Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App Dodoma
MKURUGENZI Mtendaji wa shirika la umeme nchini (TANESCO ) amesema kuwa kukatikatika kwa umeme kunatokana na kuzidiwa kwa gridi ya Taifa kutokana na ongezeko la watumiaji.
Hayo yameelezwa leo Machi 26,Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo,Mhandisi Gissima Nyamohanga wakati akieleza mafanikio na mwelekeo wa Shirika hilo kuelekea miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita.
Ameeleza kuwa shirika lina mipango ya kutumia teknolojia ili kuboresha upatikanaji wa umeme, ikiwa ni pamoja na kuwezesha wateja kununua tokeni moja kwa moja.
Kuhusu kununua umeme kutoka nje, amesema sababu ni kijiografia, hasa katika maeneo magumu kufikika.
"Mfano wa Sumbawanga, akisema kuwa ni bora kununua umeme kutoka Zambia kuliko kuacha watu waendelee kuteseka," Amesema.
Mkurugenzi huyo pia amesisitiza kuwa shirika linatarajia kuhakikisha ifikapo mwaka 2027, kila Mtanzania, hata wale wa maeneo ya pembezoni, wanapata umeme wa ndani.
Sambamba na hilo ametaja sababu za kukatika kwa umeme katika treni ya mwendakosi (SGR) huku likidai lipo mbioni kuanzisha Mkoa maalumu kwa ajili ya kushughulikia changamoto za umeme katika treni hiyo.
Amesema Mpango wa Shirika ni SGR kuwa Mkoa ili kuweza kutatua changamoto na watakuwa na Meneja Uratibu ambaye atakuwa akishughukia mradi huo pekee ambaye atakuwa na timu maalumu.
"Timu maalumu ambayo kazi yake ni kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika,"amesema Mkurugenzi huyo.
Mwisho
0 Comments