Header Ads Widget

MAREKANI KUMKAMATA TRAORÉ? KWA NINI MICHAEL LANGLEY ANA WASIWASI?

 


Katika hali isiyo ya kawaida, jina la Kapteni Ibrahim Traoré, kiongozi kijana wa Burkina Faso anayejitambulisha kama mpigania haki za Waafrika, limeingia katika vichwa vya habari vya dunia si kwa mapinduzi aliyoyafanya tu, bali kwa kile kinachotajwa kuwa ni shinikizo kutoka kwa Marekani kutaka akamatwe.

Tuhuma hizi hazijatolewa na mtu wa kawaida, bali ni kutoka kwa Jenerali wa nyota nne wa Marekani, Michael E. Langley, ambaye ni Kamanda wa Kikosi cha Marekani cha Afrika kinachoitwa United States Africa Command (AFRICOM).

Katika kikao rasmi cha Baraza la Seneti la Marekani wiki hii, Langley aliitwa kutoa tathmini kuhusu hali ya usalama barani Afrika. Katika maelezo yake, alimtaja wazi Kapteni Traoré, akisema kwamba anatumia dhahabu ya taifa lake "kujilinda binafsi" badala ya kuwalinda wananchi, na akaongeza kuwa kuna haja ya kumchukulia hatua kali za kimataifa, akisema:

"Tunapendekeza hatua mahususi, vikwazo vya kifedha, ushirikiano wa kimataifa, na ikiwa itahitajika, Traoré azuiliwe ili kulinda maslahi ya kikanda na kimataifa."

Kauli hiyo imetafsiriwa na wengi kuwa ni wito wa wazi wa kumkamata kiongozi huyo. Lakini je, kweli Traoré ni tishio kwa usalama wa dunia, au ni kiongozi asiyejiweka chini ya amri ya mataifa ya Magharibi?

Michael Langley: Jenerali wa hadhi ya nyota nne Marekani



Jenerali Michael E. Langley aliteuliwa mwezi Juni 2022 kushika wadhifa wa Kamanda wa AFRICOM, uteuzi uliothibitishwa na Baraza la Seneti mnamo Agosti 6, 2022. Kwa uteuzi huo, Langley aliingia kwenye historia kama Mmarekani Mweusi wa kwanza kufikia hadhi ya Jenerali wa nyota nne (Four-Star General) katika Jeshi la Wanamaji la Marekani, tangu kuanzishwa kwake miaka 246 iliyopita.

Cheo cha Jenerali wa nyota nne ni miongoni mwa vyeo vya juu kabisa katika safu ya kijeshi nchini Marekani. Kinampa mamlaka ya kutoa maamuzi ya kimkakati kuhusu operesheni za kijeshi duniani, hasa katika bara la Afrika ambako AFRICOM inaendesha shughuli za kijeshi na za ujasusi katika zaidi ya nchi 50.

Licha ya hadhi hiyo, Langley sasa anakabiliwa na maswali ya kiitikadi, hasa miongoni mwa Waafrika wanaomwona kama msaliti wa asili yake, anayesimamia maslahi ya kibeberu dhidi ya mustakabali wa bara lake la asili.

Alivyotamka Traoré azuiliwe, kupitia mitandao ya kijamii wengi wa waafrika wamemjia juu.

"Hii ni huzuni, ikizingatiwa kwamba kijana huyu amekuwa akifanya kazi kwa bidii sana na kufanya mengi kwa ajili ya raia wa Burkinafaso', anaandika Mtanzania Shirad21 kwenye mtandao wa instagram.

Na wengi waliandika "Langley umesahau asilia yako, tuachie Afrika yetu".

Licha ya kuwa mweusi kwa asili, Langley anachukuliwa na wengi kama sehemu ya mfumo wa kisasa wa ubeberu unaolenga kudumisha ushawishi wa Magharibi barani Afrika. Wachambuzi wa kisiasa, kama vile Dkt. Sékou Touré kutoka Chuo Kikuu cha Dakar, aliyehojiwa na gazeti la Le Quotidien la Senegal, anasema kwamba "Langley, kwa nafasi yake, ni sehemu ya mfumo wa kijeshi wa Marekani unaolinda maslahi ya kibeberu katika Afrika, huku akizingatia maslahi ya Marekani badala ya maslahi ya wananchi wa Afrika."

Hii ni hoja ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara kuhusu jinsi Marekani inavyotumia viongozi wa Kiafrika ili kulinda mifumo ya kiuchumi na kijeshi ya Magharibi.

Kwa nini Langley anataka Traoré akamatwe, ni kweli tishio?


Kapteni Ibrahim Traoré alichukua madaraka mwaka 2022 kwa mapinduzi ya kijeshi, akiahidi kusafisha mfumo wa kifisadi, kuleta usalama, na kurejesha rasilimali za taifa mikononi mwa wananchi wa Burkina Faso.

Moja ya hatua kubwa aliyochukua ilikuwa ni kufukuza vikosi vya Ufaransa na kusitisha ushirikiano wa kijeshi na mataifa ya Magharibi, hatua zilizowashangaza na kuwakera viongozi wa kimataifa ikiwemo Marekani.

Langley, katika Seneti, alieleza wasiwasi wake kwamba:

"Traoré anatumia mapato ya dhahabu kufadhili mamluki wa kigeni na kulinda utawala wake binafsi. Hii ni hatari kwa utulivu wa kikanda na inaleta mashaka kuhusu mahusiano ya kimataifa na makundi yanayopinga Marekani."

Kauli hiyo ilionekana kuashiria kuwa Marekani haioni tena uongozi wa Traoré kama halali au salama kwa maslahi yake barani Afrika, na hivyo inatafuta njia za kumwondoa au kumzuia kuendeleza ajenda yake ya kujitegemea.

Wachambuzi wengi wa masuala ya siasa na usalama wameibua hoja kwamba hatua ya Langley si kuhusu usalama wa kweli, bali ni hofu ya Marekani na mataifa ya Magharibi juu ya kuibuka kwa viongozi huru barani Afrika.

Dkt. Sékou Touré, mchambuzi wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dakar, aliyehojiwa na gazeti la Le Quotidien nchini Senegal, anasema: "Hili si suala la usalama, ni suala la udhibiti. Langley anajua fika kuwa dhahabu ya Burkina Faso imekuwa silaha ya kiuchumi kwa Traoré. Marekani inahofia mfano huu kuenea katika mataifa mengine ya Afrika."

Kauli hiyo inaungwa mkono na Dkt. Aminata Diallo, mtaalamu wa siasa za ukanda wa Sahel kutoka Chuo Kikuu cha Abidjan, aliyeliambia RFI kwamba: "Mmarekani mweusi anayeongoza juhudi za kuzuia Afrika huru, hilo ndilo tatizo kubwa. Hii ni sura mpya ya ukoloni wa kijeshi kupitia Waafrika waliopandikizwa kwenye mifumo ya kibeberu."

Nini mtazamo wa Traoré?


"Tutachimba dhahabu yetu sisi wenyewe sio kwa ajili ya Ufaransa, kwa ajili ya watu wetu", ilikuwa kauli maarufu ya Traoré alipoamua Ufaransa iondoke kwenye ardhi ya Burkina Faso.

Na kauli hii na hatua iliyochukuliwa imeonekana na wengi kama chanzo kuiibua Marekani na kina Langley kutaka akamatwe. Traoré ni mwanajeshi haogopi hilo amesema mara kadhaa atapambana kwa ajili ya watu wake jambo linalompa sifa kubwa Afrika.

"Asilimia 80 ya maisha yangu ni vita, tutajilinda nanyi mjilinde kwa faida yetu sote", anawaambia wananchi wake katika moja ya mikutano yake na kuongeza "Mapambano tunayopambana sio kwa ajili ya Burkina Faso, lakini kwa ajili ya Afrika nzima".

Kwa baadhi ya Waafrika, Traoré ni mfano wa kiongozi anayejitoa kwa ajili ya watu wake. Kwa wengine, hasa mashirika ya kimataifa yanayoegemea upande wa Magharibi, yeye ni tishio linalostahili kukabiliwa.

Katika mazingira ya sasa ambapo mataifa ya magharibi na Asia yamekitia mizizi Afrika, viongozi kama Traoré wanajitokeza kama nembo ya kizazi kipya cha Afrika kisichotaka tena kutegemea msaada wa kigeni au ulinzi wa mataifa ya nje. Wanasisitiza matumizi ya rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya ndani, ujasiri wa kidiplomasia, na ukombozi wa kiuchumi.

Lakini juhudi hizi zinakumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa mataifa yenye ushawishi kama Marekani, ambayo kupitia taasisi ya kijeshi Marekani kama AFRICOM, inayoongozwa na Langley yanajaribu kudhibiti siasa za bara hili kupitia usalama na misaada ya kijeshi. Inasubiriwa kuona kama Je, Marekani itamkamata kweli Traoré, baada ya kauli ya kiongozi mkubwa wa kijeshi Langley?


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI