Na. Edmund Salaho - Nyerere
Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania(TANAPA) leo Aprili 09, 2025 imemwagiza Mkandarasi anaejenga miundombinu ya Utalii katika Hifadhi ya Taifa Nyerere kuikamilisha kwa wakati miundombinu hiyo kama ambavyo makubaliano yaliyoingiwa kwenye Mkataba.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya miradi inayotekelezwa na Mradi wa REGROW ndani Hifadhi hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA Jenerali (Mstaafu) George Waitara alisema,
“Miradi ninayoiona hapa inakwenda naona kazi ni nzuri sana nitoe pongezi kwa Menejimenti ya Hifadhi ya Nyerere kwa usimamizi mzuri, nisisitize mkandarasi kumaliza kazi hii kwa wakati”.
Awali, akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya REGROW kwa Bodi ya Wadhamini, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Ephraim Mwangomo ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Nyerere
alibainisha kuwa kupitia uwanja mpya wa ndege ambao upo kwenye hatua za mwisho za ukamilishwaji wake Hifadhi ya Nyerere inategemea kupata wageni wengi kwani ndege kubwa na zile ndogo zitakuwa na uwezo wa kuleta wageni na hivyo kuongeza mapato ya Serikali kupitia Utalii.
“Serikali ya Awamu ya Sita kupita mradi wake wa REGROW imerahisisha kuboresha utendaji kazi wa Hifadhi, na nje ya maeneo ya Hifadhi kwa kugusa jamii zinazozunguka Hifadhi hapa kwetu tumepewa upendeleo kwani tumeweza kujenga Geti la Mtemere, Malazi ya wageni Mtemere yenye vyumba 20 vya kisasa, Uwanja wa Ndege wa kisasa, Sehemu ya kupumzikia wageni (Campsite) yenye uwezo wa kupokea wageni zaidi ya 100 kwa wakati mmoja, pamoja na Nyumba za kisasa za watumishi,” alisema Kamishna Mwangomo
Aidha, Kamishna Mwangomo alitoa wito kwa wawekezaji nchini kuchangamkia fursa za kuja kuwekeza katika Hifadhi ya Taifa Nyerere
“ Nitoe wito kwa wawekezaji, kuja kuwekeza katika huduma za malazi hapa Nyerere kwani miundombinu imeimarishwa sana hivyo swala la biashara ya malazi kwa watalii itakuwa ni biashara nzuri na ya uhakika ”.
0 Comments