Jeshi la polisi mkoa wa Mbeya linamshikilia binti mmoja aliyetajwa kwa jina la Anna Mwakilima [24] mkazi wa Mbuyuni Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya akituhumiwa kwa wizi wa mtoto mwenye umri wa miezi miwili na nusu aitwaye Juliana Kiwelo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP Benjamin Kuzaga, ameeleza kuwa Desemba 22, 2024 Aneth Mgaya [20] mkazi wa Kijiji cha Mwakaganga Wilayani Mbarali aliibiwa mtoto wake aitwaye Juliana Kiwelo (miezi 2.5) na mwanamke ambaye alimfahamu kwa sura kwani siku moja kabla ya tukio yaani Desemba 21, 2024 saa kumi jioni mtuhumiwa alifika nyumbani kwa Aneth Mgaya na kuomba hifadhi ya kulala siku moja kwa madai kuwa ametokea Mbeya Mjini na yupo Ubaruku Mbarali kwa ajili ya biashara ya kuuza vitenge.
Kuzaga anasema siku iliyofuata yaani Desemba 22, 2024 majira ya saa moja asubuhi Aneth Mgaya aliamka na kutoka nyumbani kwake kwenda kununua vitafunio katika eneo la jirani na kumuacha mtuhumiwa na watoto wawili lakini baada ya kurudi hakumkuta mtuhumiwa wala watoto wake.
Amesema ufuatiliaji ulifanyika na kufanikiwa kumpata mtoto mmoja aitwaye Grace Petro [07] Mwanafunzi wa Darasa la awali katika Shule ya Msingi Charles Hope iliyopo Mwakaganga ambaye ni mdogo wake Aneth Mgaya ambaye alikutwa ametelekezwa jirani na Chuo cha Ufundi Wilaya ya Mbarali.
Kamanda Benjamin Kuzaga anasema jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya liliendelea na ufuatiliaji wa kina ambapo Desemba 28, 2024 saa 12 jioni katika Kijiji cha Mbuyuni kilichopo Kata ya Mapogoro, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Anna Mwakilima [24] mkazi wa Mbuyuni akiwa na mtoto Juliana Denis Kiwelo akiwa hai.
Mama mzazi wa mtoto amemtambua na amekabidhiwa na mtuhumiwa amekutwa akiwa amemuandikishia kitabu cha afya ya mtoto chenye jina la Patricia Christopher Mkula.
Hata hivyo Polisi Mkoa wa Mbeya chini ya kamanda Kuzaga inatoa wito kwa jamii kuchukua tahadhari kwa baadhi ya wananchi ambao bado wanaendelea na uhalifu kuacha mara moja kwani uhalifu haulipi hivyo ni vyema wakatafuta kazi nyingine ya kufanya hususani kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka 2024 na mwanzo wa mwaka mpya 2025. Pia linaendelea kutoa wito kwa wananchi kuwa makini na watu wanaofika kwenye makazi yao, waache kuwapokea na kuwakaribisha bila kujiridhisha na kupata taarifa za mahali walipotoka.
0 Comments