Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.
MKUU wa Mkoa wa Simiyu Kenani Kihongosi amefungua Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), wilaya ya Bariadi na kuwataka vijana kupendana, kujituma, kujenga Mahusiano kwenye Siasa na kuacha kubeba Wagombea.
Ameyasema hayo wakati akifungua baraza hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Bariadi Mji, ambapo amewataka kupendana, kutoumizana wala kufurahia maanguko ya vijana wenzao.
"Vijana pendaneni, dumisheni Mahusiano...Siasa ni Mahusiano, tengenezeni Mahusiano, zuieni midomo yenu kuropoka na kusemasema kwa watu...lazima mjifunze kupendana na msipende watu kuharibikiwa, tuwe watu wa kutengeneza baraka kwa watu, tuwe timu moja yaani timu Samia" amesema Kihongosi.
Kihongosi amesema serikali ya Dk. Samia Suluhu Hassan inawaamini vijana ambapo hadi sasa vijana wengi wamepewa nafasi serikali kutokana na utii wao kwa viongozi wa Chama na serikali.
Awali Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wilaya ya Bariadi, Tinana Masanja amewaahidi vijana kuendeleza mshikamano huku akiwataka kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo Udiwani na Ubunge.
Mwenyekiti huyo pia amemuomba Mkuu wa Mkoa (Kihongosi) kuzielekeza Halmashauri kuweka Mkakati mzuri wa kuwawezesha vijana kupata miradi ya Maendeleo ili waweze kujikwamua kimaendeleo.
Mwisho.
MWENYEKITI wa UVCCM wilaya ya Bariadi, Tinana Masanja (wa pili kushoto) akizungumza kwenye Baraza la UVCCM lililofanyika ukumbi wa Bariadi Mji, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Kenan Kihongosi, na kulia ni Katibu wa UVCCM wilaya ya Bariadi Hussein Kim.
0 Comments