitia Muafawa
wa Kitaifa Kuelekea Uchaguzi.
Tunapenda kuainisha masuala 10 ambayo yanahitaji kufanyiwa marekebisho au kuwekwa
saw ana kudhibitwa kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka 2025
unakuwa wa huru na wa haki.
i) Wasimamizi wa uchaguzi wasiwe watumishi wa Serikali Pekee
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inapaswa kuajiri watumishi wake na sio kutegemea
watumishi wa serikali pekee. Viongozi na Watumishi wa serikali ambao wanateuliwa
kusimamia uchaguzi sio watu huru, wenye maslahi na pia ni wengine wateule wa Rais
ambaye naye ni mgombea kwenye uchaguzi husika. Hoja hii ni ya muhimu sana na
uwezekano wa kufanyia kazi kabla uchaguzi ni mkubwa kama tutakuwa na Muafaka
wa Kitaifa.
ii) Tabia za maafisa wa uchaguzi kufunga ofisi hasa wagombea wa uchaguzi
wanaporusisha fomu wakati wa uchaguzi.
Kwa muda mrefu wasimamizi wa uchaguzi katika vituo wamekuwa na tabia ya kufunga
ofisi hasa wanaposikia kuwa wagombea wa upinzani wanataka kurudisha fomu za
uteuzi wa kuwa wagombea. Suala hili halihitaji mabadilikoya sheria bali ni kuwa na
Muafaka wa Kitaifa ambao suala hili litakuwa ni moja ya marufuku kuelekea uchaguzi
ujao.
iii) Wagombea kutoka vyama vya upinzani kuenguliwa.
Katika uchaguzi wa mwaka 2019, 2020 na 2024 wagombea kutoka vyama vya
upinzani wamekuwa wakienguliwa kwasababu mbalimbali ambazo hazina msingi
wala mashiko kama vile kutojua kusoma na kuandika, kukosea majina yao na
vyama vyao. Sisi tunaamini kwamba makosa katika kujaza fomu za uteuzi wa
wagombea hayapaswi kuwa ni hukumu ya kuwaengua wagombea ila wagombea
wanapaswa kupewa nafasi ya kurekebisha makosa hayo. Suala hili pia halihitaji
mabadiliko ya sheria kwa bali iwe ni mojawapo ya marufuku yatakayotokana na
Muafaka wa Kitaifa.
iv) Suala la mawakal kutoapishwa au kuondolewa kwenye vituo vya kupigia kura
Katika chaguzi zilizopita mawakala kutoka vyama vya upinzani wamekuwa
wakiondolewa kwenye vituo vya kupigia kura kwa nguvu. Takwa la mawakala
kuapishwa wakati wanasimamia uchaguzi ambalo ni zoezi la wazi halipaswi kuwa
kigezo kwani mawakala wengi wa upinzani wamezuiliwa kuingia vituo vya kupigia
kura kwa madai ya kwamba hawajaapishwa. Hii imepelekea mawakala wa vyama
vya upinzan kunyimwa barua za utambulisho au kukataa kuwaapisha au
kuwaapisha wakati tayari zoezi la uchaguzi linaendelea. Swala hili linaweza
jadiliwa kwa pamoja kama Taifa na kulipatia ufumbuzi kabla ya kwenda kwenye
uchaguzi.
v) Makosa ya kiuchaguzi kutambulika kama makosa ya jinai.
Wakati wa uchaguzi kumeibuka tabia ya kutumia makosa ya jinai kutia hofu
wanasiasa na wapiga kura. Vitendo vya kugeuza makosa ya uchaguzi na kuyafanya
kuwa makosa ya jinai yanaweza pia zungumzika bila kwenda kwenye maboresho
ya sheria. Uchaguzi haupaswi kuwa na makosa ya jinai.
vi) Vyombo vya habari na waangalizi uchaguzi kuzuiliwa kutoa taarifa
zinazohusiana na mapungufu ya uchaguzi siku au wakati wa uchaguzi.
Katika chaguzi zetu pamekuwa na udhibiti wa vyombo vya habari kurusha taarifa
ambazo zinaonyesha mapungufu katika zoezi la uchaguzi. Pia asasi za kiraia za
ndani zinazopewa kibali cha kutazama uchaguzi zimezuiwa kabisa kutoa maoni yao
wakati wote wa uchaguzi na badaye kutakiwa kuwasilisha taairifa ya uangalizi kwa
Tume ya uchaguzi ili kupata ruhusa ya kuitoa kwa umma.
vii) Matumizi ya nguvu kutoka kwa vyombo vya dola wakati wa uchaguzi.
Kumekuwepo na tuhuma ya vyombo vya dola hasa vyombo vya usalama kutumika
vibaya dhidi ya wapinzani wakati wa uchaguzi. Mara kadhaa wakati wa uchaguzi
wanasaia wa upinzani wamekuwa wakikamatwa , mikutano yao ikiingiliwa na wengine
kubambikiwa kesi mbalimbali na wakati mwingine wengine kupoteza maisha. Suala
hili linafanya mchakato wa uchaguzi usiwe na utulivu na kutia hofu kwa watanzania na
kuchangia kujitokeza kwa idadi ndogo ya wapiga kura.
Kwa mfano katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 katika jimbo la Hai, askari Polisi
alimwambia wazi mgombea wa upinzani kwamba hatashinda uchaguzi huo wa jimbo
la Hai. Askari huyo hakuwahi kuchukuliwa hatua zozote hadi hivi leo. Mfano hai
mwingine ni kukamatwa kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Mhe. Tundu Lissu
wakati akihutubia mkutano wa hadhara Aprili 09, 2025 huko Mbinga na kusafirishwa
hadi Dar es Salaam na kufunguliwa kesi ya Uhaini. Vilevile mikutano ya hadhara
Songea iliyokuwa inaendelea ya CHADEMA kuzuiliwa na Jeshi la Polisi pasipo sababu
za msingi na za kisheria.
viii) Mapungufu mengi ya Sheria na Kanuni za uchaguzi.
Kwa mfano sheria hazitoi ulazima wa wakala au mgombea kuwepo eneo la
kuhesabia kura na kutokuwepo kwake hakuwezi kubatilisha chochote
kinachohusiana na matokeo ya uchaguzi. Mapungufu haya ya Sheria na Kanuni
yametumika vibaya hasa dhidi ya wapinzani ambapo mawakala wamekuwa
wakiondolewa kwa nguvu katika vituo vya kupigia au kuhesabia kura. Katika vituo
vya kupigia kura vilivyopo kwenye magereza, mawakala wa vyama na waangalizi
au watazamaji wa uchaguzi hawaruhusiwi kuingia kwenye vituo hivyo vya kupigia
kura. Katika vituo hivi mawakala, waangalizi na watazamaji wa uchaguzi
wanapaswa kuruhusiwa kuingia katika vituo hivyo. Muafaka wa kitaifa unaweza
jadili swala hili na kuanisha mambo ambayo yanaweza fanyiwa kazi kwa sasa na
yale ambayo yatafaniwa kazi baaada ya uchaguzi kama vile kupatikana kwa Katiba
mpya.
ix) Uwazi katika Mchakato wa Kuandikisha Wapiga Kura na Manunuzi ya Vifaa
vya Uchaguzi
Pia eneo hili limekuwa likilalamikiwa katika chaguzi zote na tunadhani inaweza
kuwa sehmu ya muafaka kuelekea uchaguzi mkuu ujao. Watanznia waachwe wawe
huru katika kuhoji na kudai taairfa za msingi kuhusu uchaguzi.
x) Suala usalama wa Kura na Utoaji wa Matokeo
Mara kwa mara kumekuwepo na malalamiko wakati wa uchaguzi kuhusu uwepo
wa kura feki , usalama wa kura na pia mchakato wa usambazaji wa matokeo kutoka
vituo kwenda maeneo ya majumuisho kutiliwa shaka. Mambo yote haya yanaweza
kufanyiwa kazi kwa pamoja kama sote tutakuwa na nia ya kuwa na uchaguzi huru
na haki.
3. Hitimisho
a) Tunashauri sana wadau wote wa uchaguzi , viongozi wa kisiasa, wananchi,
viongozi wa dini, wagombea na wasimamizi wa uchaguzi kuona umuhimu wa
kutafuta muafaka wa kitaifa kwa lengo la kuandaaa mazingira tulivu, huru na yenye
haki kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
b) Ni ukweli usiopingika kuwa hoja zilizotajwa hapo juu ndio zimekuwa kilio wakati
wote wa uchaguzi na sio busara kuelekea katika uchaguzi ujao bila kukaa chini
kama Taifa na kuzifanyia kazi.
c) Tunalishauri Taifa na viongozi wote wa nchi, vyama vya siasa, viongozi wa dini na
wananchi kuona umuhimu wa kuweka tofauti zetu pembeni na kuwa na Muafaka
wa Kitaifa kabla ya kuelekea kwenye uchaguzi ujao.
d) Ili kuweza kufikia hatua ya kuwa na Muafaka wa Kitaifa , tunashauri pia mashtaka
yanayomkabili Mkwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu yaondolewe kwa
mujibu wa sheria chini ya ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ili kupisha utekelezaji
wa mchakato huu wa Muafaka wa Kitaifa tunaoupendekeza. Mashtaka haya ni
makubwa na yanakwenda kuweka dosari kubwa katika uchaguzi wa mwaka huu
endapo ataendelea kushikiliwa kwa mashtaka haya ya uhaini. Sisi tunadhani bado
kuna nafasi ya kufanya marekebisho ya hati mashtaka haya yanayomhusu Tundu
Lisu na kuondoka kosa hili uhaini katika hati yake ya mashtaka ilia pate dhamana
na kurejea katika shughuli zake za kisasa na pia kushiriki mchakato huu wa
Muafaka wa Kitaifa tunaopendekeza.
e) Tunashauri wanasiasa wote nchini wakati huu wa kuelekea uchaguzi wajitahidi
sana kuchuja aina za matamshi wanayotoa wakati mwingine bila kujua madhara
yake au kwa nia nzuri lakini hupelekea kujiweka katika mazigira ya hatarishi zaidi.
f) Vyombo vya dola viepuke kwa namna yoyote ile kutumia mamlaka yao vibaya kwa
kuingilia uhuru wa vyama vya siasa kufanya siasa hapa nchini.
g) Kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi ni vyema kutambua kuwa haki ya kujieleza
inapaswa kulindwa kwa kila namna kwa kuwa ndio nyenzo muhimu wakati huu wa
uchaguzi. Serikali , taasisi za umma , wananchi na wanasisa mnapaswa kuwa na
uvimulivu na ustahimilivu wa maneno mengi ya kisiasa yanayotolewa wakati huu
wa uchaguzi.
h) Bado tunaamini kabisa maboresho ya msingi yanaweza kufanyika kwa kipindi
kilichobaki lakini inahitaji utashi wa kila kundi kuhakikisha hili linawezekana.
Maboresho mengine makubwa kama upatikanaji wa Katiba Mpya yanaweza kuwa
sehemu ya makubaliano ya muafaka kuwa yafanyike mara baada ya kumaliza
uchaguzi. Lakini kila kitu kiwe kimewekwa sawa katika Muafaka tunaopendekeza.
i) Tujenge utamaduni ya kukubali majadiliano na maridhiano wakati wote kama
Taifa, makundi yote yanayovutana katika jamii kuelekea uchaguzi hayana budi
kutumia busara na hekima na kukubali kujishusha na kutoa nafasi ya kuwa na meza
ya majadiliano. Tusiende kwenye majadiliano tukiwa na majawabu ya asilimia mia
moja bali tuwe tayari kupoteza na kupata na kuweka mbele uzalendo na utaifa.
j) Tunawasihi sana Wazee na Viongozi wastaafu wa Taifa wavunje ukimwa na
watumie busara na uzoefu wao kulishauri Taifa kukubali kuenenda katika
mazingiria ambayo kila Mtanzania ataona kuwa anatendewa haki katika Taifa lake.
k) Tuache kudhani na kuchukulia suala la uchaguzi kama ni jambo la wanasiasa pekee,
suala la uchaguzi linamgusa kila Mtanzania aliye hai leo na atakayezaliwa kesho.
Sote tunapaswa kuguswa pale tunapoona kuna mazingira yanapelekea kuvunja haki
za kiuchaguzi , kuvunja amani na utulivu hapa nchini. Kila mtu atumie nafasi yake
kuhakikisha tunatanguliza maslahi ya Taifa zaidi katika uchaguzi ikiwa ni pamoja
na kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki,huru na wa amani.
l) Falsafa ya 4R ni wakati wake huu sasa kutumika ipasavyo ili kuhakikisha
tunakwenda katika uchaguzi tukiwa na umoja , uhuru , haki na
mshikamano.Tunamsihi sana na kumshauri Rais Samia kuona umuhimu na ulazima
wa kusaidia kufanyika kwa mchakato huu wa kupata muafaka wa Kitaifa Kuelekea
Uchaguzi kwa tunaamini hata yeye anaamini katika mazungumzo an majadiliano.
Onesmo Olengurumwa (Wakili)
Mratibu wa Kitaifa - Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania
Aprili 11, 2025 Dar es Salaam, Tanzania.
0 Comments