Header Ads Widget

RAIS SAMIA AZINDUA DARAJA LA JPM KIGONGO- BUSISI

 



NA CHAUSIKU SAID, MATUKIO DAIMA MWANZA 


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Daraja la JPM Kigongo-Busisi na kuwataka vijana waliotumika katika ujenzi wa daraja hilo kutumia ujuzi walioupata kuchangia ujenzi wa madaraja mengine nchini.


Akizungumza leo Juni 19, 2025 katika hafla ya uzinduzi wa daraja hilo lenye urefu wa kilomita 3 na upana wa mita 6, Dk. Samia amesema ujenzi huo umegharimu shilingi bilioni 718, huku asilimia 90 ya wafanyakazi wake wakiwa vijana wa Kitanzania. Amesema mafanikio haya ni hatua muhimu katika kuongeza nguvu kazi ya kitaifa yenye ujuzi wa ujenzi wa miundombinu mikubwa.


"Daraja hili limejengwa kwa lengo la kuunganisha barabara ya Usagara na Sengerema, na litakuwa kichocheo muhimu cha uchumi kupitia fursa mbalimbali za maziwa makuu," alisema Dk. Samia.


Rais Samia alieleza kuwa wazo la ujenzi wa daraja hilo lilianzia kwa mtangulizi wake, Hayati John Pombe Magufuli, aliyekuwa na dhamira ya kufungua fursa za kiuchumi kwa wakazi wa maeneo hayo na taifa kwa ujumla. Alisisitiza kuwa ahadi yake tangu alipoingia madarakani ilikuwa ni kukamilisha miradi yote ya kimkakati iliyoanzishwa na mtangulizi wake.


"Nilipokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wangu wakati daraja likiwa limekamilika kwa asilimia 25 tu, lakini niliapa kuhakikisha miradi yote ya kimkakati, ikiwemo SGR, Bwawa la Mwalimu Nyerere na daraja hili, inakamilika kwa maslahi ya Watanzania," alisema Rais Samia.


Akitoa historia fupi ya mradi huo, Rais Samia alieleza kuwa tangu mwaka 1971, serikali ilikuwa ikitegemea huduma ya vivuko vilivyonunuliwa kwa ajili ya kusafirisha watu na mizigo katika eneo hilo, lakini kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya usafiri, serikali iliamua kujenga daraja hilo la kudumu ili kuboresha huduma za usafirishaji na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.


Mwisho.









Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI