Header Ads Widget

MBUNGE AMKALIA KOONI MKANDRASI KWA KUSUASUA MRADI WA MAJI MSANGANO-CHITETE



Na Moses Mg'wat, Momba.


Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, ameeleza kutoridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Msangano-Chitete katika Halmashauri ya Momba, huku akionya kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa Mkandarasi.


Mradi huo unaotekelezwa na Mkandarasi mzawa wa kampuni ya Jampta kutoka Jijini  Dar es Salaam kwa gharama ya Shilingi bilioni sita, umekuwa ukisuasua licha ya kampuni hiyo kulipwa malipo ya awali ya Shilingi milioni 800.


Mhandisi Kundo alisema, tayari serikali imelipa zaidi ya Shilingi milioni 800, lakini kazi zilizofanyika hadi sasa haziendani na thamani ya fedha hizo.


"Kumekuwa na tabia ya baadhi ya wakandarasi wazawa kuchelewesha miradi, serikali haitokubali wananchi waendelea kuteseka kwa sababu za uzembe wa mkandarasi," alisema Naibu Waziri Kundo.


Mhandisi Kundo alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Momba, Elias Mwandobo, kuhakikisha vyombo vya uchunguzi, ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),  vinachunguza matumizi ya fedha za mradi huo.


Kwa mujibu wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Momba, Mhandisi Beatus Katabazi, mradi huo wa Msangano-Chitete ulianza utekelezaji wake tangu mwaka 2023 na ulitarajiwa kukamilika Juni 2024. 


Mhandisi Katabazi alieleza kazi zilizofanyika hadi sasa ni ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita milioni moja ambao umefikia nusu tu, huku ulazaji wa mabomba ukikamilika kwa kilomita 8.5 pekee kati ya kilomita 74.9 zilizopangwa.


Alisema mradi huo unatarajiwa kuhudumia zaidi ya wakazi 30,000 kutoka vijiji nane vya Kata za Msangano na Chitete, pindi tuu utakapokamilika.


Awali Mbunge wa Jimbo la Momba, Condesta Sichalwe, alimueleza Naibu Waziri kuhusu Mkandarasi huyo  kushindwa kuzingatia muda wa utekelezaji wa mradi.


Mbunge Sichalwe alitoa shutuma kali dhidi ya mkandarasi, akidai kuwa, awali kabla ya fedha za mradi kupatikana Mkandarasi huyo alionekana mwenye nia ya dhati ya kutaka kufanya kazi, lakini baada ya fedha kupatika amekuwa ni mtu wa kutoa visingizio na kufanya mradi kuendelea kuauasua na kuzua malalamiko kwa wananchi.


Mbali na mbunge, naye Diwani wa Kata ya Msangano, Isack Sinkala, alimlalamikia mkandarasi huyo, akidai kazi zimekuwa zikisimama mara kwa mara, huku baadhi ya wafanyakazi wakionekana kama walinzi tu.


Kwa upande wake, Mkandarasi kupitia Mhandisi Mkuu wa Mradi, Kundael Mfwangavo, aliahidi kuongeza nguvu kazi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa muda uliobaki.


Naibu Waziri, Mhandisi Kundo amesisitiza kuwa serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi kwa wakati.








Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI