Header Ads Widget

HALMSHAURI TUNDUMA YAPONGEZWA, CHONGOLO ASEMA “MMEFUTA HASIRA ZANGU”.

 



Na Moses Ng’wat, Tunduma

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, ameonyesha kuridhishwa kwake na hatua ya ujenzi wa bwalo la chakula katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Dkt. Samia SH, iliyopo Kata ya Namole, Halmashauri ya Mji Tunduma, Wilayani Momba, huku akisema kuwa “mmefuta hasira zangu” kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika.

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo ambao awali ulikuwa ukisuasua na kusababisha wasiwasi juu ya utekelezaji wake, Chongolo alisema amefurahishwa na hatua ya mradi ulipofikia kutokana na  usimamizi wake.

"Nikupongeze sana Mkuu wa Wilaya na uongozi wa Halmashauri. Leo mmefuta hasira zangu zote kwani nimeona na kufurahishwa na kazi nzuri ya usimamizi mliyoifanya katika mradi huu,” alisema Chongolo kwa msisitizo.



Aliongeza kuwa, “Mara ya mwisho nilipokuja hapa nilikataa hata kusaini kitabu cha wageni, lakini sasa nambo ni mazuri na mradi unaridhisha.”

Mradi wa ujenzi wa bwalo hilo, ambalo litagharimu takriban shilingi milioni 886 hadi kukamilika kwake.

Hata hivyo,  Chongolo ameagiza kuwa bwalo hilo lazima lianze kutumika ifikapo Aprili 25, mwaka huu na ameahidi kuwa siku hiyo atashiriki mlo wa pamoja na wanafunzi kama ishara ya kuunga mkono juhudi za utekelezaji bora wa mradi huo.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Tunduma, Mariamu Chaurembo, amesema Halmashauri imefanya mabadiliko ya bajeti na kutenga shilingi milioni 350 kwa ajili ya kukamilisha kazi zilizobaki.

“Bwalo hili linatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi milioni 886 hadi litakapokamilika, na tunaahidi kuwa tutakamilisha kazi kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili,” alisema Chaurembo.

Ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa ni sehemu ya muendelezo wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri zote za Mkoa wa Songwe, ikiwa ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana katika kila mradi.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI