Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenan Kihongosi akiongea na Walimu kwenye Kliniki ya kusikiliza kero za Walimu iliyoandaliwa na CWT.
Na Mwandishi wetu, Matukio Daima App.
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Kenan Kihongosi leo 18 Februari, 2025 amezindua kliniki maalumu ya kusikiliza kero mbalimbali za Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Kusekwa Wilayani Bariadi.
Kliniki hiyo ya kusikiliza kero za Walimu imeratibiwa na Chama cha Walimu Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais menejiment ya utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Fedha, pamoja na Tume ya mtumishi wa Walimu TSC.
Akizingumza wakati wa ufunguzi huo, Kihongosi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia utekelezaji wa Kliniki ya kusikiliza na kutatua Kero za Walimu.
Amewataka Walimu kutumia fursa ya Kliniki ya kutatua changamoto kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Amewataka Viongozi Mkoani Simiyu kuhakikisha wanatoa huduma kwa kuzingatia haki bila uonevu kwa Mwalimu yoyote ndani ya Mkoa wa Simiyu.
Amewasisitiza walimu kuepuka migogoro na migomo na badala yake kutafuta suluhu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa kistaarabu.
Naye Makamu wa Rais wa Chama cha Walimu Tanzania Mwl. Selemani Ikomba amewataka Walimu Mkoani Simiyu kuimarisha umoja na mshikamano ili kurahisisha upatikanaji wa suluhu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Kliniki ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za Walimu Mkoani Simiyu itafanyika kuanzia Tarehe 18 hadi Tarehe 2 Machi, 2025.
Mwisho.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenan Kihongosi.
0 Comments