Na Thobias Mwanakatwe,ITIGI
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Manyoni,Jumanne Makhanda,amewataka wananchi kuwapuuza watu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi kwa maslahi yao binafsi na kwamba Uchaguzi Mkuu mwaka huu utafanyika kama kawaida na utakuwa huru na wa kidemokrasia.
Amesema hayo leo (Aprili 25, 2025) kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi ambacho kilitanguliwa na kikao cha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa ajili ya kupitisha mabadiliko ya jimbo la Manyoni Magharibi ambalo limebadilika na sasa litaitwa Jimbo la Itigi.
"Wanaotaka kuvuruga amani ni kwa matakwa yao wenyewe lakini niwahakikishie uchaguzi mkuu mwaka huu utafanyika na utakuwa huru na wa kidemokrasia na kimsingi wanaotaka kuvuruga amani vyombo vya ulinzi na usalama vipo vitashughulika nao," amesema Makhanda.
Makhanda amewataka madiwani na watendaji wa Halmashauri hiyo kuendelea kuwaeleza wananchi miradi iliyotekelezwa na serikali ya CCM ili waendelee kuwa na imani ya CCM na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa CCM.
"Uchaguzi mwaka huu utakwenda vizuri sana kwasababu serikali ya CCM imetekeleza ilani vizuri sana kwa asilimia 99.99 kwa hiyo tutembee kifua mbele na CCM itapata ushindi wa kishindo," amesema Makhanda.
Aidha, Mwenyekiti huyo wa CCM Wilaya ya Manyoni amewapongeza watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ayoub Kambi kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakisimamia vizuri miradi ambayo serikali imetoa fedha kuitekeleza.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Itigi, Hussein Simba, amesema wakati tunaelekea kwenye uchaguzi madiwani wajipe moyo watashinda kwasababu ilani imetekelezwa vizuri.
Kwa upande wake Katibu wa Siasa na Uenezi Wilaya ya Manyoni, Charles Chimaisi,amesema wakati wa uchaguzi hakuna haja ya kuumizana kwasababu wote tunafahamiana ila wanaokuja hatuwafahamu.
Mwisho
0 Comments