Header Ads Widget

UFAHAMU MDOGO WA MADHARA YA KUTOMALIZA DOZI KUNAVYOHATARISHA AFYA YA WATANZANIA WENGI.

 

  Mwanahabari Zacharia Nyamoga akifanya mahojiano na Bibi Isabella Kigae kutoka Kijiji cha Idunda kuhusu ufahamu juu ya madhara ya kutomaliza Dozi. Picha na Gelvas Edmund


Na Zacharia Nyamoga, Iringa


KUTOKUWA na uelewa wa kina kuhusu athari za kutomaliza dozi ya dawa kama ilivyoshauriwa na mtaalamu wa Afya miongoni mwa wagonjwa kunahatarisha afya ya wananchi wengi, tatizo linalochangia kuongezeka kwa usugu wa dawa na kutishia mifumo ya afya nchini.


Kwa mujibu wa Sera ya Afya ya Tanzania ya mwaka 2007 inalenga kuboresha afya ya wananchi kwa kuhakikisha wanapata huduma bora za kinga, tiba, na elimu ya afya, kifungu cha 5.1 cha sera hiyo kinasisitiza umuhimu wa kuelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya dawa ikiwa ni pamoja na madhara ya kutomaliza dozi kama inavyoshauriwa na wataalamu.


Aidha katika Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura ya 219, inaelekeza kuwa dawa zote zilizoidhinishwa lazima zitumike kwa kufuata maelekezo ya daktari au mtoa huduma ya afya. 


Licha ya mwongozo huu, changamoto za kutomaliza dawa bado ni kubwa, hasa kwa wagonjwa wanaotumia dawa za muda mrefu kama wale wenye kifua kikuu (TB) au wanaoishi na virusi vya UKIMWI.


CHANZO CHA CHANGAMOTO HII.


Ili kufahamu zaidi, nilizuru Kijiji cha Idunda, Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa, ambapo nilikutana na Bibi Isabella Kigae na Abeli Chotamasege ambao walitoa maoni tofauti kuhusu changamoto hii.

 

  Mwanahabari Zacharia Nyamoga akifanya mahojiano na Bibi Isabella Kigae kutoka Kijiji cha Idunda kuhusu ufahamu juu ya madhara ya kutomaliza Dozi. Picha na Gelvas Edmund


Bibi Isabella alisema, “Kijiji chetu hatuna zahanati kabisa, tunategemea ya Kijiji cha Kimala, lakini hata huko hakuna dawa. Inatulazimu kutembea zaidi ya kilometa 50 hadi Kituo cha Afya cha Kidabaga kwa umri huu, kurudi mara kwa mara ni ngumu, miguu yangu huvimba sana.” alisema Bibi Isabella 


Abeli Chotamasege akizingumza sababu za wagonjwa wengi kutomaliza dozi kama inavyoshauliwa na wataalamu wa Afya.


Kwa upande wake, Abeli Chotamasege alisema uchumi mdogo huwafanya wagonjwa kununua dawa nusu dozi. “Hakuna anayependa maradhi shida ipo kwenye uchumi unaandikiwa dawa za elfu 40 au zaidi, ambayo kwetu ni kubwa tunaishia kununua kidogo kidogo kwenye maduka ya dawa,” alisema.


Maneno haya yanaakisi hali halisi ya maisha ya watu wa vijijini, ambapo uchumi na ukosefu wa huduma za karibu ni changamoto kuu.


ATHARI ZA KUTOMALIZA DOZI


           DKT SYLVIA MAMKWE, MGANGA MKUU WA MKOA WA IRINGA



Dkt. Sylvia Mamkwe, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, anasema tatizo hili lina madhara makubwa. “Wagonjwa wengi huacha dozi njiani punde wanapojihisi nafuu kutomaliza dawa kunaweza kusababisha usugu wa dawa (drug resistance), ambapo vimelea vinajifunza kupinga dawa, na matibabu yanakuwa magumu zaidi, hii inaweza kusababisha magonjwa sugu kama vile 'multi-drug resistance' au 'extensively drug resistance,' hali inayoongeza changamoto kwa mgonjwa na mfumo wa afya,” amesema Dkt. Sylvia 


MAPENDEKEZO YA WATAALAMU.


Wadau wa afya wanasisitiza kuwa elimu endelevu ni muhimu katika kutatua changamoto hii. Dkt. Faith Mwakasege wa Chuo Kikuu cha Ruaha anapendekeza kutumia njia bunifu kama vikundi vya kijamii, vipindi vya redio, na mafunzo kwa viongozi wa jamii ili kuwafundisha wananchi kuhusu athari za kutomaliza dozi za dawa.


Aidha, Dkt. Mohamed Mwenga wa USAID Afya Yangu anapendekeza kusogeza huduma za afya vijijini, kuboresha usambazaji wa dawa, na kuimarisha upatikanaji wa bima ya afya kwa wote hatua hizi, anasema zitakuza upatikanaji wa matibabu na kupunguza changamoto zinazowakabili wagonjwa wengi.


HITIMISHO


Tatizo la kutomaliza dozi linaathiri si tu afya ya mgonjwa mmoja mmoja bali pia mfumo mzima wa afya, Elimu kwa jamii, kuboresha miundombinu ya afya, na kupunguza gharama za dawa ni hatua muhimu za kupunguza athari za tatizo hili. Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha tunafuata ushauri wa wataalamu wa afya ili kujenga jamii yenye afya bora na salama.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI