Na Matukio Daima Media,Mufindi
Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Mufindi, Jasmin Ng’umbi, amepongeza hatua ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Amos Makala, kuongoza harambee ya ghafla kwa ajili ya kumsaidia mjumbe wa Baraza Kuu la Wanawake wa Chadema (BAWACHA) Taifa, Sigrada Mligo, aliyejeruhiwa na mlinzi wa makamu mwenyekiti wa Chadema Taifa John Heche mkoani Njombe .
Kuwa katika mkutano mkubwa wa hadhara wa CCM uliofanyika Machi 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Mashujaa mjini Mafinga, Makala aliongoza zoezi la uchangiaji kwa wanachama wa CCM na wananchi waliohudhuria, ambapo kiasi cha shilingi milioni 1.5 kilipatikana.
Kuwa mchango huo ulitolewa na Wana CCM wote wakiongozwa na Makala mwenyewe MNEC Salim Abri Asas,mwenyekiti CCM mkoa wa Iringa Daud Yassin, Wabunge , wananchi na Wana CCM wote .
Kuwa tendo hilo limeibua hisia mbalimbali, hususan kwa wanawake wa Mufindi Vijana na makundi mbali mbali huku Vijana kupitia mjumbe huyu wa kamati ya utekelezaji wilaya Jasmin Ng’umbi amesifu hatua hiyo kuwa ni kielelezo cha uongozi wa CCM unaozingatia utu na mshikamano wa kitaifa bila kujali itikadi za vyama.
Ng’umbi alisema kuwa hatua hiyo ya Amos Makala inadhihirisha dhamira ya CCM ya kutanguliza utu mbele, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kaulimbiu yao ya "Kazi na Utu – Tunasonga Mbele".
Alisema kuwa siasa ni chombo cha maendeleo na mshikamano wa jamii, hivyo ni muhimu kwa viongozi wa vyama mbalimbali kushirikiana kusaidia jamii bila kubagua itikadi.
Kwani katika hotuba yake, Makala alisisitiza kuwa CCM itaendelea kuwa chama kinachoangalia maslahi ya wananchi wote, bila kujali tofauti za kisiasa.
Alisema kuwa tukio hilo la kuchangia kwa hiari limetoa somo muhimu kuhusu mshikamano na upendo miongoni mwa Watanzania, hasa wakati wa changamoto.
NO REFORM, NO ELECTION HAINA NGUVU MBELE YA CCM
Pamoja na tukio hilo la huruma, Makala pia alitumia jukwaa hilo kueleza kwa kina jinsi kauli mbiu ya "No Reform, No Election" ya Chadema isivyo na nguvu mbele ya CCM.
Alisema kuwa chama hicho kimejipanga kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao unafanyika kwa haki na uwazi, huku kikiendelea kushinda kwa kishindo kwa sababu ya utekelezaji wa sera madhubuti za maendeleo zinazoendelea kubadilisha maisha ya Watanzania.
Makala alibainisha kuwa serikali ya CCM, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imeonyesha mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali, zikiwemo elimu, afya, miundombinu, na uchumi wa kidigitali.
Alisisitiza kuwa Watanzania wanatambua jitihada hizo na hawawezi kuunga mkono mbinu za Chadema za kutaka kuzuia uchaguzi kwa kigezo cha mabadiliko wanayotaka kabla ya kushiriki.
Aliongeza kuwa mfumo wa kidemokrasia nchini unatoa nafasi kwa vyama vyote kushiriki uchaguzi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo, na kwamba ni jukumu la vyama vya siasa kujipanga kushiriki kikamilifu badala ya kutafuta visingizio vya kutoshiriki.
SAMIA NA CCM WATAIBUKA KIDETE UCHAGUZI MKUU
Katika hotuba yake, Makala pia alieleza kwa kina sababu zinazomfanya Rais Samia Suluhu Hassan na CCM kuwa na nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi mkuu ujao.
Alitaja sababu kuu kuwa ni pamoja na rekodi nzuri ya serikali ya CCM katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii, usimamizi mzuri wa miradi ya kimkakati, na kuimarika kwa diplomasia ya kimataifa ambayo imeongeza fursa za uwekezaji na biashara kwa nchi.
Alisema kuwa Rais Samia amethibitisha kuwa kiongozi mahiri anayejali wananchi, ambapo amehakikisha miradi mikubwa kama ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, na uboreshaji wa huduma za afya na elimu vinaendelea kwa kasi.
Aidha, sera za kiuchumi zimewezesha ukuaji wa biashara ndogo na za kati, hali ambayo imeleta manufaa kwa wananchi wengi, hususan wanawake na vijana.
Makala alisema kuwa CCM itaendelea kuwa chama chenye dira na mwelekeo sahihi kwa maendeleo ya Tanzania, huku akiwataka wananchi waendelee kuiamini na kuipa kura ili iendelee kuongoza na kutekeleza ajenda za maendeleo kwa manufaa ya wote.
Kwa upande wake Jasmin Ng’umbi alisema kuwa hotuba ya Makala imewatia moyo Wana CCM na wasio Wana CCM wilaya ya Mufindi kuwa wananchi wameshuhudia namna CCM inavyothamini utu na mshikamano, na kwa matendo kama haya ya Amos Makala, wana uhakika kuwa chama hicho kitaendelea kuwa chaguo la wananchi katika uchaguzi ujao.
Mwisho
0 Comments