Header Ads Widget

SERIKALI YASAINI MKATABA WA MAJI WA BILIONI 119.9.

 

Na Moses Ng'wat, Tunduma.

Serikali imeendelea na juhudi zake za kuboresha huduma za maji kwa wananchi, baada ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa Tunduma-Vwawa wenye thamani ya shilingi bilioni 119.9

Hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya mwaka kati, mjini Tunduma na  kushuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Maji, Juma Aweso na  Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

Akitoa taarifa ya Mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, alisema kuwa mradi huo

utatekelezwa na mkandarasi kutoka kampuni ya CCECC ya China kwa fedha kutoka serikali ya Tanzania.

Alisema  utahusisha ujenzi wa chanzo cha maji (intake) kwenye Mto Momba, kituo cha kuchakata na kutibia maji (Treatment Plant), mtandao wa mabomba ya kusambaza maji, matenki ya kuhifadhi maji, pamoja na ununuzi na ufungaji wa pampu za maji.

Alisema chanzo hicho kitakuwa na uwezo wa kuchukua maji lita 21,506,000 kwa siku, na kituo cha kuchakata maji kitaweza kuzalisha lita 20,000,000 kwa siku.

Vilevile, ujenzi wa mtandao wa mabomba utahusisha mabomba yenye kipenyo cha kati ya 100mm hadi 600mm, na matenki yatakayohifadhi lita 5,000,000 – Uwanjani/Uhuru, lita 3,000,000 – Ikana na lita 2,000,000 – Nkangamo. 

Pia, alisema mradi huo utahusisha ujenzi wa ofisi kwa ajili ya uendeshaji na usimamizi wa mradi, na ununuzi wa vitendea kazi mbalimbali.

Akizungumza baada ya utiaji saini, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, alisema kuwa utekelezaji wa mradi huu ni sehemu ya ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa mkoa wa Songwe.

Alisisitiza kuwa mradi huo utakuwa chachu ya maendeleo kwa mki wa Tunduma katika Wilaya ya Momba na mji wa Vwawa katika Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Aweso, alizungumzia umuhimu wa mradi kwa wananchi wa Tunduma, akisema kuwa mradi huu utatatua changamoto kubwa ya maji katika mji wa Tunduma.

Alimpongeza Mbunge wa Tunduma, Silinde, kwa juhudi zake katika kushinikiza utekelezaji wa mradi huu, akisema kuwa ni vigumu kupata viongozi wanaojitolea kwa dhati kuleta maendeleo.

Aweso pia alimtaka mkandarasi kufanya kazi kwa kuzingatia mkataba na alionya kuwa atawajibika endapo atachelewesha utekelezaji.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Momba, Elias Mwandobo, alifafanua kuwa upatikanaji wa maji katika mji wa Tunduma ni asilimia 45.2, na mradi huu utakuwa muarobaini wa tatizo hilo, kwani utahakikisha kuwa mji huo unapata huduma ya maji kwa wingi na ubora.

Aweso alisema kuwa Mradi huo awali ulipangwa kutekelezwa kwa fedha za wafadhili wa nje, lakini baada ya ushauri wa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, sasa utatekelezwa kwa fedha za ndani, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kudhibiti utegemezi wa nje na kuimarisha uchumi wa ndani.

Kwa upande wa Silinde, alieleza shukrani zake kwa Serikali ya Rais Samia, akisema kuwa mradi huu utaboresha maisha ya wananchi wa Tunduma na kusaidia kuondoa changamoto za maji kwa wananchi wa Tunduma na maeneo ya jirani.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI