Header Ads Widget

UWEPO WA CT-SCAN BUKOBA-RRH WAWEZESHA UPASUAJI WA AWALI WA UBONGO HOSPITALINI HAPA: DKT MAGEMBE

Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, ameeleza kufurahishwa na uwepo wa mashine ya kisasa ya CT-Scan katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera iliyowezesha Madaktari katika hospitali hiyo kuanza kutoa huduma za upasuaji wa awali wa ubongo kwa wagonjwa wa dharura.

Dkt. Magembe alitoa kauli hiyo leo, Januari 26, 2025 alipotembelea hospitali hiyo kwa ziara maalum yenye lengo la kukagua utoaji wa huduma za afya hospitalini hapo na kujionea jinsi watumishi wanavyoendelea kuchukua tahadhari katika kujikinga na Magonjwa wakiwa kazini.

“Nimefurahishwa sana na jinsi mashine ya CT-Scan inavyosaidia madaktari wetu kuanza kutoa huduma za upasuaji wa awali wa ubongo huduani kwa wagonjwa wa dharura hasa waliopata ajali na kuvuja na damu kichwani, Kwasasa wagonjwa hao wanapata huduma hapa kitu ambacho sio cha kawaida kwa hospitali ya Mkoa kutoa huduma hii, mara nyingi huduma kama hii utolewa na hospitali za Kanda au Taifa,” alisema Dkt. Magembe.

Kupitia ziara hiyo, Dkt. Magembe alitembelea pia Kitengo cha Watoto Wachanga (NCU) na kupongeza watumishi wa kitengo hicho kwa kuendelea kutoa huduma bora, kujituma na kufuata miongozo ya kitaalamu ili kupunguza vifo vya watoto wachanga.

Aidha, alitembelea Jengo la Dharura (EMD) na Kitengo cha Kusafisha Damu (Dialysis) ambapo aliwapongeza watumishi kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwataka kuendelea kutoa huduma bora kwa lengo la kuokoa maisha ya Watanzania.

Dkt. Magembe alisisitiza kuwa serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa katika kuboresha huduma za afya nchini kwa kusambaza vifaa tiba vya kisasa, kujenga hospitali mpya za wilaya, na kuanzisha vituo vya afya ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Dkt. Museleta Nyakiroto alimshukuru Dkt. Magembe kwa kutembelea hospitali hiyo na kuahidi kuwa wataalamu wa afya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba wataendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kufuata miongozo iliyotolewa na Wizara ya Afya.





 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI