Header Ads Widget

WALIMU WA TAALUMA S/M NA SEKONDARI WAMSHUKURU PROF. MUHONGO MJADALA UBORESHAJI ELIMU



Na Shomari Binda-Musoma 


WALIMU wa taaluma wa shule za msingi na sekondari wamemshukuru mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Profesa Sospeter Muhongo kwa kuleta mjadala ( Dialouge) wa uboreshaji  ufundishaji na uelewa wa wanafunzi kuongeza ufaulu.


Wakitoa shukurani zao leo machi 25,2025 ikiwa ni siku ya kwanza ya majadiliano hayo yatakayofanyika kwa siku 3 walimu hao wa shule za Musoma Vijijini wamesema wamekuwa wapya na majadiliano hayo yamewasaidia.


Wakizunguma mara baada ya maelezo ya watoa mada ya uboreshaji waadhiri kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam ( UDSM) wamesema mbunge Muhongo amekuwa na maono ya mbali katika jambo hilo.


Wamesema kutokana na mabadiliko ya muongozo wa mitaala ya elimu katika ufundishaji yapo mambo muhimu ambayo wameyapata ambayo yatakwenda kuwasaidia wanafunzi kupata ufaulu mzuri.


Mmoja wa walimu hao Malima Musa kutoka shule ya sekondari Bwasi amesema kwenye uboreshaji wa eneo la ufundishaji wamejifunza namna ya kuwasaidia wanafunzi darasini na kuelewa kile wanachofundishwa ili kufanya vizuri kwenye masomo.


Amesema suala la kutoa motisha kwa wanafunzi wanaofanya vizuri kwenye mihula ya mitihani ili kuongeza juhudi kwa wengine.


Mwalimu huyo amesema wamejadiliana pia suala la kufatilia tabia nzuri za wanafunzi na wale wenye tabia mbaya zikiwemo za utoro kurekebishwa kwa kuwashirikisha wazazi na jamii inayozunguka shule.


" Ntumie nafasi hii kutoa shukurani nyingi kwa mheshimiwa mbunge Profesa Sospeter Muhongo kwa kutuletea mjadala huu tunaojadiliana hapa leo.


" Kila mwalimu hapa amefurahishwa na majadiliano haya na imani yetu yanakwenda kuongeza ufaulu kwenye shule zetu ndani ya jimbo zima la Musoma Vijijini",amesema.


Mwalimu Fabian Eronje kutoka shule ya msingi Rwanga amesema baadhi ya viongozi wa kisiasa wamekuwa na vitisho kwa walimu ikiwa ni pamoja kushinikiza walimu kuhama kwenye maeneo yao jambo linaloshusha ari ya ufundishaji na kuomba eneo hilo kuangaliwa.


Mmoja wa waliotoa mada kwenye mjadala huo Dk.George Kahangwa amesema walimu wakiamua na majadiliano waliyoyapata mabadiliko makubwa yanakuja Musoma Vijijini na kuongeza ufaulu.


Amesema walimu wamepewa dhamana ya kuwasaidia wanafunzi kwenye ufundishaji na wanapaswa kufanya hivyo kwa kushirikiana na wazazi,walezi na jamii inayozunguka shule.


Katika siku ya kwanza ya majadiliano yamewahusisha licha ya walimu wa shule za msingi na sekondari kikao cha pili kiliwashirikisha waratibu wa elimu wa Kata 21pamoja na watendaji wa Kata ( WEO)


Dk.Zabron Kengera akizungumza na watendaji wa Kata na maafisa elimj Kata amesema ujio wa majadiliano hayo yamekuja kutokana na kufanya vibaya kwenye matokeo ya elimu Musoma Vijijini na kutafuta ufumbuzi.


Amesema kushuka kwa elimu na kufanya bibaya kila mmoja anahusika wakiwemo watendaji wa Kata na afisa elimu Kata hivyo ni muhimu kuwa na majadiliano na kuacha kunyoosheana vidole.


Kesho machi 26,2025 majadiliano hayo yataendelea ambapo saa 3 asubuhi hadi saa 6 yatawashirikisha walimu wakuu wa shule za msingi na kuanzia saa 8 mchana hadi saa 11 jioni utakuwa mijadala kwa wakuu wa shule za sekondari.


Mwisho.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI