Kuna mambo yanakera sana hasa yale yanayofanywa na wengi wa viongozi wa dini, siku hizi nao, bila haya wamejipa kazi ya upambe na uchawa wa wanasiasa.
Ukiwaangalia matendo yao, mahubiri yao na mienendo yao unaweza kusema nao ni wanasiasa, tena wanasiasa wasioiujua hata siasa yenyewe, bali ni upambe na uchawa ambao kwa Tanzania ya leo imekuwa kikwazo cha maendeleo.
Taasisi za dini hasa hii ya wavaa kanzu imezidi kuonesha ni jinsi gani inatumika kufanya kazi ya upambe na uchawa kwa "Mama."
Wengi wa viongozi wa dini na viongozi wanasiasa nchini wamekuwa kama watoto wa familia moja (ya siasa), ukiwasikiliza viongozi hao wa dini utagundua mahubiri yao yamelenga nini, matamshi yao, matendo yao na mienendo yao, bila shaka utaona haipishani kabisa na tabia, hotuba, matamshi, matendo na mienendo ya wanasiasa walio wengi hapa nchini, ambayo haiendeni kabisa na misingi ya taasisi zao.
Sasa hivi kumeibuka tabia au kasumba ya viongozi wa dini kujikusanya na kufanya maombezi ya kiongozi wa juu "Mama", na wakati mwingine wanatoa mpaka na vitisho kabisa kwa wale wanaomkosoa "Mama" kama ndiyo njia ya kumlinda "Mama" kisiasa.
Viongozi hao wanafanya hivyo ilihali wanajua vitendo hivyo havina tofauti na vile vinavyofanywa na (Wasanii), wapembe na ni kujidhalilisha mbele za - si mbele ya waumini na wananchi peke yake, bali pia mbele za Mwenyenzi Mungu muumba mbingu na nchi.
Haya ndiyo yanayofanya wananchi watamani orodha nyingine mpya ya mafisadi papa kama ile ya Dk. Slaa ya mwaka 2008.
Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema, "Watu walio hatari sana ni wale wanafikiri kuwa wanajua kila kitu, na wala hawana haja ya kujifunza zaidi. Hii ni tabia mbaya ambayo huzuia kabisa maendeleo.
Sababu moja ambayo ilizuia sisi waafrika kuendelea ni majibu rahisi kwa (kwenye) matatizo makubwa.
Majibu ya namna hiyo huzuia binadamu kupata sababu za kweli za matatizo yao." mwisho wa nukuu.
Hii maana yake ni nini? Viongozi wa dini wanafikiri kumsifia na kumuombea kiongozi wa juu "Mama" ndiyo njia sahihi ya kumsaidia, la sivyo wanajaribu kujipendekeza na kufanya upambe kwa minajiri yao binafsi hasa ya kimaslahi. Hawalisaidii taifa.
Taifa hili bado halijapata kiongozi mwenye kuutafsiri uongozi wa nchi uliowekwa kwenye kitabu kinachoitwa "Azimio la Arusha" ambacho kilikuwa ndiyo dira ya Tanzania.
Alipokuja Rais Dkt. John Magufuli Watanzania waliamini kuwa "huyu Magufuli" ndiye tuliyemtumaini kuifanya Tanzania kuwa taifa lenye nguvu kisiasa, kiuchumi na kijeshi, pamoja na jitihada za Magufuli za kujenga matumaini kwa wananchi na ambazo kimsingi hazikuwa na weledi au misingi endelevu, naye hakuweza kutimiza matarajio ya Watanzania.
Hivyo, Azimio la Arusha lilikuwa dira ya taifa kama ambavyo tu mataifa makubwa duniani kama China, Marekani, Dubai na kwingineko ambayo yalikuwa chini ya ukoloni wa Mwingereza kama sisi Tanzania, kisha yakaamua kujikomboa kwa kuja na misingi or Dira ya maendeleo ya mataifa yao: yaliweza kufika yalipo sasa kutokana na viongozi wenye maono, dhamira na mbinu za kuvusha wananchi kiuchumi.
Azimio la Arusha liliundwa na wanachama pamoja na viongozi wa TANU, lakini bahati mbaya kwamba hata wao akina 'Nyerere' hawakuwa tayari kulitekeleza azimio hilo kutokana na ukweli kwamba hawakuwa na uwezo wa kulitekeleza.
Ili Azimio la Arusha liweze kutekelezwa lilihitaji kiongozi mwenye maono, dhamira na nguvu za kulitekeleza azimio hilo.
Moja ya silaha ambayo ingetumika kulitafsiri Azimio la Arusha kwa vitendo ni kutengeneza wasomi wa fani mbalimbali zikiwemo za kisayansi kama walivyofanya viongozi wa China na mataifa mengine yenye maono.
Wasomi hawa wangeifanya Tanzania kuwa na uchumi imara kwa sababu kuoitia fani zao wangezalisha shughuli za kiuchumi ambazo zingewaajiri watanzania hata wale wasio wasomi.
Pili, Jeshi letu lingekuwa imara na huru badala ya kuwa chini ya Mwingereza au mmarekani.
Huwezi kujitegemea kwa vyovyote vile kama huna wataalamu wa nyanja mbalimbali muhimu za kiuchumi na kijeshi.
Kutokana na ukweli kwamba nchi yetu haina wasomi wataalamu katika nyanja hizo muhimu kama walivyofanya china, imelifanya taifa letu kuwa dhaifu kisiasa, kiuchumi, kitamaduni na kijeshi kiasi kwamba hatuna uwezo wa kuyapinga mataifa yenye nguvu pale yanapotaka kupora rasilimali za nchi yetu.
Mikataba mibovu inayofanywa na watawala wetu ni kielelezo cha haya ninayoyasema, tangu utawala wa awamu ya kwanza, dhamiri ya viongozi wetu ilifinyangwa na vitisho vya mataifa makubwa yenye nguvu kama Marekani na Uingereza kupitia taasisi zao kama Benk ya dunia na Shirika la fedha duniani, nk.
Wengi wa viongozi wa dini na wanasiasa wetu nchini pengine hili hawalijui na ni kutokana na ujinga wao au hofu yao ya kuingia matatani na mabeberu wetu, na ndiyo maana deni la taifa halijawahi kupungua zaid ya kuwa linapanda kila kunapoitwa leo.
Tunajua, unapokwenda kukopa kwa mtu au kwenye taasisi yoyote ya kifedha utalazimika kuweka dhamana, dhamana ya kitu kisichohamishika, kwa maneno mengine viongozi wetu wanapokopa wanaiweka rehani nchi (ardhi pamoja na rasilimali zake) yetu, miongoni mwa rasilimali ni pamoja na raia wa nchi husika.
Unapokuwa na mkopo maana yake nusu, kama si robo tatu ya mali zako zisizohamishika, ni mali ya aliyekukopesha mpaka pale utakapomaliza deni lako; na mkopo wowote huwa na mashariti na faida anazozipata anayekukoposha, na kwa nchi inaweza kuwa ni kuchimba madini, kusomba wanyama au misitu, kuwatoza kodi kubwa raia au kuwauzia bidhaa fulani kwa lazima nk.
Kutokana na ujinga wa viongozi wa dini na wanasiasa walio wengi, wamefanya maisha yetu kuwa uwanja wa mapambano yanayoendelea ya wale wanaotaka kuulinda ubinadamu wetu dhidi ya wale wanaotaka kuuteketeza, wale wanaotaka kujenga misingi imara kupitia "rasmu ya Jaji Warioba" (Katiba ya Wananchi) inayolinda maisha yetu na uhai wa taifa letu dhidi ya wale wanaotaka kuikwamisha misingi hiyo, wale wanaotaka kuyafungua macho yetu ili tuone mwanga na kuikaribisha kesho dhidi ya wale (kina Wasira na Makalla) wanaotushawishi tuyafunge macho yetu tusiione kesho (nchi ya ahadi/neema).
Sote tunakumbuka kwamba licha ya kejeli zote alizorushiwa Dk. Slaa baada ya kuitangaza hadharani orodha ya mafisadi papa, wapo watuhumiwa wa ufisadi huo walifikishwa mahakamani wakiwemo wale waliomtishia mwanzoni kumshitaki.
Mafisadi papa hao, Lowasa na Rostam walilazimika kujiuzulu, Lowassa alijiuzulu uwaziri mkuu, na Rostam alijiuzulu nyadhifa zote za CCM na hata ubunge.
Ni katika ripoti hiyo ya aibu, orodha ya mafisadi papa aliyoitangaza Dk. Slaa, na kuwaumbua vigogo hao, ndipo nchi ilitulia kidogo, maana mafisadi papa wengine ambao hawakuwemo katika orodha hiyo walitulia kidogo.
Lakini si hivyo tu, nani asiyejua kuwa ujasiri huo wa Dk. Slaa wa kuitangaza hadharani orodha ya mafisadi papa ulikisaidia chama chetu cha Mapinduzi (CCM) kuzinduka usingizini na kuanza kuishinikiza serikali kupambana na ufisadi?
Ni katika kipindi hicho ndipo CCM ilianza kukurupuka na kuibuka na misamiati ya 'kuvuana magamba'; hata kama ilikuja kugundulika baadaye kuwa (magamba hayo kama akina "Chenge" hayakuvuliwa yakaishia kiunoni), ule ulikuwa ni usanii mtupu!
Sasa hivi kumeibuka wimbi la machawa, si viongozi wa dini wala wale wanaojiita wanaharakati na wasomi, wengi wao sasa wanafanya kazi ya upambe na uchawa, wamefikia hata kukejeli hoja za viongozi wa vyama vya upinzani, wamejipa kazi hii ya hovyo bila kujua umuhimu wa vyama vya upimzani katika harakati za ukombozi.
Watu hawa "machawa" hawajui chama tawala kinapokaa muda mrefu madarakani hugeuka mkoloni au wakala wa wakoloni, hawaelewi kuwa njia ya kuondokana na ukoloni huo nikuvipa nafasi vyama vya siasa vya upinzani kushughulika na ukoloni huo.
Kwa vyovyote vile, tupende au tusivipenda vyama vya siasa vya upinzani, tunapaswa kuvipongeza kwa kazi nzuri na ngumu walizonazo kuueleza umma ukweli juu ya ufisadi na maovu yanayofanywa na watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa ndani ya CCM na serikalini.
Ni hoja yangu kwamba, kwa kuwa miaka mingi imeshapita tangu itangazwe orodha ile ya aibu ya vigogo mafisadi, Watanzania wanahitaji itangazwe orodha nyingine mpya ya mafisadi; maana hali bado na imeongezeka kuwa mbaya zaidi kuliko hata ilivyokuwa mwaka 2008.
Kwiyeya Singu. 0784977072
0 Comments