Header Ads Widget

WAKULIMA WAWEZESHAJI WAGAWIWA BAISKELI KUSIMAMIA ZAO LA PAMBA

 


Na Mwandishi wetu, Matukio daima App.



WAKULIMA wawezeshaji zaidi ya 200 wilayani Meatu Mkoani Simiyu wamegawiwa Baiskeli na serikali ili waweze kusimamia na kuongeza tija ya uzalishaji wa zao la Pamba.


Mpango huo unakuja ikiwa ni sehemu ya Utekelezaji wa Mkakati wa Bodi ya Pamba wenye lengo la kuwafikia wakulima na kuwapa Elimu ya Kilimo bora cha Pamba.


Akikabidhi Baiskeli hizo, Mkuu wa Wilaya ya Meatu Fuadhi Ngatumbura alisema zana hizo zimetolewa ili kuleta tija na kuongeza uzalishaji wa Pamba katika wilaya hiyo.


Amesema wilaya ya Meatu ndio kinara wa Uzalishaji wa Pamba katika Mkoa wa Simiyu na Taifa kwa ujumla na kwamba Kuna muunganiko wa wakulima na Maafisa Ugani.


"Kwa muunganiko wa wakulima, Maafisa Ugani na Elimu wanayopata tunaweza kuvuka lengo la uzalishaji...kwani takwimu za uzalishaji zinaongezeka licha ya changamo ya hali ya hewa, zana za kilimo na uelewa mdogo wa baadhi ya wakulima" amesema.


Amewataka Maafisa Ugani wa serikali na wakulima wawezeshaji kutimiza wajibu ili kulinda dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan aliyeanza kujenga mazingira rafiki kwa wakulima ya kutoa zana za kilimo pamoja kuweka ruzuku kwenye sekta hiyo.


"Serikali ina mategemeo makubwa sana na wakulima wawezeshaji, ni rahisi mkulima kukuelewa kuliko kiongozi wa serikali nanyi mmebeba Mafanikio ya Pamba...muendelee kutoa huduma na kuwafikia wakulima kwa wakati" amesema Ngatumbura.


Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya alipiga marufuku wakulima kulisha Mifugo au kuuza mbegu za Pamba ambazo zinazalishwa kwa gharama kubwa na serikali.



Mkaguzi wa Pamba wilaya ya Meatu, Renatus Philbert amesema bado kuna changamoto ya huduma za Ugani kwa wakulima ambapo Bodi ya Pamba, Serikali na Wadau wa Pamba wameamua kuwekeza katika huduma za Ugani katika msimu wa 2024/25.


Ameeleza kuwa katika uwekezaji huo, serikali imeajiri Maafisa Ugani 2000 kwa kushirikiana na wadau kupitia Mpango wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) na wilaya ya Meatu imepewa Maafisa Ugani 116.


"Tumekuwa na wakulima wawezeshaji 208 ambao wanafanya kazi kwa kujitolea, serikali imeona iwapatie Baiskeli ambazo zitasaidia kuwafikia wakulima na kusaidia utoaji wa huduma za ugani ambao watashirikiana na Maafisa Ugani wa BBT kwa kila kijiji" alisema.


Sage Lugembe ambaye ni Mkulima mwezeshaji kutoka Nzanza Amcos amesema usafiri wa Baiskeli waliopita utasaidia kuwafikia wakulima kwa lengo la kutoa Elimu ya upandaji, matumizi ya mbolea na unyunyiziaji.


Naye Mutama, mkulima mwezeshaji kutoka Kijiji Cha Mwamanungu ameeleza kuwa Baiskeli hizo zitawasaidia kutimiza majukumu yao ya kusimamia na kuongeza uzalishaji wa Pamba.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI