Header Ads Widget

ONYO KWA WANANCHI WA MANISPAA YA BUKOBA KUHUSU UTUNZAJI WA TAKA.

 




Na Shemsa Mussa -Matukio Daima               _ Kagera 


Wananchi wa Manispaa ya Bukoba, Mkoani Kagera, wamepewa onyo kali kuhusiana na tabia ya kutunza taka ndani ya kaya zao na katika maeneo ya biashara.

Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu kuu wa Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera Daktari Peter Mkenda, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Daktari Mkenda amesisitiza kuwa tabia hii ni hatari kwa afya za wananchi na ameonya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wale watakaobainika kuendeleza utaratibu huo.

 Amefafanua kuwa manispaa hiyo imeimarisha mfumo wa ukusanyaji taka ambapo magari yanapaswa kuzoa taka kwa muda uliopangwa, ingawa ugumu unakuja pale wananchi wanaposhindwa kutoa taka kwa wakati.

"Taka hazipaswi kukaa zaidi ya masaa 48 katika kaya au maeneo ya biashara," amesema Mkenda.

 "Baada ya muda huo, taka zinaanza kuoza, kutoa harufu mbaya na kuvuta wadudu wanaosambaza magonjwa, hivyo kuleta hatari kubwa kwa jamii."

Aidha, Mganga Mkuu huyo amewakumbusha wananchi kutekeleza wajibu wao kwa kuhakikisha wanapeleka taka zao kwenye magari ya kuzoa taka, huku akisisitiza kuwa sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2009 itatumika kuwadhibiti wale wanaokiuka kanuni hizo. 

Kuhusiana na ushuru wa taka, Mkenda amesisitiza umuhimu wa kulipa ushuru wa usafi wa mazingira, ambao ni shilingi elfu 2,000 kwa mwezi.

 Ameongeza kuwa ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha kuwa hakuna taka zilizobaki kwenye kaya zao, kwani zinachangia pakubwa katika kuenea kwa magonjwa.

katika kipindi hiki cha mvua, ameonya kuhusu kuhatarisha afya kutokana na matumizi ya maji yasiyo salama yanayotokana na mito ambayo inabeba uchafu.

 Amewataka wananchi kuzingatia kanuni za afya, ikiwemo kuzuia matumizi ya maji kutoka vyanzo ambavyo siyo sahihi.

"Mito inabeba uchafu wa kila aina na matumizi mabaya ya maji yanaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko kama vile kipindu pindu," amesisitiza. Daktari Mkenda

Aidha amewakumbusha historia ya magonjwa ya kuharisha na kutapika ambayo hujitokeza mara nyingi baada ya mvua nyingi, na akaonya kwamba ni viashiria vya magonjwa kama kipindu pindu.

Amewasihi wananchi kuchukua tahadhari kwa kudumisha usafi, kunywa maji yaliyochemshwa, kutumia maji ya bomba, kula vyakula vya moto, na kuwa na mazoea ya kunawa mikono mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa mbalimbali. 

Hata hivyo amesema  kuwa ni muhimu wananchi kufuatilia taarifa zinazoelekeza afya kutoka kwenye tovuti za wizara ya Afya na vyombo vya habari ili kuwa na ufahamu sahihi kuhusu masuala ya kiafya.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI