Polisi Mkoa wa Mbeya inamshikilia mtuhumiwa Mussa Mwile (28) mkazi wa Kanyegele Wilaya ya Rungwe na wenzake kumi na nne (14) kwa tuhuma za kupatikana na mali ya wizi ambao ni unga wa sembe baada ya Gari lililokuwa likisafirisha shehena ya Unga kupata ajali.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP Benjamin Kuzaga, amesema kwamba mnamo Januari 15, 2025 majira saa mbili asubuhi katika eneo la Mlima Kanyegele Kata ya Kiwira, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe katika Barabara kuu ya Mbeya Tukuyu, Gari lori yenye namba za usajili LA10214 aina ya Freight Liner lililokuwa likiendeshwa na Dereva aitwaye Damson Vincent (35) mkazi wa Lilongwe Malawi likitokea Mbeya kuelekea Malawi likiwa limebeba shehena ya Unga wa Sembe liliacha njia na kusababisha majeraha kwa Dereva wa Gari hilo.
Kamanda Kuzaga amesema baada ya ajali hiyo, wananchi wa Kijiji cha Kanyegele na Vijiji jirani vya Mpandapanda na Igula walifika katika eneo la ajali na kuanza kuiba Unga wa Sembe uliokuwa kwenye mifuko ya kilogramu 25 ipatayo 1253 na kutoweka nayo wakitumia usafiri wa Pikipiki maarufu bodaboda.
Kufuatia tukio hilo, amesema Polisi mkoa wa Mbeya lilifanya msako na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Mussa Zacharia Mwile na wenzake 14 wakiwa na vielelezo ambavyo ni Unga wa Sembe ulioibwa mifuko 65 mizima na minne ikiwa nusu, turubai mbili za gari hiyo pamoja na Pikipiki saba zilizokuwa zikitumika kubeba na kusafirisha mali hiyo ya wizi.
Kamanda amesema pikipiki zilizokamatwa ni MC 887 CVY Kinglion, MC 511 DCW Kinglion, MC 137 EMW Kinglion, MC 326 EDK Kinglion, MC 800 BBW T-better na Pikipiki mbili ambazo hazina namba za usajili akitaja chanzo cha tukio hilo kuwa ni kujipatia kipato kwa njia isiyo halali.
Pia amesema msako unaendelea ili kuwapata watuhumiwa wengine na vielelezo huku jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa baadhi ya wananchi wenye tabia ya kukimbilia eneo la ajali pindi magari yanapopata ajali na kuanza kuiba mali kuacha mara moja kwani ni kinyume cha sheria na ni hatari kwa usalama wao.
Aidha, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wenye taarifa za mtu au watu waliohusika kuiba na kuficha mali hiyo kutoa taarifa ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria
0 Comments