Na Gabriel Kilamlya Habari na Matukio DaimaAPP NJOMBE
Wakati serikali mkoani Njombe ikizindua maadhimisho ya wiki ya misitu duniani Wananchi mkoani hapa wametakiwa kutumia maonesho hayo kupata elimu ya kuongeza thamani mazao ya misitu kwa kuwa asilimia kubwa ya mapato katika mkoa yanatokana na misitu.
Akizindua maadhimisho hayo mkuu wa wilaya ya Njombe Juma Sweda kwa niaba ya Mkuu wa mkoa anasema kwa kuwa wakazi wengi uchumi wao unategemea misitu ni vyema wakafika kupata elimu ya misitu katika maonesho hayo kwani itawasaidia kukuza biashara ya mazao ya misitu.
Seleboni Mushi ni Mkurugenzi msaidizi Idara ya misitu na Nyuki wizara ya maliasili na utalii ambaye anasema Pamoja na maadhimisho hayo kuhusisha wiki ya upandaji miti lakini wananchi wanayo fursa ya kunufaika na shughuli zinazoendelea zikiwemo za utoaji elimu ya Wanyama Pamoja na misitu.
Halmashauri ya wilaya ya Njombe kupitia ofisa maliasili wake Ahmad Maguo anasema wanachokifanya katika maonesho hayo kwa sasa ni kuhakikisha wakulima wa misitu na wadau wanapata elimu ya namna ya kuongeza thamani ya misitu.
Wanyama mbalimbali waliopo katika viwanja vya sabasaba mjini Njombe kwenye maonesho hayo wakiwemo Simba wameonekana kuwa kivutio kikubwa kwa wakazi wa Njombe
Kilele cha wiki ya misitu na Upandaji miti kinatarajiwa kufikia tamati hapo machi 21 mwaka huu chini ya waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa.
0 Comments