Akutwa akiongoza malori kwenye foleni mjini Tunduma.
Na Mose Ng'wat,Songwe.
BANGROS Sikaluzwe (37), Mkazi wa Ilolo, Wilaya ya Mbozi, amekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, kwa tuhuma za kujifanya askari wa Jeshi la Polisi Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Januari 22, 2025 na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Akama Shaabani, imeeleza kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 22, 2025, majira ya saa 7:45 usiku katika msako uliofanyika Mtaa wa Majengo, Mjini Tunduma, Wilayani Momba.
Kaimu Kammanda, Akama alisema mtuhumiwa alikamatwa akiwa anafanya kazi za usalama barabarani katika barabara ya Tunduma-Sumbawanga kwa kuyapanga malori yanayovuka mpaka wa Tunduma kuelekea Zambia na nchi nyingine za kusini mwa Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Kaimu Kamanda, mtuhumiwa huyo alikutwa akiwa amevaa sare za polisi, pia akiwa na vifaa vingine vya jeshi hilo kama, Pingu alizokuwa amezining’iniza kiunoni, Kisu cha kukunja, pamoja na Tochi aliyokuwa ameshika mkononi.
Kaimu Kamanda, Akama , alisema kuwa uchunguzi wa haraka ulibaini kuwa Bangros si askari polisi halali, bali ni mgambo aliyekuwa akijifanya askari kwa malengo ambayo bado hayajathibitishwa.
Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limewaonya wananchi kuacha tabia ya kuvaa sare za polisi au kujifanya askari, kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
0 Comments