Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima App Dodoma
SHEIKH wa Mkoa wa Dodoma, Alhaji Dkt. Mustapha Shaban Rajabu, amekosoa tabia za wanawake wanaojipamba kinyume na maagizo ya Mungu, akisema ni muhimu kuhifadhi maadili ya dini katika jamii.
Katika hotuba yake baada ya ibada ya Eid ul-Fitr iliyofanyika katika msikiti wa Gadafi, alieleza kwa kusisitiza kwamba wanawake wengi sasa wameacha kufuata njia sahihi za kuvaa na kujipamba, hali ambayo inasababisha kuharibika kwa maadili.
Sheikh Rajabu ametaja kuwa wanawake wanaojipaka kope, nywele bandia, na kujichubua kwa kujiongezea mwangaza ni sawa na kujipaka uchafu, akiongeza kuwa hali hiyo inaathiri ibada zao.
“Katika dini ya Kiislamu, wanawake wanapaswa kuvaa mavazi yanayositiri mwili kwa ufasaha. Ikiwa mwanamke atakuwa na sehemu kubwa za mwili wazi, hiyo inamfanya kuwa kama yupo uchi, " Amesema
Aidha, amesisitiza kwamba si wanawake pekee walio na jukumu hili; wanaume pia wanapaswa kuheshimu sheria za mavazi.
Amekemea wanaume wanaovaa mavazi yanayoonesha maumbile yao, akisema kuwa ni kinyume cha maadili na inawafanya kuwa machukizo mbele za Mungu.
“Dini inakataza hilo na wanaume hao wanachukizwa na Mungu,” ameongeza.
Sheikh Rajabu amehimiza jamii nzima kuzingatia maadili ya Kiislamu kwa kujitambua na kuwa mfano mzuri.
“Ni jukumu letu sote kuhifadhi heshimae na hadhi zetu kama waumini , " Amesema Sheikh
Amesema kuwa ili kudumisha amani na umoja, ni lazima tuzingatie mafundisho ya dini katika maisha yetu ya kila siku.
Mwisho
0 Comments