Na Shomari Binda-Musoma
MBUNGE wa jimbo la Musoma Vijijini Profesa Sospeter Muhongo ametoa wito kwa wananchi na taasisi za umma na binafsi kufika bustani ya miche ya miti TFS kuchukua na kupanda kipindi hiki cha mvua.
Katika taarifa yake iliyotolewa leo machi 21,2025 kupitia ofisi yake amesema miche ya kivuli,mbao na matunda imeoteshwa ya kutosha kupitia TFS hivyo ni wakati wa kuchukua na kupanda.
Muhongo amesema miti ina umuhimu mkubwa katika utunzaji wa mazingira na kulinda uoto wa asili kwenye maeneo
Amesema kupitia bustani hiyo iliyopo Musoma mjini miche hiyo inatolewa bure hivyo hakuna sababu za kutochukua na kupanda
Mbunge huyo amesema kwa taasisi zikiwemo shule za msingi na sekondari wanatakiwa kupeleka maombi kwenye halmashauri ili waweze kusaidiwa usafiri wa kufikisha miche hiyo kwenye maeneo yao.
" Upandaji wa miti ina umuhimu mkubwa katika utunzaji wa mazingira ili kuondokana na ukame ni wito wangu kwa taasisi na wananchi tukachukue na kupanda.
" Pale kwenye bustani ya TFS iliyopo Musoma mjini ipo miti ya kivuli,mbao na matunda itakayo tusaidia kwenye maeneo yetu na inatolewa bure",amesema.
Amesema idadi ya miche hiyo ni mingi na ameshafanya mawasiliano na wahusika hivyo watakaofika mapema watapata miche mingi zaidi.
Ameongeza kuwa miche kama ya mbao na matunda itasaidia kwenye uchumi na ile ya kivuli maeneo ya taasisi na hata kwenye makazi inasaidia licha ya kulinda na kuhifadhi mazingira.
0 Comments