Header Ads Widget

𝐊𝐀𝐌𝐏𝐄𝐍𝐈 𝐘𝐀 𝐊𝐈𝐇𝐈𝐒𝐓𝐎𝐑𝐈𝐀 "𝐕𝐀𝐋𝐄𝐍𝐓𝐈𝐍𝐄 𝐖𝐄𝐄𝐊𝐄𝐍𝐃 𝐆𝐀𝐓𝐄𝐀𝐖𝐀𝐘 𝐍𝐀 𝐓𝐀𝐍𝐀𝐏𝐀" 𝐍𝐃𝐀𝐍𝐈 𝐘𝐀 𝐊𝐈𝐒𝐈𝐖𝐀 𝐂𝐇𝐀 𝐒𝐀𝐀𝐍𝐀𝐍𝐄


Na Philipo Hassan - Mwanza

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Busybee imezindua Kampeni yake ijulikanayo "Valentine Weekend Gateway na TANAPA", Januari 21, 2024 jijini Mwanza, lengo likiwa ni kuhamasisha Watanzania na wasio Watanzania kutembelea Hifadhi za Taifa kipindi hiki cha msimu wa Sikukuu ya Wapendanao.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Jully Lyimo, anayeshughulikia Kitengo cha Maendeleo ya Biashara TANAPA Makao Makuu, alianza kwa kufunga rasmi kampeni ya Shangwe la Sikukuu na TANAPA iliyozinduliwa Disemba 01, 2024 Jijini Arusha.

Kamishna Lyimo alieleza mafanikio ya kampeni hiyo kwa kutaja ongezeko kubwa la watalii wa ndani: “Kampeni ya Shangwe la Sikukuu na TANAPA ilifanikiwa kuvuka lengo la awali ambalo lilikuwa ni kupata watalii wa Kitanzania na 28,000.” 

Kamishna Lyimo Aliongeza: “Jumla ya Watanzania 36,933 walitembelea Hifadhi za Taifa kuanzia tarehe (1/12/2024 hadi 5/1/2025), sawa na ongezeko la asilimia 44% ukilinganisha na Watalii waliotembelea katika kipindi kama hicho kwa mwaka jana (1/12/2023 hadi 5/1/2024).”

Akizungumzia dhima ya uzinduzi wa kampeni mpya ya Valentine Weekend Gateaway na TANAPA, Kamishna Lyimo alisema, “Leo tunazindua kampeni hii kwa Hifadhi zote 21, tunawahamasisha Watanzania wote watembelee Hifadhi zetu maana tumeandaa vifurushi rafiki vya bei nafuu vinavyomwezesha kila Mtanzania kumudu gharama za kutalii msimu wa wapendanao.”

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dr. Tutindaga Mwakijambile, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, alitoa maelezo kuhusu Kisiwa cha Saanane ambapo ni mahali pa kipekee kwa wapendanao. Mandhari tulivu, fursa za kipekee za kupumzika, na shughuli mbalimbali za kuburudisha zinazotengeneza uzoefu wa kukumbukwa milele.

Kamishna Dr. Tutindaga aliongeza, “tumejiandaa kuwahudumia wapendanao, Watalii wataweza kutembelea Kisiwa cha Saanane chenye msitu wa kijani uliosheheni miamba minene ya mawe iliyobanana, wanyama kama Swala, Nyumbu, Simba, Mamba, na Ndege wa aina mbalimbali pamoja na mandhari nzuri ya jiji la Mwanza.”

Mkurugenzi wa Kampuni ya Busybee, Baraka Nyororo, alieleza kwa upana kuhusu ushirikiano na TANAPA katika kuandaa tukio hilo adhimu katika jiji la Mwanza, ambapo Watanzania wengi wanatarajiwa kushiriki kutembelea kisiwa hicho siku ya Februari 15, 2025

Baraka alisema, “Tutaandaa tukio la Usiku mzuri kwa wapendanao ambapo watafurahia Night Excursion, Valentine Romantic Dinner, Bonfire, Games, burudani ya Muziki, matembezi ya miguu pamoja na kutazama nyota wakati wa usiku.”

TANAPA imeendelea kunadi na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika Hifadhi za Taifa nchini hasa kupitia matukio ambayo yamepelekea kupatikana kwa mafanikio yanayochangia kufanikisha adhima ya Serikali ya kufikisha watalii milioni tano (5) na mapato ya dola bilioni sita (6) ifikapo mwaka 2025.







Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI