Na Fadhili Abdallah, Kigoma
BENKI ya EXIM imetoa kiasi cha shilingi Milioni 52 kuunga mkono ujenzi wa shule mbili mpya za sekondarin katika wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma ikiwa ni kusaidia kukabili changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
Meneja masoko na mawasiliano wa Benki ya Exim, Stanley Kafu alisema kuwa benki hiyo imetoa kiasi cha shilingi milioni 52 kwa ujenzi wa madarasa mawili katika shule za Sekondari Kaphunya na Nyakatundu wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma sambamba na uwekaji wa madawati kwenye madarasa hayo ikitoa pia jezi seti mbili na mipira mitatu kwa kila shule.
Kafu alisema kuwa ujenzi wa madarasa hayo unatokana na maombi yaliyowasilishwa kwao na uongozi wa serikali wilaya ya Buhigwe hivyo kupitia mpango wa benki hiyo wa kurejesha kwa jamii (SCR) na hivyo kusaidia ujenzi huo na kwamba uboreshaji wa miundo mbinu ya elimu ina manufaa makubwa kwa wanafunzi kuongeza ufaulu na kupunguza utoro.
Akizungumza wakati akipokea shule hizo Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye alisema kuwa ujenzi wa shule mpya za sekondari na uboreshaji wa shule hizo unaofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau una mchango mkubwa katika kuondoa changamoto za mimba kwa wanafunzi wasichana na utoro kwa wanafunzi huku ufaulu ukiongezeka.
Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya Buhigwe, Michael Ngayarina alisema kuwa serikali itaendelea kuunga mkono nguvu za wananchi katika kuanzisha shule mpya za sekondari, kumalizia maboma ambayo hayajakamilika sambamba na kuboresha shule zilizopo kutokana na faida kubwa za shule hizo kwa jamii.
Mkuu huyo wa mkoa Kigoma katika hafla hiyo ameishukuru Benki ya Exim kwa mchango wake katika ujenzi wa shule hizo mbili sambamba na wadau wengine ambao wamekuwa wakisaidia miradi inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja kwa kurudisha kwa jamii faida wanayopata.
Mmoja wa wanafunzi waliohudhuria makabidhiano hayo,Abisa Pastor kutoka Shule ya Sekondari Kaphunya alisema kuwa kabla ya madarasa hayo walikuwa wanafunzi wa madarasa tofauti wakichanganywa na kusomea daresa moja hivyo uwepo wa darasa jipya utawafanya watenganishwe na taaluma itakuwa kubwa.
Mwisho.
0 Comments