NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR - MATUKIO DAIMA APP
CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kupitia Kituo chake cha Kikanda cha Umahiri katika Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani Zanzibar (ZARTSA) kimetoa mafunzo ya usalama barabarani kwa madereva na makondakta wa gari za abiria wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, wakati wa kufungua mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja leo, Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini 'B' Othman Ali Maulid, amesema uzowefu unaonesha kuwa mwendo kasi unachangia ajali nyingi za barabarani na kuwataka wadau hao kufuata kanuni na sheria za usalama barabarani, alama za barabarani ili watumiaji wa barabara wabaki kuwa salama.
Ameeleza kuwa Serikali imeweka miundombinu ya barabara ili kuhakikisha sekta ya usafiri nchini inaimarika na kuwasihi kuitumia miundombinu hiyo kama ilivyokusudiwa pasi na kuathiri watumiaji wengine wa barabara.
"Tunapoendesha vyombo vyetu kwa mwendo wa wastani itasaidia kupunguza ajali na endapo zitatokea hazitakua na athari kubwa kama itakavyokua ajali ya mwendo kasi.” alisema Mkuu huyo.
Aidha amewataka waliopatiwa mafunzo hayo kuwa mabalozi wazuri wa elimu hiyo ili kuiweka Zanzibar katika hali ya usalama kwani Zanzibar bila ya ajali inawezekana.
Naye Mkuu wa Kituo cha Kikanda cha Umahiri katika Usalama Barabarani - NIT, Ndg. Godlisten Msumanje amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo madereva na makondakta katika matumizi salama ya barabara.
Alieleza kuwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kinatoa mafunzo mbalimbali kwaajili ya kuandaa wataalam wa sekta ya Usafirishaji, kufanya tafiti na kutoa ushauri elekezi.
Amesema uzoefu unaonesha kuwa tatizo la ajali za barabarani ni janga la kitaifa hivyo elimu inahitajika zaidi ili kuondoa tatizo hilo
“tumekuja Zanzibar kutoa elimu ya usalama barabarani kwa makundi mbalimbali ili kuhamasisha matumizi sahihi ya barabara.” Alisema.
Akiwasilisha mada ya Sheria na alama za barabarani mkufunzi kutoka NIT Mhandisi Mhoja Roheje, amesema madereva wengi wanaenda kinyume na taratibu na sharia za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuendesha bila kuwa na leseni ya udereva, kutokagua vyombo vyao kabla ya kuingia barabarani pamoja na kutofuata alama za barabarani.
“Iwapo utakua na leseni lakini unajaza abiria kupitia kiasi bado hujafuata sheria jambo ambalo linahatarisha usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara na kuiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa adhabu kali ili kukomesha tabia za madereva na makonda wanaofanya makosa hayo.”alisema Mhandisi huyo
Kwa upande wa madereva na makonda waliyopatiwa mafunzo hayo wameahidi kuyafanyia kazi yale yote waliojifunza na kuziomba taasisi husika kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
0 Comments