Header Ads Widget

KRFA YAPATA VIONGOZI WAPYA BILA KUPINGWA

Moshi.CHAMA cha Soka Mkoa wa Kilimanjaro (KRFA) kimefanya uchaguzi wa viongozi wapya kwa nafasi mbalimbali, ambapo wagombea wote watakaoongoza kwa miaka minne wamepita bila kupingwa katika uchaguzi uliofanyika Jana jumapili, Januari 26, 2025, wilayani Moshi.

Uchaguzi huo uliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya KRFA, Jackson Kaniki, kwa usimamizi wa wajumbe kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Khalid Mohamed, ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, na Pamela Mboya, Katibu wa Kamati hiyo.

Katika mkutano huo, wajumbe 23 wamepiga kura za ndiyo kwa viongozi waliogombea nafasi tatu za Mwenyekiti, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya KRFA, huku wagombea wote wakipita bila kupingwa kwa sababu ya kukosekana wapinzani.

Isaac Munis amefanikiwa kutetea nafasi yake ya Mwenyekiti wa KRFA, huku Abdalah Thabiti na Hamad Gao wakichaguliwa kuwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.

Nafasi nyingine ya Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya KRFA imechukuliwa na Jafari Kiango, baada ya wagombea wote kupigiwa kura za ndiyo.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Munis amesema ataendeleza juhudi za kuboresha soka la Kilimanjaro.

Aidha, amemteua Prof. Daudi Mavula kuwa Makamu Mwenyekiti wa KRFA, nafasi ambayo pia inampa uanachama wa Kamati ya Utendaji ya chama hicho.

"Yeye ni Profesa na mimi sijasoma sana. Natamani nizungukwe na watu waliokwenda shule vizuri," amesema Munis. 

Ameongeza kuwa ameteua Dk. Agness Kessy kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya KRFA, akisema: "Kwa mujibu wa katiba yetu, nafasi mbili za Mwenyekiti zinatakiwa kugawanywa kwa jinsia tofauti. Naomba mnikubalie huyu ambaye nimeteua."

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya KRFA, Jackson Kaniki, amesema uchaguzi huo ulikuwa huru na haki. "Hakukuwa na upinzani kwa wagombea, hivyo kura za ndiyo zilitosha kumpitisha kila mgombea aliyekidhi vigezo," amesema Kaniki.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Khalid Mohamed, amesema uchaguzi huo umefuata taratibu za TFF kwa asilimia 100.

 "Sasa hivi uchaguzi katika mikoa unaendeshwa kwa utulivu bila vurugu. Kila mwenye haki ya nafasi hupata bila pingamizi," amesema.

Ameongeza kuwa viongozi waliochaguliwa wanapaswa kusimamia mpira kuanzia ngazi za chini hadi mashindano ya kitaifa, huku wakizingatia taratibu na kanuni zinazotakiwa ili kukuza soka kwa manufaa ya taifa na vilabu vyote.



 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI