Na Matukio Daima media
KATIKA harakati za kudumisha mahusiano mazuri kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na jamii, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Mufindi, Dickson Nathani Lutevele Villa, amemwakilisha Naibu Katibu Mkuu wa CCM Taifa, John Mongela, kwenye harambee ya ujenzi wa Kanisa la Waadventista Wasabato Lumwago na kufanikisha kupatikana zaidi ya Tsh Milioni 3.7.
Katika hafla hiyo, Mwenezi Villa alitoa mchango wa shilingi milioni 3.7 kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa kanisa hilo, hatua ambayo imepongezwa sana na waumini wa kanisa hilo pamoja na viongozi wa dini.
Wakizungumza wakati wa tukio hilo, viongozi wa Kanisa la Waadventista Wasabato walitoa shukrani zao kwa CCM kwa ushirikiano mkubwa unaoendelea kuonyeshwa katika masuala ya kijamii, hususan kuchangia maendeleo ya jamii kupitia taasisi za kidini.
Katika hotuba yake, Villa alisisitiza umuhimu wa viongozi wa dini kuendelea kuwaombea viongozi wa serikali na wa CCM.
Alieleza kuwa sala na maombi ya viongozi wa kidini ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha kwamba viongozi wa serikali wanatekeleza majukumu yao kwa hofu ya Mungu na kwa maslahi mapana ya taifa.
Aliongeza kuwa viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika kudumisha amani na utulivu wa nchi.
Alisisitiza kwamba bila amani, maendeleo hayawezi kupatikana. “Tunaitegemea sana amani hii ambayo tunaendelea kuijivunia kama taifa.
Nawaomba viongozi wa dini kuendelea kuwa chachu ya umoja na mshikamano kati ya wananchi na serikali,” alisema Villa.
Hata hivyo Villa ametumia nafasi hiyo kuhamasisha wa Wananchi Kushiriki Katika Mambo ya Maendeleo katika maeneo yao.
Mbali na wito wa maombi, Villa aliwataka wananchi wote kuhakikisha wanajitokeza kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Alieleza kuwa zoezi hilo linalotarajiwa kuanza hivi karibuni ni la msingi katika kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika maamuzi ya kidemokrasia, hususan uchaguzi ujao.
Aidha, Villa alitoa wito kwa viongozi waliochaguliwa hivi karibuni katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa weledi na ufanisi.
Alisema kuwa viongozi hao wanapaswa kuhakikisha hawamkwamishi Rais Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili yake.
Villa alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za dhati za kudumisha amani na kuleta maendeleo nchini.
Alisema kuwa CCM inaendelea kujivunia utulivu wa taifa ambao umekuwa ni msingi wa maendeleo katika sekta zote.
“Rais wetu Samia ameendelea kuwa mfano bora wa uongozi wenye maono, anayejali watu wake na anayeweka mbele ustawi wa taifa letu.
Alisema kuwa Amani hii tunayojivunia leo ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na serikali yake.
" Tunapaswa kuungana naye kuhakikisha tunadumisha amani hii kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema Villa.
Katika tukio hilo, Villa alieleza kuwa CCM itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za kijamii, hususan makanisa na misikiti, katika kuhakikisha kwamba maendeleo yanawafikia wananchi wote bila ubaguzi.
Alieleza kuwa chama hicho kinaamini katika mshikamano na ushirikiano wa dhati kati ya serikali, vyombo vya dini, na jamii kwa ujumla.
“CCM ni chama kinachojali watu wake. Tunatambua kuwa maendeleo tunayoyalenga hayawezi kufikiwa bila ushirikiano wa dhati kutoka kwa jamii nzima.
Tunawahakikishia kuwa tutaendelea kushirikiana na kila mmoja wenu kuhakikisha tunajenga taifa lenye nguvu na lililojaa matumaini,” alisisitiza Villa.
Harambee ya ujenzi wa Kanisa la Waadventista Wasabato Lumwago ilikuwa ishara ya mshikamano mkubwa kati ya CCM na jamii.
Katika tukio hilo liliwakutanisha viongozi wa dini, wanasiasa, na wananchi kwa lengo la kufanikisha maendeleo ya kijamii na kiroho.
Hotuba ya Villa ilibeba ujumbe mzito wa mshikamano, amani, na maendeleo huku akisisitiza kuwa viongozi wa kidini wana nafasi muhimu katika kuhakikisha taifa linaendelea kuwa na amani, ambayo ni msingi wa maendeleo.
Aidha, aliwakumbusha wananchi na viongozi wa serikali za mitaa umuhimu wa kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kuinua hali ya maisha ya Watanzania wote.
Kwa mchango wake wa fedha na ujumbe wa matumaini, Villa alionesha kwa vitendo nia ya CCM ya kuendelea kushirikiana na jamii kwa karibu, huku akisisitiza dhamira ya chama hicho ya kuona maendeleo yanawafikia kila Mtanzania.
0 Comments