Na Fadhili Abdallah
Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa Kigoma AbdulKadri Mushi amewata viongozi wa CCM wilaya ya Kibondo kufanya ziara na kutangaza utekelezaji wa miradi mikubwa inayofanywa na serikali ya awamu ya sita ya Raisi Samia Suluhu Hassan badala ya kudandia ziara za mbunge na viongozi wengine wanaofanya ziara katika wilaya hiyo.
Mushi alisema hayo akiongoza kamati ya siasa ya mkoa Kigoma kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani humo ambapo amebainisha kuwa serikali imepeleka fedha nyingi na miradi mikubwa imetekelezwa lakini viongozi wa CCM na kamati ya siasa ya wilaya hiyo hawajatekeleza kikamilifu wajibu wao wa kuisemea miradi hiyo ili wananchi wajue serikali yao inachofanya.
Kauli hiyo ya MNEC huyo wa CCM inakuja kufuatia viongozi wa wilaya hiyo kukiri kuwa kama chama hawajafanya ziara wala mikutano ya hadhara na wananchi kuelekeza miradi hiyo na badala yake wamekuwa wakihudhuria mikutano ya ziara za mbunge wa jimbo hilo Dk.Florence Samizi na ndipo wanapata nafasi ya kuzungumza na wananchi.
Alisema kuwa kauli yake wilayani humo ni agizo kwa viongozi wote wa CCM katika kamati za siasa za wilaya katika mkoa Kigoma kuandaa na kufanya mikutano ya kwao na kuzungumza na wananchi kuelekeza kazi kubwa iliyofanywa kupitia kiasi cha shilingi Trilioni 11.5 zilizotolewa na serikali ya awamu ya sita ya Raisi Samia katika kutekeleza miradi ya wananchi mkoani humo.
Akizungumzia kauli hiyo ya Mjumbe wa halmashauri kuu ya Taifa Mwenyekiti wa CCM, Hamisi Tairo amemuomba radhi kiongozi huyo na kamati ya siasa ya mkoa iliyotembelea miradi wilayani humo na kubainisha kuwa walikumbwa na udhaifu wa kibinadamu na kwamba baada ya ziara hiyo chama wilayani humo wataanda ziara zao na kufanya mikutano ya wananchi kueleza hali ya utekelezaji wa ilani kupitia miradi iliyotekelezwa.
Kauli hiyo ya kuomba radhi ya Mwenyekiti wa CCM wilaya Kibondo inakuja baada ya Mjumbe wa NEC kukataa maneno ya utetezi ya Katibu wa CCM wa wilaya Kibondo aliyesema kuwa kuna mkutano walifanya wakati wa maadhimisho ya CCM mwaka huu ambapo Mjumbe huyo wa NEC alisema kuwa anatoa maagizo na maelekezo ya chama na hataki malumbano.
Mwisho.
0 Comments