Header Ads Widget

KWANINI ZELENSKY HAWEZI KUIACHIA URUSI ENEO HILI?

 


Hapo awali Vladimir Putin alikanusha kuhusika kwa njia yoyote katika unyakuzi wa eneo la Crimea mnamo Februari 2014, wakati makomando waliovalia sare za kijani kibichi walipoliteka bunge la eneo hilo na kutawala rasi hiyo.

Hatua ya "wanajeshi hao" iliashiria mwanzo wa vita vya Urusi dhidi ya Ukraine, ambavyo viliishia katika uvamizi kamili wa 2022.

Mustakabali wa Crimea sasa uko katikati ya mpango wa amani wa Rais Donald Trump na umemfanya Volodymyr Zelensky wa Ukraine kukataa kutambua udhibiti wa Urusi katika rasi hiyo.

Masharti kamili ya mpango wake hayajachapishwa, lakini ripoti zinaonyesha kuwa itajumuisha Marekani kutambua Crimea kama sehemu ya kisheria ya Urusi - de jure kwa Kilatini.

Kwa mujibu wa Trump, rasi ya kusini ya Ukraine "ilipotea miaka iliyopita" na "sio sehemu ya majadiliano" katika mazungumzo ya hivi punde kutafuta ya amani.

Lakini kwa Zelensky kuachana na Crimea kama sehemu isiyoweza kugawanyika ya Ukraine itakuwa ni kutojali.

Kwa maneno ya mbunge wa upinzani Iryna Gerashchenko "uadilifu wa eneo na uhuru ni mstari mwekundu kwa Ukraine na raia wake".

Trump alitoa hoja kwamba "ikiwa [Volodymyr Zelensky] anataka Crimea, kwa nini hawakuipigania miaka 11 iliponyakuliwa na Urusi?"

Risasi chache zilifyatuliwa, lakini Crimea ilitekwa kwa mtutu wa bunduki wakati kulikuwa na umbwe wa kiutawala.

Baadaye Putin alikiri kunyakua ardhi hiyo katika mkutano wa usiku kucha na maafisa wake siku chache baada ya kiongozi wa Ukraine aliyedaiwa kuungwa mkono Urusi kuondolewa madarakani mjini Kyiv.

Wanajeshi wasiojulikana walisemekana kuuteka mji wa Crimea lakini baadaye ilibainika wazi walikuwa Warusi

Crimea ni kizingiti kwa Trump

Kwa kiongozi wa Marekani ambaye yuko mbioni kufikia mkataba wa amani, Crimea huenda ikawa kizingiti.

Trump hajakosea akisema kuna uwezekano mdogo wa Ukraine kuikomboa Crimea siku za usoni, na huo ndio ukweli wa mambo - hili ni eneo ambalo limekuwa chini ya utawaliwa wa Urusi kiuhalisia. Lakini hatua hiyo bado haijatambuliwa rasmi kisheria.

Zelensky anaashiria "tamko la Crimea" la 2018 la waziri wa mambo ya nje wa wakati huo wa Trump, Mike Pompeo.

Pompeo alisema Marekani inapinga "jaribio la Urusi kunyakua Crimea" na kuahidi kuendelea na mikakati ya kuhakikisha Ukraine inarejeshewa eneo lake.

Zelensky anachomaanisha ni kwamba Trump aliunga mkono msimamo wa Ukraine kuhusu eneo la Crimea wakati huo, na inapaswa kuzingatia hilo wakati huu.

Ikiwa unyakuzi wa ardhi ambao haujatambuliwa na jumuiya ya kimataifa utaidhinishwa na Marekani kuwa halali, hiyo itamaanisha nini kwa sheria za kimataifa na kanuni za mkataba wa Umoja wa Mataifa?

Wiki chache baada ya vita vikali vya Urusi kuanza, kulikuwa na pendekezo la awali huko Istanbul la kuweka kando suala hilo ili Urusi na Ukraine ziweze kulisuluhisha katika miaka 10-15 ijayo.

Mpango huo haukufanyika na sasa inaiona ilikuwa ni njia ya kuepuka kikwazo hicho.

Zelensky amebanwa na katiba ya Ukraine

Trump na Makamu wa Rais JD Vance wameonekana kuvurugwa na misimamo ya Zelensky

Zelensky alisisitiza kwamba hana uwezo wa kuachana na Crimea: "Hili halina mjadala. Hii ni kinyume na katiba yetu."

Kifungu cha 2 cha katiba kinasema kwamba uhuru wa Ukraine "unajumuisha eneo lake lote" ambalo "ndani ya mpaka wake wa sasa haugawanyiki na hauwezi kukiukwa".

Mabadiliko yoyote katika eneo la Ukraine lazima yafanyike kupitia kura ya maoni ya kitaifa, ambayo lazima iidhinishwe na bunge la Ukraine.

Sio tu Rais Trump ambaye ana shida na Kyiv. Urusi pia inaiona katiba ya Ukraine kama "kizuizi" kwa juhudi za amani.

Katiba inaweza kubadilishwa, lakini sio wakati huu ambapo Ukraine inaendeshwa chini ya sheria za kijeshi.

Je, Urusi ina haki ya dhidi ya Crimea?

Rais wa Urusi Vladimir Putin

Kwa sababu za kihistoria, Warusi kwa muda mrefu wanalichukulia Crimea kama sehemu ya eneo lao na Putin amezungumzia hilo akisifia "uhusiano ambao hauwezi kuvunjika" akiongeza kwamba rasi hiyo, pamoja na hoteli zake katika ufuo wa Bahari Nyeusi ni eneo tulivu.

Lakini Crimea pamoja na maeneo mengine ya Ukraine zilipiga kura ya uhuru kutoka kwa Muungano wa Kisovieti uliovunhika mwaka 1991. Ilikuwa na hadhi ya jamhuri inayojiendesha ndani na Kyiv iliruhusu Urusi kukodisha bandari ya Sevastopol kama sehemu ya Meli zinazotumia Bahari Nyeusi kutia nanga.

Baada ya kunyakua eneo hilo mwaka 2014 Putin alitaka kuimarisha udhibiti wa Urusi dhidi ya Crimea, kwanza kwa kujenga daraja la maili 12 kwenye Mlango-Bahari wa Kerch mnamo 2018 na baadaye kuliteka daraja la ardhini kando ya Bahari ya Azov mnamo 2022.

Putin alihisi kuwa anasahihisha makosa ambayo Urusi ilitendewa wakati kiongozi wa Usovieti Nikita Khrushchev alipoihamisha Crimea hadi Ukraine mwaka 1954. Urusi, alisema, "haikuibiwa tu, bali iliporwa".

Crimea ilinyakuliwa kwa mara ya kwanza na na Urusi chini ya theCatherine the Great mnamo 1783 na kwa kiwango kikubwa ilisalia kwa sehemu ya Urusi hadi uamuzi wa Khrushchev.

Urusi na Ukraine wakati huo zilikuwa jamhuri za Muungano wa Kisovieti kwa hivyo halikuwa jambo kubwa kwa Kremlin mnamo 1954.

Zaidi ya nusu ya wakaazi wa Crimea walikuwa Warusi, kwa sababu idadi kubwa ya watu wa jamii ya Tatars katika eneo la Crimea walifukuzwa chini ya kiongozi wa kiimla wa Soviet Joseph Stalin mnamo 1944.

Jamii ya Tatars ilifanikiwa kurejea Crimea kutoka uhamishoni mnamo mwaka 1989 wakati Umoja wa Kisovieti uliposambaratika, na sasa wanakadiria takriban 15% ya wakaazi wa Crimea.

Urusi ilipanga kura ya maoni Machi 2014 lakini hatua hiyo ililaaniwa vikali na jumuiya ya kimataifa na hatimaye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likapitisha azimio linalounga mkono uhuru wa Ukraine.

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu iliamua kwamba shughuli za Urusi katika Crimea ni sawa na "unyakuzi".

Refat Chubarov, Mwenyekiti wa Mejlis, chombo kinachowakilisha jamii ya Watatars wa Crimea, amesisitiza kuwa Ukraine ina wajibu wa kupinga mkataba wowote unaojumuisha kuachia eneo lake kama sehemu ya kufikia amani.

"Crimea ni makaazi asilia ya Watatar wa Crimea na ni sehemu muhimu ya Ukraine," alisema.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI