Na Matukio Daima App, Kibaha
MAKAMU wa Rais Dk Philip Isdor Mpango anatarajiwa kuzindua mbio za Mwenge kitaifa Mkoani Pwani Aprili 2 mwaka huu kwenye uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya juu ya uzinduzi huo amesema kuwa maandalizi ya uzinduzi yanaenda vizuri.
Kikwete amesema kuwa tayari Makamu wa Rais ameshathibitisha kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo wa mbio za Mwenge kwa mwaka 2025.
"Kwa vitu vilivyobakia niwaombe mhakikishe vinafika kwa wakati ili kila kitu kiwe kwenye sehemu yake na bado tutaendelea kuangalia maandalizi ili siku hiyo mambo yawe mazuri,"amesema Kikwete.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa maandalizi yako vizuri ambapo hadi Machi 29 mambo mengi yatakuwa yamekamilika.
Kunenge amesema kuwa huduma zote zitapatikana kuanzia suala la afya, vyoo, maji, taa kubwa, umeme ambapo kutakuwa na jenereta endapo umeme utakatika.
Amewataka wananchi wa Mkoa huo na mikoa jirani na Watanzania kwa ujumla kujitokeza siku hiyo ili kuweka historia ya Pwani kuzindua mbio za Mwenge Kitaifa.
MWISHO.
0 Comments