Header Ads Widget

SEKTA YA MIFUGO KUCHANGIA KIWANGO KIKUBWA CHA UCHUMI



Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App Dodoma


SEKTA ya Mifugo Inachangia kwa kiwango kikubwa uchumi wa Taifa, huku ikiwategemeza mamilioni ya Watanzania kupitia ajira, chakula, na kipato. 


Hata hivyo, changamoto ya magonjwa ya mifugo imeendelea kudhoofisha uzalishaji, hali inayohitaji hatua za haraka na za kimkakati. 


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Ashatu Kijaji, amesisitiza jukumu kubwa la wataalam wa sekta hiyo kuwahamasisha wafugaji kuhusu umuhimu wa chanjo za mifugo ili kufanikisha lengo la kitaifa la kuchanja asilimia 70 ya mifugo. 


Dkt. Kijaji ameyasema hayo katika kikao kazi cha uzinduzi wa uhamasishaji wa kampeni ya chanjo za mifugo kitaifa uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, Desemba 18, jijini Dodoma.


Waziri huyo amesema kuwa hatua hiyo inalenga kuimarisha sekta ya mifugo, kuongeza uzalishaji, na kuboresha biashara ya mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi. 


Aidha, amesisitiza kwamba ushirikiano kati ya wafugaji na wataalam ni muhimu ili kufanikisha kampeni hiyo.


“Niombe ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ili kuweza kuwafikia wafugaji kwa upana mkubwa zaidi. Ushirikiano huu utasaidia kuleta mafanikio makubwa katika sekta hii muhimu,” alisema Dkt. Kijaji.



Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe, amesema kuwa utekelezaji wa kampeni hiyo ni jambo la kitaalamu, na ndiyo sababu wameamua kuwakutanisha wafugaji na wataalam ili kuhakikisha wanashirikiana kikamilifu.


 Prof. Shemdoe ameongeza kuwa kampeni hiyo inalenga kutoa elimu kwa wafugaji juu ya umuhimu wa chanjo, huku ikibeba malengo ya kuongeza uzalishaji wa mifugo na kufanikisha biashara ya mazao ya mifugo.


Uzinduzi huo umebeba kauli mbiu isemayo: "Tokomeza Magonjwa ya Mifugo ili kuongeza Uzalishaji na kuwezesha Biashara ya Mifugo na Mazao yake ndani na nje ya Nchi." Kauli mbiu hii inasisitiza umuhimu wa afya bora ya mifugo kama msingi wa ukuaji wa sekta ya mifugo nchini.


Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imedhamiria kuhakikisha wafugaji wanapata elimu sahihi na huduma bora ili kufanikisha lengo la kuwa na mifugo yenye afya bora, ambayo itachangia kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI