Na Matukio Daima media
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema ongezeko la joto hapa nchini limesababishwa na kushuka kwa jua la utosi.
Taarifa iliyotolewa na TMA leo Februari 12,2025 imeelezwa kwamba maeneo yanayoathiriwa na joto hilo zaidi ni yale yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
"Hali hii imesababishwa na kusogea kwa jua la utosi sambamba na upungufu wa mvua unaojitokeza katika maeneo hayo.
"Kwa kawaida vipindi vya jua la utosi nchini hufikia kilele mwishoni mwa Novemba kila mwaka wakati linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa).
"Jua la utosi huambatana na hali ya ongezeko la joto kwa sababu uso wa Dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine," ilisomeka hivyo sehemu ya taarifa hiyo.
Imebainisha kwamba kati ya Februari 5 hadi Februari 11, 2025 kituo cha hali ya hewa cha Mlingano jijini Tanga kiliripoti kiwango cha juu zaidi cha nyuzi joto 36.0°C sawa na ongezeko la nyuzi joto 2.1°C ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa Februari.
"Februari 10,2025 kituo cha hali ya hewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam kiliripoti kiwango cha juu cha nyuzi joto 35.0°C hilo ni ongezeko la nyuzi joto 2.2°C.
"Katika tarehe tajwa, kituo cha Tanga kiliripoti nyuzi joto 35.1°C sawa na ngezeko la nyuzi joto 2.3°C wakati kituo cha Kibaha kilisoma nyuzi joto 35.8 °C sawa na ongezeko la nyuzi joto 3.0°C.
"Mkoa wa Kilimanjaro kituo chetu kiliripoti uwepo wa nyuzi joto 34.3°C hiyo ilikuwa Februari 9,2025 sawa na ongezeko la nyuzi joto 0.6°C," ilieleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa TMA ongezeko la unyevu angani katika kipindi hiki linalosababishwa na mvuke wa bahari hasa maeneo ya ukanda wa pwani na maeneo jirani limechangia pia mwili kuhisi joto zaidi ya viwango vinavyoripotiwa.
Vipindi vya ongezeko la joto vinatarajiwa kuendelea kujitokeza katika mwezi huu wa Februari, 2025 hususan katika maeneo ambayo msimu wa mvua za Vuli umeisha.
0 Comments