Na. Philipo Hassan - Manyara.
Kamishna wa Uhifadhi, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Musa Kuji amefungua kikao kazi cha Maandalizi ya bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kikao kinachofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara uliopo eneo la Mto wa Mbu mkoani Manyara.
Kikao hicho cha siku mbili kilichoanza leo Januari 27, 2025 na kutarajia kutamatika tarehe 28.01.2025 kimelenga kufanya tathmini ya bajeti iliyopita ya mwaka wa fedha 2023/2024 na kutathmini mwenendo wa bajeti inayoelekea ukingoni ya mwaka huu wa fedha 2024/2025.
Hata hivyo wajumbe wa kikao hicho pia watajadili na kupitisha mapendekezo yatakayotumika kuandaa bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka mpya wa fedha 2025/2026 ili kuendana na kasi ya ukuaji wa sekta ya uhifadhi na utalii nchini.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho Kamishna kuji alisema “Kikao kazi hiki ni muhimu kwani kitawajengea uwezo wa kuandaa bajeti inayotekelezeka kulingana na vipaumbele vya shirika huku ikiakisi matamanio ya Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha Uhifadhi na Utalii.
Kikao kazi hicho cha maandalizi ya bajeti ya mwaka 2025/2026 kinachoendelea Ziwa Manyara ni hatua muhimu ya maandalizi ya rasilimali fedha zitakazotumika kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vitendea kazi vitakavyotumika kuimarisha Uhifadhi na kukuza Utalii kwa ajili ya mustakabali wa taifa letu.
0 Comments