Na Shomari Binda-Musoma
DIWANI wa Kata ya Mukendo manispaa ya Musoma Abasi Chamba ameandaa Iftar na kufikisha ujumbe kwa jamii kuwa na upendo na kushikamana wakati wote.
Ujumbe huo ameutoa jana machi 29,2025 nyumbani kwake baada ya tukio hilo la kufuturisha lililowashirikisha wakazi wa Kata ya Mukendo,jamii ya watu wa Musoma na wageni mbalimbali.
Amesema hakuna jambo lililo bora kwenye jamii kama kuwa na upendo na kushirikiana kwenye masuala mbalimbali bila kuweka utofauti na kubaguana.
Chamba amesema upendo ambao jamii imeuonyesha kwenye kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan wanapaswa kuendelea nao hata katika kipindi cha miezi mingine.
" Ndugu zangu nawadhukuru sana kwa upendo mliouonyesha kwangu kwa kufika katika Iftar hii tuliyoiandaa na familia yangu na marafiki zangu walionipa ushirikiano.
Upendo huu tuendelee nao na kuendelea kushirikiana hata kwenye matukio mengine kwenye jamii tunapoishi pasipo kubaguana",amesema.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi( CCM) Wilaya ya Musoma mjini Benedict Magiri amesema jambo alilofanya diwani huyo la kuikutanisha jamii pasipo kubagua imani za kidini ni jambo jema linalopaswa kuigwa na kila mmoja.
Amesema suala la upendo aliloliongelea ni ujumbe ambao kila mmoja akiushika jamii haiwezi kutofautiana.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu,Malezi na Mazingira ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Musoma mjini Asha Muhamed akizungumza kwa niaba ya Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya hiyo Taifa Mgore Miraji amesema mjumbe huyo ametoa shukurani kwa wote waliohudhuria kwenye Iftar hiyo.
Amesema Mgore kama mke wa diwani huyo ameona namna jamii ilivyoonyesha upendo kwa kufika kwenye tukio hilo kwani wameacha majukumu yao.
Awali akitoa salamu za Sheikh wa Wilaya ya Musoma Abubakar Mukama Sheikh wa Kata ya Kamnyonge Amani Kapama amesema suala la kufuturisha ni ibada na kuikumbusha jamii kutenda ibada mbalimbali katika kutengeneza mapokezi mazuri kesho mbele ya Mwenyezi Mungu.
Amesema kila mwanadamu anapaswa kutenda mambo mema kwenye jamii na kile alichokifanya diwani Abasi Chamba ni mafano mzuri wa kuigwa.
0 Comments