Na Matukio Daima media,Mwanza
Wakati Taifa likipanga kusherekea uhuru wa Tanganyika Desemba 9, Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) inaishukuru serikali ya awamu ya sita chini wa Uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa kwenye taasisi yetu.
Akiongea jijini Mwanza jana, Mkurugenzi Mkuu wa TASHICO Eric Hamissi amesema kuwa uwekezaji huo unaohusisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ndio ambao unaoijengea Kampuni hiyo uwezo wa kujiendesha kibiashara na kutanua wigo wa uendeshaji wake.
“Bila uwekezaji huu mkubwa, huu mchakato wa kubadilisha jina la Kampuni usingukwa na maana yoyote na badala yake ingekuwa ni kama kubadilisha chupa tu wakati mvinyo ni ile ile,” alisema.
Aliongeza: ““Ningependa kutumia fursa hii kuwashukuru wadau wote ambao wamekuwa wameshirikiana nasi kwa njia mbalimbali katika safari yetu hadi sasa.”
Hamissi alitabanaisha kuwa mara tu baada ya Uhuru, Shirika lilikuwa chini ya Uangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini Serikali iliendelea kutoa huduma ya usafiri kwa njia ya maji katika maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa kwa kutumia meli tatu (3) za MV. Victoria (1960) na M.V. Clarias (1961) katika Ziwa Victoria; na M.V. Liemba (1913) katika Ziwa Tanganyika.
“Hata hivyo, Serikali ilinunua meli mpya saba (7): Ziwa Victoria: M.V. Butiama, (1980), MT. Ukerewe (1983), M.V. Serengeti (1988), Ziwa Tanganyika: M.T. Sangara (1981), M.V. Mwongozo (1982) wakati kwenye Ziwa Nyasa ni M.V. Songea, M.V. Iringa,” alisema.
Alisema kuwa MSCL ilianzishwa chini ya Sheria ya Makampuni sura 212, tarehe 08 Disemba 1997 kutoka Shirika la Reli (TRC). Lakini rasmi MSCL ilianza kazi tarehe 01, Agosti, 1999 ikiwa na meli 14 na boti moja,
“Hadi mwaka 2015, Kampuni ilikuwa inamiliki meli 14 ambazo kati ya hizo Meli 9 zipo katika Ziwa Victoria, Meli 3 na Boti 1 katika Ziwa Tanganyika na Meli 2 katika Ziwa Nyasa,” alisema.
Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa kwakuwa meli nyingi zilikuwepo kwa muda mrefu, hivyo zilichakaa na kupelekea nyingine kusimamishwa kutoa huduma kutokana ili kulinda usalama wa chombo na usalama wa maisha ya watu na mali zao ambapo mwaka 2017, Kampuni ilikuwa na meli tano tu zilizokuwa zinatoa huduma; Ziwa Victoria kulikuwa na MV.Umoja, MV Clarias wakati Ziwa Tanganyika kulikuwa na MV Liemba, MT Sangara na kwenye Ziwa Nyasa kulibaki na MV Songea.
MPANGO WA SERIKALI KUFUFUA MELI
Hamissi alisema kuwa kutokana na kudorora kwa Kampuni katika utoaji wa huduma pamoja na umuhimu wake kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya maziwa makuu na uchumi wa nchi kwa ujumla, Serikali iliamua kufufua huduma za usafiri kwa njia ya maji kwa abiria na mizigo katika maziwa hayo.
“Mwaka 2018, Serikali ilianza kutenga fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi mikubwa minne katika Ziwa Victoria na Mwaka 2022, Serikali iliielekeza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kukabidhi meli tatu (3) za MV. Mbeya II, MV. Njombe na MV. Ruvuma kwa MSCL ambazo hadi sasa meli hizo zinaendelea kutoa huduma katika Ziwa Nyasa,” alisema.
AWAMU YA KWANZA YA MIRADI (2018 – 2023)
Alisema kuwa awamu hiyo ya kwanza ilihusisha miradi minne mojawapo ikiwa ni ujenzi wa Meli mpya ya MV Mwanza “Hapa Kazi Tu”, yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria, wakati tulifanya ujenzi wa Chelezo - ambayo inatumika kama kitanda cha meli kabla haijashushwa katika maji wakati ikiundwa. na meli ya MV. Mwanza iliundwa kwenye Chelezo hii,
“Kwenye awamu hii tulifanya ukarabati wa Meli za MV Victoria – Iliitwa New Victoria Hapa Kazi Tu ambayo inasafiri kutoka Mwanza Kwenda Bukoba kupitia Kemondo na ilianza kutoa huduma mwaka 2020 pamoja na kulifanyika ukarabati wa MV Butiama – iliitwa New Butiama Hapa Kazi Tu inasafiri kila siku kutoka Mwanza kwenda Nansio, kisiwa cha Ukerewe,” alisema.
AWAMU YA PILI YA MIRADI (2023 – 2028)
“Awamu hii inahusika miradi nane (8) ampapo Ziwa Victoria miradi Minne (4) ambayo ni ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 katika Ziwa Victoria, ukarabati mkubwa wa meli MV. Umoja inayobeba mabehewa katika Ziwa Victoria. Mkataba wa mradi huu ulisainiwa tarehe 15 Juni, 2021 na kukamilika Septemba, 2023. Kwa sasa meli inaendelea kusafirishamizigo tangu Oktoba 2023,” alisema.
Aliongezea kuwa katika awamu hii walifanya vilevile ukarabati wa meli ya uokozi na kuvuta matishari ya MT. Ukerewe katika Ziwa Victoria. Mkandarasi anaendelea na ukarabati pamoja na ukarabati mkubwa wa meli ya kubeba shehena ya mizigo (mafuta) ya MT. Nyangumi iliyopo Ziwa Victoria Mkataba wake ulisainiwa tarehe 17 Novemba 2023.
Alisema kuwa kwenye Ziwa Tanganyika miradi minne (4) ilitekelezwa ambayo ni ukarabati wa meli ya kubeba shehena ya mafuta ya MT. Sangara katika Ziwa Tanganyika na ujenzi wa meli mpya ya kubeba shehena ya mizigo kiasi cha tani 3,500 katika Ziwa Tanganyika.
“Tuliweza vile vile kutekeleza ujenzi wa Kiwanda cha Kujengea Meli katika Ziwa Tanganyika pamoja na Ukarabati mkubwa wa meli ya MV. Liemba katika Ziwa Tanganyika. Mkandarasi ameshakabidhiwa mradi anaendelea nao vizuri,” alisema.
Alisema kuwa miradi hii ya awamu ya pili kwa ujumla inafikia Dola za Kimarekani 326,027,480.02 ambayo ni sawa na Shilingi 893,315,295,254.8 kwa kubadili dola kwa $1 = 2,740.
KUBADILI JINA NA KUWA TASHICO
Mkurugenzi Hamissi alisema kuwa tarehe 18. 11. 2024 Kampuni ya Huduma za Meli ilibadili jina rasmi na kuwa KAMPUNI YA MELI TANZANIA (TASHICO). “Mabadiliko haya yanaletwa na mapinduzi yanayofanywa katika Sekta ya Usafiri kwa njia ya maji na Serikali ya Awamu ya Sita ya Mhe. Dokta. Samia Suluhu Hassan.”
Alisisitiza: “Mabadiliko haya pia ni kutokana na mipango ya TASHICO kuwa na meli katika bahari ya hindi ambayo upembuzi yakinifu umeanza na meli hizo zitakuwa zikisafiri mashariki ya Kati pamoja na mashariki ya mbali kama vile China n.k.”
Alisema kuwa mchakato umeanza wa kuwa na meli zetu Bahari ya Hindi, mwaka huu wa fedha 2024/2025 unafanyika upembuzi yakinifu na mwaka wa fedha 2025/2026 ujenzi unaanza wa meli moja ya mizigo.
“Hata hivyo kutakuwa na meli za mizigo zitakazofanya safari zake kwenda katika visiwa vya Comoro.”
Alisema kuwa hadi kufikia mwaka 2030, TASHICO inategemewa kuwa na wafanyakazi 5,000 ili kuweza kukidhi mahitaji ya meli tulizonazo.
“Lengo ni kuendelea kujitanu ili kuweza kutoa mchango mkubwa katika pato la taifa kupitia usafiri kwa njia ya maji. Nchi yetu imezungukwa na maji kuanzia baharini hadi maziwa makuu kwahiyo kwahiyo Serikali inakwenda kuleta mapinduzi katika sekta hii kupitia TASHICO,” alisema
Sababu za Kubadilisha Jina
Alisema kuwa uamuzi wa kubadilisha jina la taasisi yetu kutoka MSCL na kuwa TASHICO umelenga kuleta mabadiliko makubwa katika utambulisho wetu na kuweka msingi imara kwa ajili ya ukuaji wa kampuni.
“Tunaamini kuwa jina jipya litatusaidia kwenye yafuatayo: Kuwa na utambulisho wa kitaifa wenye nguvu: Jina TASHICO linatutambulisha wazi kama kampuni ya Kitanzania yenye mizizi imara katika nchi yetu tofauti na jina la awali. Jina jipya linaonyesha kujitolea kwetu katika kuendeleza uchumi wa Tanzania na kuunganisha maeneo mbalimbali ya nchi yetu na nchi jirani na Kuongeza ushindani katika soko la kimataifa: Kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa Kampuni wa kutanua wigo wa shughuli zake kutoka kwenye ukanda wa maziwa makuu hadi bahari kuu, tunaamini Jina hili jipya litaifanya taasisi yetu kujiendesha kiushindani wa kibiashara tofauti na jina la awali. Aidha, jina hili jipya lina mvuto ambao utasaidia kutufungulia milango mipya katika soko la kimataifa. Jina hili litatusaidia kuvutia wateja wapya, washirika wa kimataifa na wawekezaji. Tumejiandaa kuingia katika masoko mapya, ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa mizigo ya jumla, mafuta, na bidhaa nyinginezo.
Alisema kuwa jina jipya litaakisi wigo mpana wa shughuli zetu: Tofauti na jina la awali, ambalo lilikuwa halitoa taswira ya shughuli za msingi za taasisi yetu, TASHICO linaonyesha wazi kuwa taasisi yetu inajishughulisha mahususi na shughuli za usafirishaji kwa njia ya maji (yaani usafiri wa meli).
Faida Zinazotarajiwa Kutokana na Jina Jipya
“Ni imani kuwa jina jipya litaleta faida nyingi kwa kampuni yetu, wafanyakazi wetu, wananchi na Taifa kwa ujumla. Baadhi ya faida hizo ni pamoja na: Kuongezeka kwa mapato: Kwa kuwa jina TASHICO litatusaidia kuvutia wateja wapya na kupanua wigo wa biashara yetu, tunatarajia kuona ongezeko kubwa la mapato.
Pamoja na hayo amesema kubadilishwa kwa jina la taasisi yetu kunatarajiwa kubadilisha utamaduni wa utendaji kazi wa taasisi yetu (cooperate culture) kutoka hali ya kutoa huduma na kuwa na utamaduni wa kujiendesha kibiashara. Hii itasaidia kubadilisha mtazamo wa watumishi wa taasisi na wadau wake na hivyo kujielekeza katika utendaji unaojikita kwenye ushindani wa kibiashara ambao utasaidia kuongeza ufanisi na ubora wa huduma zinazotolewa na Kampuni yetu kwa wateja wake.
Kuimarisha uchumi wa nchi:
Alisema wataweza kuongeza mchango wao katika sekta ya usafirishaji, tutakuwa tukichangia katika kukuza uchumi wa nchi yetu na kuboresha maisha ya wananchi.
Kuongeza ufanisi na ubunifu:
Jina jipya litatuchochea kuwa na ubunifu zaidi na kutafuta njia mpya za kuboresha huduma zetu. Tutaendelea kuwekeza katika teknolojia mpya ili kuhakikisha kuwa tunatoa huduma bora zaidi kwa wateja wetu, alisema.
TIJA YA TASHICO KWA UCHUMI WA TAIFA
Serikali Kuimarisha usafiri wa njia ya maji katika maziwa ya Tanzania—Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria, na Ziwa Nyasa—kupitia uwekezaji wa serikali katika ujenzi wa meli za mizigo na abiria kunaweza kuwa na faida nyingi kwa Watanzania na kwa taifa kwa ujumla.
Kuboresha Uchumi na Biashara ya Kikanda
Kuongeza Biashara ya Ndani na Nchi Jirani: Maziwa haya yanapakana na nchi kadhaa za Afrika Mashariki na Kati. Uwekezaji unaofanywa na Serikali kwa TASHICO katika ujenzi wa meli za mizigo utawezesha Tanzania kuimarisha biashara na nchi jirani kama Uganda, Kenya, Zambia, Burundi, DRC na Malawi, jambo ambalo litapanua soko kwa bidhaa za ndani na kuleta fedha za kigeni.
Kupunguza Gharama za Usafirishaji: Usafiri wa maji ni wa gharama nafuu ukilinganisha na usafiri wa barabara au anga. Mizigo inayotoka bandari ya Dar es Salaam kuelekea Uganda kwa njia ya barabara hutumia muda mrefu kuliko ukitumia Ziwa Victoria kupitia Mwanza, mfano kutoka Bandari ya Dar es Salaam (Tanzania) hadi Kampala (Uganda) kwa barabara ni Kilometa 1,717 lakini kutoka Dar es Salaam hadi Kampala kupitia Ziwa Victoria ni Kilomita 1,470.
Halikadhalika kwa Mizigo inayokwenda Kalemie, DRC ni rahisi kupita Ziwa Tanganyika kuliko kupita njia ya Barabara aidha upite Tunduma kisha Zambia Kilomita 1,922 au upitie Burundi kilomita 1,877. Ila kutoka Dar es Salaam kwenda Kalemie (DRC) kupitia Bandari ya Kigoma ni Kilomita 1,375.
Kuimarisha Miundombinu na Maendeleo ya Kiuchumi
Kuongeza Uwekezaji wa Miundombinu: Serikali imevutia uwekezaji katika miundombinu inayozunguka bandari za maziwa haya, ikiwemo barabara, reli, na bandari kavu. Hii imechangia maendeleo ya kiuchumi kwa maeneo yanayozunguka maziwa haya.
Kukuza Sekta ya Utalii:
Alisema kuwa kupitia uwekezaji huu Serikali itavutia watalii wa ndani na wa nje wanaotaka kusafiri kupitia maziwa haya. Kwa mfano ukarabati wa MV. Liemba ambao unaendelea huko Kigoma, utakapo kamilika meli hii itatumika pia kama kivutio cha utalii jambo ambalo italeta mapato zaidi kwa serikali na kwa jamii zinazozunguka maziwa hayo.
Kuongeza Ajira na Maendeleo ya Jamii
Alisisitiza kuwa ujenzi wa meli, pamoja na uendeshaji wake, utahitaji wafanyakazi wa fani mbalimbali, kama vile mafundi, wahandisi, mabaharia, na wahudumu. Hii itasaidia kupunguza ukosefu wa ajira, hasa kwa vijana. Kwa sasa TASHICO ina wafanyakazi zaidi ya 250 lakini hadi kufika mwaka 2030, TASHICO inataraji kuwa na wafanyakazi 5,000
Kuboresha Huduma za Kijamii:
Usafiri wa maji utarahisisha usafirishaji wa bidhaa muhimu kama vile chakula, dawa, na vifaa vya elimu kwenda maeneo ya pembezoni ambayo ni vigumu kufikika kwa usafiri wa barabara. Hii itasaidia kuboresha hali ya maisha ya jamii hizo.
Usalama na Ufanisi katika Usafirishaji
Alisema kuwa usafiri wa maji unabeba mizigo mingi kwa mara moja, hivyo kusaidia kupunguza msongamano na uharibifu wa barabara. Kwa mfano meli ya MV. Umoja iliyopo Ziwa Victoria ina uwezo wa kubeba Tani 1,200 ambayo ni sawa na malori 40 na MT. Sangara ya Ziwa Tanganyika ina uwezo wa kubeba mafuta lita 410,000 ambayo ni sawa na karibu malori 12 ya mafuta
Kuboresha Usalama kwa Wasafiri:
Aliongeze kuwa Serikali kupitia Uwekezaji huu wa meli za abiria unalenga kutoa usafiri salama na wa uhakika kwa wakazi wanaoishi kwenye mwambao wa maziwa haya ambapo kuna wale wanaosafiri kati ya mji na mji ndani ya nchi na hata nchi jirani.
Kuimarisha Muungano na Mshikamano wa Kikanda
Mkurugenzi Hamissi alisema Usafiri wa njia ya maji unaimarisha uhusiano kati ya Tanzania na nchi jirani zinazotumia maziwa haya, hivyo kuimarisha mshikamano wa kikanda na kuwezesha urahisi wa kubadilishana bidhaa na huduma.
Kuunganisha Jamii za Maziwani:
Kwa kuwekeza kwenye usafiri wa maji, amesema serikali inaboresha upatikanaji wa huduma kwa jamii zinazoishi karibu na maziwa, na kuimarisha mawasiliano na ushirikiano kati ya mikoa ya Tanzania inayozunguka maziwa haya nan chi za jirani.
Mwisho
0 Comments