Dawa mpya ya kutibu saratani ya matiti sasa imeanza kutumika nchini Uingereza.
Dawa hiyo kwa jina Capivasertib inasemekana haina madhara makubwa kwa wagonjwa kama zilivyo nyingine ambazo zina makali mno.
Ina tiba mahsusi inayolenga protini ya AKT, molekuli inayochochea ukuaji wa saratani.
Dawa hii hufanya kazi kwa kuzuia kabisa shughuli ya protini hiyo, hivyo kudhibiti ukuaji wa seli hatari.
Wanasayansi wamekuwa wakifanyia kazi dawa hii kwa zaidi ya miaka ishirini, na sasa wanaamini kuwa ndiyo yenye ufanisi mkubwa zaidi kuwahi kuonekana kwa wagonjwa walio na saratani ya hatua ya juu.
“Inatoa mbadala wenye ufanisi mkubwa, unaoweza kufanya kazi kwa muda mrefu — kwa miezi mingi, na kwa baadhi ya wagonjwa hata kwa miaka,” alisema Profesa Nick Turner, mtafiti mkuu na profesa wa onkolojia ya tiba katika Taasisi ya Utafiti wa Saratani na Hospitali ya Royal Marsden.
Majaribio ya dawa hiyo yanaonesha inapunguza uvimbe kwa karibu robo ya wanawake walio na saratani ya matiti na inaendelea kufanya kazi mwilini kwa muda mrefu wa hadi mwaka mmoja.
Saratani ya matiti ndiyo inayoripotiwa zaidi nchini Uingereza huku mwanamke mmoja kati ya saba kuathirika na saratani katika maisha yake, na asilimia 75 ya wagonjwa wakisalia hai kwa zaidi ya miaka kumi baada ya kugunduliwa.
Mafanikio katika matibabu yanaendelea kuleta matumaini mapya.
Iwapo saratani itarudi na kusambaa katika maeneo mengine ya mwili, lengo kuu la matibabu huwa ni kuidhibiti, kupunguza dalili, na kuboresha ubora wa maisha ya mgonjwa.
Matibabu yanayoweza kutolewa ni pamoja na tiba ya kufubaza makali ya saratani, matibabu kwa njia ya eksirei, na dawa maalum zinazozuia ukuaji wa saratani — kwa kuzuia homoni, kuimarisha kinga ya mwili, au kulenga moja kwa moja vichocheo vinavyosababisha ukuaji wa seli za saratani.
Dawa hii inafaa wagonjwa walio na mabadiliko fulani ya kinasaba yanayoathiri hadi nusu ya wale wanaougua saratani ya matiti katika awamu ya pili inayotegemea homoni — aina ya kawaida zaidi ambayo hukua kwa utegemezi wa homoni ya oestrogen.
Kwa upande wake, Profesa Peter Johnson, Mkurugenzi wa Huduma za Saratani katika NHS England, alisema kuwa dawa hiyo ni “chaguo la ziada” kwa wagonjwa ambao saratani yao imeendelea licha ya kupitia tiba ya homoni awali — japo si kila mtu atakayefaa kuitumia.
Bi Claire Rowney, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la hisani la Breast Cancer Now, alisema kuwa amefarijika sana kuona dawa hii ikiwapa wagonjwa “tumaini la muda wa ziada wa kuishi na kutekeleza mambo yanayowapasa zaidi katika maisha yao.”
0 Comments