Header Ads Widget

SERIKALI YASISITIZA UTEKELEZAJI WA HAKI ZA WATUMISHI WA UMMA


Na Hamida Ramadhan Matukio Daima App Dodoma 

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kusimamia mapato na malimbikizo ya madai kwa watumishi wa umma. 

Katika ufunguzi wa kikao cha 30 cha Baraza Kuu la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) jijini Dodoma, Kikwete alisisitiza kuwa Serikali haitakubali waajiri wanaoshindwa kutekeleza matakwa ya kisheria kuhusu ushirikishaji wa mabaraza ya wafanyakazi. 

“Ni muhimu kwa waajiri kufuata sheria na kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki zao na Serikali itachukua hatua stahiki dhidi ya waajiri watakaoshindwa kutekeleza wajibu wao,” amesema Kikwete.

Waziri Kikwete alikiri kwamba Serikali inatambua changamoto hizi na iko tayari kushirikiana na TALGWU kutafuta suluhisho la kudumu. 

"Tutaendelea kufanya kazi pamoja na vyama vya wafanyakazi ili kuhakikisha tunatatua matatizo yanayowakabili watumishi wa umma. Ufanisi wetu unatokana na ushirikiano na uwazi katika usimamizi wa fedha,” alisema Kikwete.


Katibu wa TALGWU, Rashid Mtima, ameeleza changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya umma, ikiwa ni pamoja na malipo ya fedha za likizo kutolipwa kwa wakati, matatizo katika malipo ya leseni kwa kada ya afya, na ucheleweshaji wa fedha za uhamisho.

 "Tunahitaji mfumo thabiti ambao utaweza kutatua changamoto hizi mara moja, ili watumishi wetu waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kwa moyo mmoja,” alisisitiza Mtima.


 Aliongeza kuwa mfumo wa PEPMIS umekuwa na dosari zinazohitaji marekebisho ili kuboresha utendaji wa watumishi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Mitaa Tanzania TALGWU  Tumaini Nyamhokya ilipongeza juhudi za Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. 

Amesema Samia Suluhu Hassan, akitaja hatua kama vile kupandisha madaraja ya watumishi, kuboresha mifumo ya kikokotoo cha mafao, na kuimarisha miundombinu ya usafiri, ikiwemo mradi wa treni ya umeme (SGR).

"Tunafarijika kuona juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya kazi, lakini bado tunahitaji kuhakikisha haki za wafanyakazi zinafikiwa kwa wakati,” alihimiza Mtima.

Kikao hicho kililenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na vyama vya wafanyakazi, na kujadili mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizopo ili kuhakikisha watumishi wa umma wanapata haki zao na mazingira bora ya kazi. 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI